Mavuno ya aibu ya Rais wa Sierra Leone, Valentine Strasser

0
1250
Valentine Strasser alipoingia madarakani mwaka 1992 akiwa na miaka 25

JOSEPH HIZZA NA MTANDAO

ANAVAA nguo chakavu, ambazo watoto mitaani wanaziita matambara, hunywa pombe za kienyeji kama vile ulanzi au nyingine za bei nafuu, hamiliki gari wala nyumba yoyote.

Aidha anaishi katika banda la uani la nyumba ya mama yake na anahofiwa kupoteza uwezo wake kiakili.

Huyu ni Valentine Strasser, Mkuu wa Nchi ya Sierra Leone kati ya mwaka 1992 na 1996.

Akiwa ametopea katika ulevi na kuonekana kama mzee, Strasser ,ambaye sasa ana miaka 51 hujipatia pensheni ya Sh 100,000 kwa mwezi tu.

Iwapo u mgeni wa siasa za Afrika Magharibi katika mapema miaka ya 90 kuelekea katikati ya miaka hiyo 90, kuna uwezekano hukuwa ukifahamu hili

Katika kipindi hicho, Magharibi mwa Afrika kulikuwa na mlolongo wa tawala za kidikteta, kiimla na kijeshi kuanzia Ibrahim Babaginda wa Nigeria, J.J Rawlings wa Ghana, Sani Abacha (Nigeria), Charles Taylor (Liberia), Yahya Jammeh (Gambia) na wengineo.

Akiwa anaonekana katika orodha ya wakati huo ya mabwana vita, majenerali na majenerali waliogeuka watawala wa kiraia ni Valentine Strasser, ambaye anashikilia rekodi ya kuwa mtawala mdogo kabisa wa kijeshi barani Afrika.

Strasser aliingia madarakani Aprili 29, 1992 akiwa na umri wa miaka 25.

Pamoja na maofisa wengine sita kivita waliongoza harakati zilizoin’goa Serikali ya Sierra Leone iliyoongozwa na Rais Joseph Saidu Momoh.

Ili kuweka sawa kumbukumbu sawa, Yakubu Gowon wa Nigeria aliingia madarakani akiwa na umri wa miaka 32, J.J Rawlings akiwa na miaka 31 bila kumsahau Yahya Jammeh aliyeingia madarakani akiwa na miaka 29.

Kama ilivyo kila aina nyingine ya Mapinduzi barani Afrika, utawala mpya wa kijeshi Sierra Leone ulikaribishwa kwa mikono miwili na wengi walijitokeza mitaani kuwashangilia askari waliojaa ujana wakisherehekea.

Chini ya uongozi wa Saidu Momoh, uchumi wa Sierra Leone uliporomoka vibaya. Ilikuwa nadra kwa gesi na maji kwa ajili ya raia kupatikana na watumishi wa umma walikaa miezi mingi bila mishahara.

Kapteni Strasser aliwaongoza wenzake kuvamia Ikulu, ambako walimkuta Rais Momoh amejificha katika chumba cha maongezi ndani ya kabati lililopo humo, ambapo wakamlazimisha kukimbia, akatorokea Conkry nchini Guinea.

Ilikuwaje lakini? Kijana Strasser mwenye ndoto nyingi, alikuwa amepewa jukumu la kusimamia Wilaya ya Mashariki ya Kailahun kushughulika na uasi na machafuko yaliyoongozwa na koplo wa zamani wa jeshi aliyekuwa akipambana na Serikali ya Momoh.

Baada ya vita kupamba moto katika mstari wa mbele, Strasser na wenzake wakaishiwa vifaa kama buti na vingine muhimu kijeshi.

Juhudi zao za kuitaka Serikali ya Sierra Leone iwapatie vifaa vingine waendelee na mapambano ziligonga mwamba, bila kusahau kuwa askari walikuwa na miezi kadhaa bila mishahara.

Aprili 29, 1992, Strasser aliongoza timu ya askari vijana kuandamana wakiwa katika magwada yao ya kijeshi kutoka Kailahun kwenda Ikulu kupinga hali zao hizo.

Ripoti zinasema kuonekana kwa askari katika mji mkuu wa Freetown kuliwashtua wengi na kumlazimisha Rais Momoh kukimbia nchi

Hilo likatengeneza ombwe la uongozi na Strasser na watu wake vijana na kama yeye maarufu kama wavulana wakachukua fursa hiyo kutwaa madaraka na kuunda Chama cha National Provisional Ruling (NPRC).

