25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Mavugo unajua mashabiki wanataka nini?

laudit-mavugoNA BADI MCHOMOLO

KATIKA usajili ambao Simba waliamini kuwa wamefanikiwa mwaka huu ni kumsajili nyota kutoka nchini Burundi, Laudit Mavugo.

Mchezaji huyo alihusishwa na klabu hiyo yenye makao yake makuu Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo, jijini Dar es Salaam tangu misimu miwili iliyopita, lakini ilikuwa ngumu kumnasa.

Lakini msimu huu wamefanikiwa kumpata mchezaji huyo na waliamini kuwa anaweza kuwa msaada mkubwa katika michezo ya Ligi Kuu.

Ni wazi kwamba, uwezo wa Mavugo ulikuwa katika misimu hiyo miwili iliyopita ambapo alikuwa anasakwa na klabu hiyo ya Simba, lakini baada ya hapo uwezo wake umepungua, tofauti na kipindi hicho.

Tayari mashabiki wa Simba wameanza kumchoka, lakini si kosa lake, ni kosa la Kamati ya Usajili ambayo iliamini kuwa bado ana kiwango kile cha misimu miwili iliyopita.

Yeye hajafanya kosa kusaini mkataba na Simba kwa kuwa sehemu ya maisha yake ni kucheza soka. Kikubwa ambacho kinamsumbua Mavugo ni kushindwa kupachika mabao kama mchezaji namba tisa.

Siyo kama hajafunga bao, lakini mabao aliyoyafunga ni machache, hayana uwiano na michezo aliyocheza, lakini kwa upande wangu ninaamini bado ana nafasi ya kuweza kurudisha imani kwa mashabiki wake.

Kutokana na kusikiliza kelele za mashabiki ambao wameanza kumzomea mchezaji huyo, inamfanya awe na tamaa ya kutaka kufunga bao kila apatapo nafasi ya kulishambulia lango ya wapinzani wake.

Hili ni tatizo kwake, kikubwa ambacho anatakiwa kukifanya ni kutulia kabisa na kupunguza papara za kutaka kufunga, ila anaweza kurudisha imani kwa mashabiki hata kama ataweza kutoa pasi za mwisho na kutengeneza nafasi nyingi.

Nguvu alizonazo mchezaji huyo zinaweza kubadilisha matokeo muda wowote, kwa kuwa anaweza kupambana na mabeki, lakini kinachomsumbua ni kwamba anataka kufunga yeye kila anapopata nafasi, huku akiwa na lengo la kutaka kuwatuliza.

Tatizo hilo si kwake tu, linawakuta wachezaji wengi ambao wanasajiliwa kwa mbwembwe na gharama kubwa na wanashindwa kufanya kile ambacho mashabiki wanakusudia kukiona kwa wakati huo.

Obrey Chirwa, mshambuliaji wa Yanga SC, naye alikuwa na janga kama hilo la kuzomewa na mashabiki wake kutokana na kushindwa kupata mabao haraka, lakini kwa sasa ameanza kuwatuliza mashabiki kwa kuwa ameanza kufunga.

Imani ya mashabiki kwa mchezaji huyo imetulia, lakini kwa baadhi ya mashabiki wa Simba bado hawana imani na Mavugo wao.

Anaweza kubadilika kwa kuwa tayari amewasoma mashabiki wa klabu hiyo nini wanataka, na ni wakati sahihi wa kufanya hivyo bila ya kufikiria wachezaji wenzake wanafanya nini kama vile Shiza Kichuya na Ibrahimu Ajib ambao wanafunga mabao mengi kama wao wanacheza namba tisa.

Nimeona mashabiki wakimzomea mchezaji huyo, hasa pale anapopata mpira na kufikiria juu ya kuupiga bila ya kuangalia mchezaji gani wa timu yake ambaye ana nafasi ya kufunga bao, lakini yeye anafanya maamuzi ya kutaka kufunga ili aweze kuwafurahisha mashabiki.

Mavugo muda ndio huu kaka wa kuwapa mashabiki kile ambacho wanakitaka, kama unashindwa kufunga kutokana na mabeki kukukamia, basi tengeneza nafasi nyingi kwa Kichuya, Ajib na wengine ambao unacheza nao ili waweze kufunga wao, lakini sifa itakuwa yenu wote, wewe uliyetoa pasi na yule aliyefunga.

Kwa kufanya hivyo, ninaamini ugomvi na mashabiki wako utakufa na baadaye unaanza kufunga wewe sasa, mashabiki hatuchelewi kusahau, fanya hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,695FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles