Kulwa Mzee , Dar es salaam
MAWAKILI 14 wa Serikali wakiingozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Clement Mashamba, wamewasilisha hoja nane za kupinga maombi ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, wakidai hayajakizi vigezo vitano kati ya sita vinavyotakiwa.
Wakili Mashamba alidai mbele ya Jaji Sirilius Matupa wa Mahakama Kuu kwamba, wamewasilisha pingamizi lenye sababu nane kupinga maombi yaliyowasilishwa na Lissu kupitia mawakili wake Peter Kibatala, John Mallya na Jeremiah Mtobesya.
Mashamba alidai katika sababu hizo nane, ndani yake kwa hoja nne ambazo kwa nyakati tofauti zitawasilishwa na mawakili na pale inapohitajika atasaidia.
Alizitaja hoja hizo nne kuwa wanahoji mamlaka ya mahakama kusikiliza maombi kama yalivyoletwa, pili kama mleta maombi ana uwezo wa kufanya hivyo, tatu kama maombi hayo yaliwasilishwa katika mahakama yenye mamlaka na nne kama nafuu zilizoombwa ni sahihi kutolewa na mahakama hiyo.
Akianza kuwasilisha hoja Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abubakar Mrisha alidai maombi yaliyowasilishwa mahakamani hayakidhi vigezo kwa sababu maombi au mashauri yanapofikishwa mahakamani lazima yawe yamezingatia vigezo sita.
“Kigezo cha kwanza kama maombi yaliletwa ndani ya miezi sita baada ya jambo husika kutolewa uamuzi, pili mwombaji awe anaelewa vizuri shauri, maamuzi yawepo kisheria, iwe hakuna namna nyingine ya kufanya kuhusu huo uamuzi, kama mahakama itasikiliza na kuona kuna haja ya kutoa uamuzi na sita maombi yanatakiwa yawe katika nia njema na wala si kwa kupotosha au kuwa na lengo la kujinufaisha binafsi.
“Mheshimiwa jaji katika maombi yaliyopo mahakamani ni kigezo kimoja walichotimiza nacho ni kuyawasilisha maombi ndani ya miezi sita, ukitazama vigezo vitano vimekosekana.
“Hakuna maamuzi yoyote yaliyoambatanishwa katika maombi ili mahakama iweze kuyapitia na kuyatolea uamuzi, maombi yoyote ni muhimu kisheria kuambatanisha maamuzi yanayomkumba.
“Katika kiapo cha Alute Mughwai alichoambatanisha ni nakala ya magazeti sio maamuzi na kwamba hakuna uamuzi wowote uliotolewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, alichofanya ni kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kwamba kuna kiti kiko wazi,”alidai na kuomba maombi yatupiliwe mbali kwa gharama.
Wakili wa Serikali Mkuu, Lucas Marunde alidai waleta maombi wanaomba mahakama imlazimishe Spika alete tamko lake la kumvua uUbunge Lissu mahakamani na wadai wapewe nakala.
“Mheshimiwa Jaji kwa mujibu wa Sheria ya uchaguzi namba 37 (3) sura ya 343 ya mwaka 2015 inasema Mbunge anapokuwa hayupo katika kiti chake kwa mikutano mitatu mfululizo ya Bunge bila kutoa taarifa, spika anafaMhamisha Mwemyekiti wa Tume ya uchaguzi kwamba kiti kiko wazi,” alidai .
Wakili Marunde alidai hakuna maamuzi yoyote kutoka kwa Spika hivyo wanaomba maombi yatupwe kwa gharama.
Hoja zingine ziliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, George Mundepo, ambaye anadai mleta maombi, Alute Mughwai hana sifa ya kufungua maombi hayo kwa niaba ya Lissu.
Anadai sheria inaruhusu madai kufunguliwa na muhusika au anayemwakilisha mwenye mamlaka kisheria lakini shauri lililopo limewasilishwa na Tundu Lissu kupitia mwakilishi wake Alute Simon Mughwai.
“Kanuni zinaeleza wakati wa kuomba ridhaa maombi yasainiwe na mwombaji au mwakilishi wake, maombi yaliyopo mahakamani yameambatabishwa na hati ya kumpa mamlaka kisheria kumwakilisha Lissu kwa sababu kashindwa kufanya hivyo mwenyewe.
“Julai 9 mwaka 2019 Lissu kasaini hati hiyo akiwa Ubelgiji ikionesha pia kiapo kimesainiwa na kupokelewa nchini humo, Wakili aliyeshuhudia Safolf Magay kasaini na kugonga muhuri kwa anuani ya Tanzania.
“Wakili hajaonesha kibali alichopewa kufanya kazi nchini humo, kwa hoja hizo kunafanya kiapo cha Alute kuwa si halali, maombi si halali kwani yaliambatana na kiapo batili hivyo yatupwe kwa gharama,”alidai.
Anadai Wakili Sadolf anafanya kazi nchini, haijawahi kuleta hati ya kiapo akionesha alikwenda Ubelgiji na wala haikuonesha kama wakili huyo alipata kibali kwa sheria ya Ubelgiji kufanya kazi nchini humo.
Kutoka na hoja hizo, aliomba mahakama iyatupe maombi kwani pamoja na mambo mengine aliyoyaleta, hana sifa ya kufanya hivyo.
Jaji Matupa jana alitakiwa kusikiliza maombi ya zuio la muda la kuapishwa kwa Mbunge Mteule, Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu na maombi ya kupinga kuvuliwa ubunge aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Tundu Lissu lakini haikuwezekana baada ya Jamhuri kuwasilisha pingamizi la awali.
Maombi ya kupinga kuvuliwa ubunge yalifunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa zamani wa Jimbo la Singida Mashariki, Lissu kupitia mawakili wake.
Amefungua shauri hilo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Wakili Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.
Maombi hayo dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiomba Kibali cha kufungua shauri la kupinga uamuzi huo.
Kwa mujibu wa maombi namba 18 la mwaka 2019, Lissu anaiomba mahakama hiyo, impe kibali cha kufungua kesi ili mahakama hiyo itoe amri ya kumtaka Spika Ndugai ampe (Lissu) taarifa yake ya kumvua ubunge.
Anaiomba mahakama hiyo itengue na kutupilia mbali uamuzi huo wa Spika Ndugai kumvua ubunge.
Mwombaji huyo anaomba mahakama itoe amri ya kusimamisha kuapishwa kwa Mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu wa Chama cha Mapinduzi.
Katika hati ya dharura Lissu anaiomba mahakama hiyo isikilize na kutoa uamuzi wa maombi yake haraka kwani vinginevyo, Mtaturu ambaye Julai 19 mwaka huu alitangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ataapishwa kushika wadhifa huo.
Hivyo anadai atakuwa ameathirika kwa kuwa atapoteza haki zake zote, kinga na maslahi yake yote yanayoambatana na wadhifa wake huo wa ubunge.
Uamuzi wa kumvua ubunge ulitangazwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, huku akitaja sababu mbili.
Spika Ndugai alizitaja sababu hizo kuwa ni kushindwa kuhudhuria vikao vvya bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na sababu ya pili ikiwa ni kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Hata hivyo Spika Ndugai alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni Katiba ya Nchi.