NPRC ikamfanya Strasser kuwa Kiongozi wa chama na nchi ikiwa ni siku tatu tangu atimize miaka 25.

Miezi ya awali ya utawala huo wa kijeshi ilikuwa mizuri. Uchumi ulionekana ukiibuka kwa matumaini na nyuso za watu zilitawaliwa na furaha zikimhesabu Strasser kama mwokovu.

Strasser na genge lake pia walipanga kukabidhi madaraka kwa serikali ya kuchaguliwa kidemokrasia.

Vijana wengi walifurahia kuingia kwa Strasser madarakani wakiamini amekuja kupigania masuala yao.

Hata hivyo ujana wa Strasser, kwa mujibu wa ripoti ukawa kaburi lake.

Mara baada ya kuingia madarakani badala ya kusaka maridhiano aliendesha vita dhidi ya kiongozi wa waasi Foday Sankoh, jambo alilolifanya kuwa moja ya vipaumbele vyake vikuu. Hata hivyo, hakufanikiwa.

Matumaini, matarajio na ari, ambayo wavulana hao waliileta ilikuwa na upande wa pili wa shilingi usiofurahisha.

Serikali ilionesha wingi wa hamasa za ujana katika matukio ya umma ikitema cheche zenye matamko na mihemko mikali isiyo na sababu.

Strasser kuchaguliwa na vijana wenzake kuiongoza Sierra Leone, si kuwa alikuwa smati au muimla bali kwa sababu alikuwa mmoja wa watu wachache mno, ambao walibahatisha kwenda shule ya sekondari na ambaye anaweza kuzungumza Kiingereza.

Bahati mbaya, mfumo wa elimu nchini Sierra Leone ulikuwa mbaya sana, kiasi kwamba Kiingereza cha kuzungumza cha Strasser kilikuwa dhaifu.

Kwa sababu ya kukosa kwa elimu tosha kwa Valentine Strasser, alikuwa mwenye aibu kwenye mikutano ya kimataifa.

Aliwahi vunja mkutano na Malkia Elizabeth II kwa kile kilichoripotiwa kuwa wingi wa haya.

Pia Valentine Strasser na kundi lake lote walitenda mambo kama watoto waharibifu.

Waliendesha magari ya bei mbaya na kuyaringisha kwa kasi mitaani, waliuza almasi ng’ambo na kuishi staili ghali za misha, vitendo vile vile walivyokuwa wakivilaani dhidi ya utawala walioupindua.

Miezi minane baada ya Mapinduzi, fungate liliisha nchini humo, kati ya mwezi wa Desemba, utawala wa kijeshi ukanyonga wanaume 29 waliotuhumiwa kula njama za kuupindua utawala huo bila usikilizaji wowote wa kesi dhidi yao.

Maisha yakabadilika kwakuwa tu ashakuwa mkuu wa nchi, kwa hiyo hakutaka kuishi kwenye nyoyo za wananchi wake Sierra Leone,

Hakukumbuka tena kulipa malimbikizo ya mishahara ya wanajeshi na watumishi wengine wa umma, alifuja almasi ya Sierra Leone na rasilimali zingine na kusababisha kuchukiwa na wananchi, wanajeshi wenzake na chama chake tawala ndani ya muda mfupi.

Naam, Sierra Leone ikaangukia tena katika nyakati za giza huku uchumi ukielekea kudidimia tena, ‘Wavulana hao walituhumiwa sana kwa rushwa na ubadhirifu.

Licha ya kuwa mwingi wa haya, Rais Strasser alikuwa mwenye mwembwe na vituko vingi, kupenda sifa na kusifiwa.

Katika moja ya mikutano ya kimataifa, hasa ule wa mwaka 1993 wa wakuu wa Mataifa ya Jumuiya ya Madola, uliofanyika Limassol nchini Cyprus, alitinga kwa mbwembwe akiwa amevaa suruali ya jinsi na fulana yenye maandishi Sunny Days in Cyprus’

Alikuwa mtu wa starehe sana, mbabe, mwingi wa vurugu na mpenda wanawake na kwa kipindi cha utawala wake wengi wa waliouawa si tu wapinzani wake bali pia watu wasio na hatia.

