|Mwandishi Wetu, Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amewataka wananchi katika jimbo lake kushirikiana na serikali na viongozi wao katika kujiletea maendeleo.
Aidha, ametoa wito kwa jamii kujitoa kwa dhati kuchangia maendeleo kama wanavyofanya kwenye shughuli mbalimbali za kijamii hasa katika sherehe mbalimbali zikiwamo harusi.
Mavunde ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akiongoza wananchi wa Kata ya Kikuyu Kusini katika ujenzi wa vyumba vya madarasa vya shule hiyo.
Katika shughuli hiyo, Mavunde amechangia matofali 1,000 na mifuko ya saruji 130, kompyuta moja, jezi, mipira na kuweka magoli ya chuma katika uwanja wa michezo uliopo katika Shule ya Msingi Kikuyu B.
Mbunge wa Jimbo la Bahi, Omary Badwel amewapongeza wananchi wa Kata ya Kikuyu Kusini kwa muitikio wao mkubwa kwenye shughuli za maendeleo na kuahidi kushirikia na Mavunde kutatua changamoto za shule hiyo kwa kuchangia mifuko 20 ya saruji iliyopo eneo ambalo na yeye ni mkazi wake na watoto wake pia wanasoma katika shule husika.