MAVUNDE AWATAKA VIJANA  KUBADILI MTAZAMO WA AJIRA

0
481

Na JUDITH NYANGE 



NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira,  Antony Mavunde, amewataka vijana kutobagua kazi kwa kudhani  ajira ni zile za serikalini au sekta binafsi.
Aliwaasa kuanza kubadili mtazamo wao katika suala hilo  waweze kujiajiri.


Alikuwa akizungumza juzi wakati wa uzinduzi wa mpango wa mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi na kuwajengea uwezo vijana   waweze kujiajiri, yaliyofanyika katika   Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Tawi la Mwanza.


 Mavunde alisema watanzania wengi wamekariri ajira ni zile za ofisini tu na kusahau tafsiri ya ajira kwa mujibu wa sera ya ajira ni shughuli yoyote inayompatia mtu kipato.


Alisema mpango huo umelenga kuwafikia vijana zaidi ya milioni nne nchini katika kuwajengea uwezo ambao utawasaidia kujiajiri .
Vilevile wataweza  kuajiriwa kwenye viwanda mbalimbali nchini kwa kutumia bidhaa zitokanazo na mazao ya mifugo kwa ajili ya uzalishaji viatu na bidhaa nyingine za ngozi nchini.


“Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012,   zaidi ya watu milioni 23 ni vijana kuanzia umri wa miaka 18 hadi 35 ambao wana nguvu za kufanya kazi ingawa changamoto iliyopo wengi wao hawana ajira rasmi, jambo ambalo mpango huo utasaidia kukuza ajira,” alisema Mavunde.


Alisema mafunzo hayo pia yamelenga kubadilisha mtazamo wa vijana kuhusu suala la ajira ikizingatiwa  ajira haijawahi kutosheleza mahitaji popote duniani.


“Idadi ya watu wanaotafuta kazi kila mwaka ni 850,000 mpaka milioni moja, ajira zinazotengenezwa kwa mwaka ni 150,000 mpaka 200,000.


“Unakuta mtu ana kibanda cha matunda kinachompatia kipato cha Sh 10,000  kila siku lakini anasema yupo tu amejishikiza hana ajira,” alisema Mavunde.


Alisema ni vema vijana wakaitumia fursa hiyo kwenda kubadilisha maisha yao na kutambua taifa linawategemea katika kujenga uchumi wa nchi.


  Mkurugenzi Mkuu Chuo cha DIT Tawi la Mwanza, Dk. Albert Mmari, alisema chuo hicho kimeanza kutoa mafunzo kwa vitendo kwa njia ya intaneti.


Alisema lengo ni kuwasaidia vijana wasiokuwa na muda wa kuhudhuria darasani kupata elimu ya utengenezaji na uchakataji wa bidhaa hizo.


Akizungumza kwa niaba ya wanavyuo wenzake, mmoja wa wanafunzi   chuoni hapo, Easter Ndyanabo, aliiomba serikali kuangalia namna ya kukabiliana na changamoto ya masoko.


Pia aliiomba serikali kuangalia namna ya kuwaajiri kwenye taasisi   waweze kujipatia tenda za kupeleka bidhaa zao kama njia za kujipatia kipato.


Uzinduzi wa mafunzo hayo ulihusisha vijana kutoka Mikoa ya Shinyanga, Mara, Geita, Bukoba na Simiyu.
Umelenga kumaliza tatizo la utegemezi wa kuajiriwa kwenye taasisi au kampuni na zaidi ya vijana 1, 000 kutoka mikoa zaidi ya 10 nchini wanatarajiwa kupatiwa mafunzo ya ufundi wa kisasa wa kutengeneza viatu kwa njia za kisasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here