Kama walivyo madikteta wengi, mtawala huyu dogo alikuwa mwingi wa vituko.

kwa vile jina lake ni Valentine, basi Sikukuu ya Wapendanao yaani Valentine Dy, ambayo dunia yote huadhimisha kila ifikapo Februari 14, akaifanya kuwa miongoni mwa Sikukuu za Kitaifa yenye mapumziko huku sherehe kubwa ikiandaliwa ikulu ya nchi hiyo na bata zikitafunwa kwa sana.

Katika harakati za kuituliza jumuiya ya kimataifa, utawala huo wa kijunta ukapanga kuendesha chaguzi mwaka 1996.

Kama ilivyokuwa kwa J.J Rawlings na Sani Abacha, Strasser akajitangazia kugombea urais, kitu kilichowakasirisha watu wengi.

Wakati taifa likienda mrama zaidi, Valentine Strasser akazidi kuchukiwa na waliomzunguka wakaendesha mapinduzi bila kumwaga damu yaliyoongozwa na naibu wake mwenye umri wa miaka 32, Maada Bio Januari 16, 1996.

Strasser hakuuawa bali alikimbilia Guinea. Kiongozi huyo kijana na wenzake ambao walifurushwa kutoka madarakani walishiriki katika makubaliano na Umoja wa Mataifa (UN), yaliyowaruhusu kusomea England.

Akasomea Chuo Kikuu cha Warwick huko Coventry, ambako alijinasibu kutaka kuwa wakili na kuja kuwatetea Waafrika alioshindwa kuwatetea akiwa madarakani.

Hata hivyo, hakuweza kukamilisha masomo kutokana na sababu ambazo bado hazijathibitishwa.

Kuna madai kuwa UN iliacha kumsomesha baada ya mwaka mmoja kufuatia maandamano ya kupinga dikteta huyo wa kijeshi na mkiukaji wa haki za binadamu kusoma humo England.

Hata hivyo, msemaji wa chuo hicho wakati huo, Peter Dunn, alisema Strasser alitumia miezi 18 kusoma, kabla ya kukiandikia chuo kuwa ameishiwa fedha na hivyo anaacha shule. Akahamia London, ambako alifanya kazi kama DJ wa kilabu moja ya usiku.

Lakini akiwa hana pesa kama za kutumbua sana kama zile alizopata akiwa mkuu wa nchi, Strasser akajitosa katika pombe katika harakati za kutuliza mawazo yaliyomzonga kutokana na mwisho wake huo mbaya.

Baada ya maisha ya England kumshinda akiwa amefilisika, mwaka 2000, aliondoka England kwenda Gambia lakini maisha yake pale yalikabiliwa na matatizo.

Alishambuliwa na ndugu na jamaa za mmoja wa watu waliouawa ufukweni na utawala wake mwaka 1992.

Serikali ya Gambia pia ikamtuhumu kula njama za kuipindua na hivyo ikamfukuza. Safari hii, Uingereza haikumchukua, hakuwa na mahali pengine pa kwenda zaidi ya nyumbani, Sierra Leone.

Tofauti na wakuu wengine wa nchi, hakufanyiwa mapokezi ya kifahari hekaluni, pensheni nono wala walinzi.

Alikuta nyumba aliyoijenga ikiwa imeteketezwa moto na askari mwaka 1999 na kulazimika kuhamia katika banda la uani la mama yake

Kazi ya kwanza, ambayo Strasser aliifanya ni kuanzisha chuo kidogo cha kufundisha kompyuta na teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).

Hata hivyo, hapo nako laana ya dhambi ya kuwanyanyasa raia wakati akiwa rais ikazidi kumwandama na hatimaye maisha ya kuendesha chuo chake yakamshinda baada ya kila kitu kwenda kombo.

Hadi sasa anaishi katika nyumba ya zamani ya mama yake huko Grafton, Sierra Leone. Maisha yake ni ya upweke bila marafiki, akizomewa na wavulana mitaani, ambao si tu humwita kila aina ya majina kuanzia omba omba, chapombe hadi mvaa matambara.

Kuonesha kiasi gani maisha yamemvuruga, amekuwa akiishi kwa kuomba omba mitaani bila kujali kama aliwahi kuwa rais wa taifa tajiri kwa rasilimli kama Sierra Leone.

Licha ya miito na maombi mbalimbali ndani na nje ya Sierra Leone Serikali imesisitiza Strasser hastahili mafao au stahili yoyote kama mkuu wa nchi wa zamani mbali ya kile jeshi alilolitumikia inachomlipa kila mwezi (Tsh 100,000) kwa sababu aliingia madarakani kwa nguvu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here