WASHINGTON, MAREKANI
RAIS Donald Trump yuko kikaangoni. Hiyo ndiyo kauli ambayo inatakiwa kuzungumzwa kwa sasa kutokana na uchunguzi unaoendelea dhidi ya iliyokuwa timu ya kampeni ya Rais Donald Trump, kama ilikuwa na uhusiano wa karibu na serikali ya Russia, pamoja na tuhuma za uvunjaji wa sheria na ukiukwaji wa Katiba anaotuhumiwa Rais huyo.
Aidha, Trump anatuhumiwa kutumia nafasi yake ya urais kama nyenzo ya kutangaza biashara zake za majengo na mengineyo pamoja na kuwakaribisha viongozi wa kidiplomasia wa serikali kwenye majengo yake, likiwamo Trump Tower.
Uchunguzi huo unaendeshwa na Mwendesha Mashtaka Maalumu, Robert Mueller, ambaye anamchunguza Rais Donald Trump iwapo alizuia sheria kufuata mkondo wake.
Hali kadhalika, Trump amekuwa akitumia mitandao ya jamii na kushambulia ripoti zilizoelezea kuwa mwendesha mashtaka maalumu anachunguza madai ya kuwa Rais aliingilia kati uchunguzi uliokuwa unafanyika dhidi yake.
Hata hivyo, Rais Trump amepinga madai hayo, baada ya kuandika kwenye ukurasa wake mtandao wa Twitter, “Walifanya majumuisho ya uongo kuhusiana na taarifa ya Russia, hawakukuta ushahidi wowote, na sasa wananituhumu kwa kuzuia sheria kufuata mkondo wake katika madai ya uongo. Vizuri.”
Aidha, Mueller pia anachunguza mahusiano ya mkwe wa Rais, Jared Kushner, ambaye pia ni mshauri wake wa juu, kuhusiana na fedha na biashara zake.
Robert Mueller ni mmoja kati ya walioajiriwa kuwafuatilia magaidi katika miaka ya 1990 kwa ajili ya Shirika la Upelelezi la FBI na baadaye alisaidia kufungua kesi ya jinai dhidi ya mshukiwa wa tukio la kigaidi la Septemba mwaka 2011, aliyejulikana kwa jina la Zacarias Moussaoui.
Mwendesha mashtaka mwingine ni yule aliyeongoza kikundi maalumu cha uchunguzi cha serikali kuu kilichofuatilia kashfa ya Shirika la Enron mwaka 2000.
Wa tatu amesimamia utetezi wa kesi zaidi ya 100 za jinai mbele ya Mahakama Kuu, akiwa katika nafasi ya naibu mtetezi mkuu kwenye Idara ya Sheria.
Hawa ni kati ya wanasheria wenye uwezo mkubwa wa timu ya Mwendesha Mashtaka Maalumu, Robert Mueller, ambaye ameajiriwa hivi karibuni kuchunguza kuingilia kati kwa Russia katika uchaguzi wa urais nchini Marekani mwaka jana.
Na pia kuchimbua iwapo kulikuwa na ushirikiano wowote kati ya serikali ya Moscow na timu ya Kampeni ya Donald Trump kabla hajachaguliwa kuwa rais Novemba, mwaka jana.
Kwa mujibu wa msemaji wake, Peter Carr, Mueller amewaajiri wanasheria 13 tangu alipoteuliwa mwezi mmoja uliopita, na anatarajia kuongeza wengine kadhaa.
Msemaji huyo amebainisha kuwa, mchunguzi mwingine ni Peter Zeidenberg, ambaye aliwahi kutumikia kama msaidizi maalumu wa upande wa utetezi mwaka 2005, kufuatia uchunguzi wa aliyekuwa msaidizi wa Ikulu ya White House, Scooter Libby, inaweza ikawahusisha makumi ya wafanyakazi wa FBI na idadi kubwa ya waendesha mashtaka.
Ajira za watu wenye uwezo mkubwa zimezingatia kuajiri wanasheria wenye weledi wa hali ya juu. Hatua ya kuwachukua watu wenye sifa na uwezo mkubwa inaonyesha jinsi Mueller alivyochukua hatua makini katika uchunguzi huu, baada ya kukabidhiwa shughuli hii Mei 17, siku nane baada ya Rais Trump kumfukuza kazi Mkurugenzi wa FBI, James Comey.
Trump amesisitiza kuwa uchunguzi huo si sahihi na kusema ni hatua ya “kumtafuta mchawi,” na kutangaza kuwa “hakuna mtu ambaye amekuja na ushahidi” kuwa yeye au timu ya kampeni yake walihusika na vitendo vyovyote kinyume cha sheria, wakishirikiana na maofisa wa Russia.
Trump aliishambulia timu ya Mueller, akisema kuwa uchunguzi huu unaongozwa na baadhi ya watu ambao ni wabaya na wenye maslahi binafsi, akikusudia kwamba kuna taarifa baadhi ya watu walioajiriwa na Mueller wametoa michango siku za nyuma kwa wagombea wa chama cha Democratic wakati wa kampeni zao za kisiasa.