30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mavunde atembelea mradi wa uchimbaji visima Nzuguni

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

NAIBU Waziri wa Kilimo na Mbunge Dodoma wa Mjini, Anthony Mavunde, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa kuweza kushirikiana na wananchi katika kutatua kero ya maji licha ya changamoto zote zilizopo.

Ameyasema hayo leo Oktoba 11, 2022 wakati wa ziara yake katika eneo la Nzuguni ambapo visima vitano vimechimbwa katika eneo hilo.

“Ninampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutatua changamoto ya upungufu wa maji katika jiji la Dodoma, tunamshukuru Rais kwa mipango ya muda mrefu ya kati na mipango ya muda mfupi ya kutatua changamoto hii,” amesema Mavunde.

Amesema yeye kama Mbunge ataendelea kuishauri serikali namna nzuri ya kupata maji kabla ya utekelezaji wa miradi mikubwa kuanza na kuweka fedha katika uchimbaji wa visima virefu pembezoni ili tuweze kupata maji ya uhakika.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa majisafi Nzuguni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph alisema zaidi ya wakazi 37,000 waishio katika ukanda wa Nzuguni jijini Dodoma wanatarajia kunufaika na mradi wa maji baada ya kubainika uwepo wa bonde lenye maji mengi katika eneo la hilo.

“Maeneo ambayo utafiti na uchimbaji visima unaendelea yanamilikiwa na wananchi na mara baada ya kukamilika kazi hizo zoezi la uthamini litafanyika kwa ajili ya kulipa fidia ili kuyatwaa kwa matumizi ya mamlaka,” amesema.

Alibainisha kuwa mradi huo utaongeza uzalishaji wa majisafi kutoka wastani wa lita milioni 67.8 hadi lita milioni 75.5 kwa siku sawa na ongezeko la asilimia 11.4 ya uzalishaji wa sasa.

Aidha, utaondoa mgao wa maji maeneo ya Nzuguni, Ilazo na Kisasa na utawezesha maji yanayohudumia ukanda huo kupelekwa maeneo mengine ya Jiji.

“Ongezeko hili litaongeza asilimia 11.7 ya mahitaji ya sasa ya jiji lote la Dodoma ambayo ni lita milioni 133.8 kwa siku,”alisema.

“DUWASA tunaishukuru Wizara ya Maji kwa kuwa tayari kutenga fedha za kutekeleza mradi huu kwa haraka na kupunguza adha ya maji katika maeneo husika, kipindi miradi mikubwa ya Farkwa na Mtera ikiendelea kutekelezwa,”alieleza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Jabir Shekimweri aliipongeza DUWASA kwa hatua hiyo huku akiishauri kuendelea na kasi ili kupata maji maeneo mengine.

Aidha, alishauri wananchi wanaopisha miradi hiyo kulipwa fedha zao mapema ili eneo libaki kuwa chanzo cha maji na wanaojenga wajulishwe kuhusu kuzingatia suala la upandaji miti ili kutunza mazingira.

Pia, aliishauri DUWASA kuzingatia afya ya walaji kwa kuhakikisha mkondo wa maji hauingiliani na mfumo wa majitaka.

Diwani wa Kata ya Nzuguni Aloyce Luhega alishauri mamlaka hiyo kuangalia uwezekano wa kupeleka maji katika eneo la Mahomanyika ambalo lipo kwenye kata hiyo lenye changamoto kubwa ya maji.

DUWASA kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Maji wamechimba visima vitano katika eneo la Nzuguni kupitia mradi huo utakaogharimu zaidi ya Sh bilioni 4.8 maji yatafikishwa kwa wakazi wa Nzuguni, Ilazo, Swaswa na Kisasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles