Na WINFRIDA NGONYANI-DAR ES SALAAM
HATIMAYE uongozi wa Simba umeingia mkataba wa miaka miawili na mshambuliaji Laudit Mavugo kwa ajili ya kuichezea timu hiyo katika msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mavugo amewasili nchini juzi akitokea Burundi tayari kukipiga katika timu hiyo, ambayo ilikuwa ikihaha kumnasa mshambuliaji huyo kutoka klabu ya Vital’O ya nchini humo.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele, alisema mazungumzo na Mavugo yamekamilika na kwamba ataungana na wenzake kambini mkoani Morogoro.
“Tumeingia naye mkataba wa miaka miwili tukiwa na imani kubwa kuwa ataleta mapinduzi makubwa, kwa ujumla ujio wake umetufurahisha na hakika kiu yetu ya kutaka kuwa naye imekatwa,” alisema.
Mavugo anakuja nchini baada ya mpango wake wa kujiunga na klabu ya Tours ya Ligi Daraja la Pili, Ufaransa, maarufu kama Ligue 2 kugonga mwamba, ambapo sasa atakitumikia kikosi cha Simba kuanzia msimu ujao.