NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI wa Kampuni ya Ulinzi ya Advanced Limited, Juma Ntinginya (47) na wenzake wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kuwahifadhi raia wa Nepal.
Washtakiwa hao walipanda kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kisoka na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji, Patrick Ngayomela.
Ngayomela alidai washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja uendeshaji wa kampuni hiyo, Henry Mwakipunda (34) na dereva Hamza Sefu (30).
Akiwasomea mashtaka yao, Ngayomela alidai kuwa Agosti 29 mwaka huu, maeneo ya Kijitonyama, wilayani Kinondoni, kinyume na sheria, washtakiwa waliwahifadhi raia wa Nepal huku wakijua kufanya hivyo ni kosa.
Washtakiwa wote walikiri kutenda makosa hayo na kwamba waliwaingiza raia hao kwa nia ya kufanya kazi katika kampuni yao.
Inadaiwa viza walizokuwa nazo zilikuwa kwa ajili ya kutembea nchini na si kufanya kazi.
Hakimu Kisoka aliwahukumu washtakiwa kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh 100,000 kila mmoja. Wote walilipa faini na kuachiwa huru.
Wakati huo huo, mshtakiwa Halit Gurbuz (33) ambaye ni raia wa Uturuki, alipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru, kwa makosa mawili ya kuishi nchini na kufanya kazi bila kibali.
Ngayomela akimsomea mashtaka, alidai Agosti 30 mwaka huu maeneo ya Mikocheni, mshtakiwa akiwa raia wa Uturuki, alikutwa akiishi nchini bila kibali.
Katika shtaka la pili, anadaiwa huku akijua hana kibali cha kuishi nchini, alikuwa anafanya kazi Kampuni ya Techno Plus bila kibali cha kumruhusu kufanya hivyo.
Mshtakiwa alikiri kosa na Hakimu Mchauru aliahirisha kesi hiyo hadi leo kwa ajili ya kumsomea hukumu. Hata hivyo, mshtakiwa alikwenda mahabusu Keko.