28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mavunde azindua timu ya kuandaa andiko la VISION 2030

*Prof. AbdulKarim Mruma kuongoza timu

*Wapewa Hadidu za Rejea 14 muhimu kujenga uchumi wa nchi kupitia madini

*Tanzania kufanya Utafiti wa eneo la asilimia 50 nchi nzima kufikia 2030

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amezindua Timu itakayoandaa Andiko la maudhui ya Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri katika hafla iliyofanyika Juni 12, 2024 jijini Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mavunde amesema kuandaliwa kwa andiko hilo ni matokeo ya maelekezo aliyoyatoa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt Samia Suluhu ya kufanyika kwa utafiti wa kina ili kuboresha eneo hilo na hatimaye kuwawezesha watanzania wasichimbe kwa kubahatisha.

Waziri Mavunde ameongeza kwamba, mpaka sasa utafiti wa kina kwa nchi nzima umefanyika kwa asilimia 16 ambapo mpango uliopo kupitia Vision 2030 ni kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

“Tanzania imejaliwa kuwa na madini mbalimbali lakini bado hatuna uwezo mkubwa wa kubaini kiwango cha madini hayo. Kupitia vision 2030 tutabaini yote hayo,’’ amesema Waziri Mavunde.

Akizungumzia kuhusu sekta zitakazo nufaika na utekelezaji wa Vision 2030, amezitaja kuwa ni pamoja na sekta ya Kilimo, Afya, Maji na Viwanda na kuongeza kwamba lengo ni kuhakikisha Sekta ya madini inajifunganisha na sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo kuziwezesha kukua.

“Hekta milioni 3.6 zimeathirika na tindikali kufanya shughuli za kilimo kuwa ngumu, tukifanya utafiti wa kina utasaidia eneo kubwa la nchi yetu. Tunaona sekta ya madini ina mchango mkubwa wa kuendeleza sekta nyingine,” amesisitiza Waziri Mavunde.

Pia, Waziri Mavunde ametaja baadhi ya manufaa yaliyotokana na matokeo ya utafiti wa kina uliofanywa kwa asilimia 16 nchi nzima na kubainisha kuwa ni pamoja na kuiwezesha Sekta ya Madini kuongoza kwa kuchangia fedha za kigeni kutokana na mauzo ya bidhaa za madini nje ya nchi ambapo mchango wake umefikia asilimia 56, kuongezeka kwa mapato ya ndani yanayotokana na sekta ya kufikia asilimia 15.

Katika hatua nyingine, Waziri Madini ameikabidhi Kamati hiyo inayoongozwa na Prof. AbdulKarim Mruma hadidu 14 za rejea zitakazowezesha kuandaliwa kwa andiko hilo na kuitaka kuhakikisha andiko hilo linawezesha utekelezaji wa vision 2030 kutoka na matokeo makubwa nane ikiwemo kusaidia kuongeza mchango wa Sekta ya madini kwenye pato la taifa, kuwezesha upatikanaji wa fedha za kigeni, kuwezesha maendeleo ya viwanda na sekta nyingine na kuwezesha ushiriki wa watanzania katika sekta ya madini.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameipongeza Wizara ya Madini kwa kufanya utafiti wa awali Mkoani Dodoma ulionesha uwepo wa aina mbalimbali za madini na kuiomba Wizara kuendelea na utafiti wa kina ili kujua kiasi cha mashapo yaliyopo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini, Dk. Mathayo David Mathayo, amesema kuwa Vision 2030 itaongeza wigo mpana kwa watanzania kushiriki katika mnyororo unaounganisha sekta nzima ya madini pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya wizara likiwemo Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa, ameipongeza Wizara ya Madini kuja na Vision 2030 akisisitiza kuwa umefika muda wananchi kunufaika na rasilimali madini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna wa Madini Dk. AbdulRahman Mwanga kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Madini, amesema kuwa wizara ipo tayari kusimamia maono Vision 2030 ambayo yataleta mabadiliko makubwa ya kisekta kwa miaka sita ijayo kupitia hadidu za rejea kama zilivyoainishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles