27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAVAZI YA MAKAMU WA RAIS YAMVUTIA ASKOFU

Na EDITHA KARLO-KIGOMA


ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Free Pentecost Tanzania (FPCT), Ezra Mtamya, amewataka wanawake wa kikristo nchini kuvaa mavazi ya heshima kama ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Amesema kiongozi huyo ni kivutio kwa watu wengi kutokana na mwonekano na mavazi  yake yenye heshima mbel ya jamii.

Hayo aliyasema jana mjini Kigoma kwenye Ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Mkuu Msaidizi na maaskofu wengine wanne wa kanisa hilo lilipo Mwanga, ambapo Askofu Mtamya alisema wanawake wanatakiwa kuvaa mavazi yanayositiri miili yao kwasababu kwa kufanya hivyo, wataendelea kuwa warembo na watapendeza zaidi badala ya kuvaa mavazi ya ovyo.

Alisema mavazi ya makamu huyo wa Rais yanampendeza na kuwa kivutio popote alipo. “Ninyi muigeni yeye kwa kuvaa hivyo,” alisema.

Askofu Mtamya alipongeza uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi zake za kuijenga Tanzania yenye maendeleo.

Alisema kama kanisa wamekuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya jamii na utunzaji wa mazingira ambapo wameiomba Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuwapa wataalamu wa mazingira pamoja na ufugaji nyuki.

Alisema kanisa linatoa pongezi kwa kazi nzuri inayofanywa na serekali ya awamu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaletea wananchi maendeleo,vita dhidi ya rushwa,ufisadi,kuzuia wizi wa rasilimali za Taifa hasa madini na wanyama pori.

Licha ya hali hiyo askofu huyo aliipongeza pia serikali kwa uamuzi wake wa kuimarisha Kampuni ya Ndege ya Tanzania(ATCL), kwa kununua ndege mpya na za kisasa.

Kutokana na hali hiyo alisema hivi sasa Tanzania inaonekana katika anga za kimataifa na kuvutia wawekezaji wengi kuja kuwekeza nchini.

“Kama kanisa tutaendelea kuwahimiza waumini wetu kufanya kazi kwa bidii na uadilifu na kuzingatia miongozo yote ya serekali kuhusu sera za kiuchumi na kwasasa tunaunga mkono sera ya kujenga uchumi wa viwanda,” alisema.

Kwa upande wake Makamu Rais Samia Suluhu Hassan, alisema serikali inatambua mchango wa madhehebu ya dini katika kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

“Serikali imeweka mazingira rafiki kwa madhehebu ya dini nchini kuweza kutoa huduma za kijamii hususan elimu na afya,” alisema Samia.

Pamoja na hali hiyo amesisitiza umuhimu wa kanisa kujiepusha na migogoro ya kiutawala ndani ya kanisa na pia liepuke kuchanganya dini na siasa.

“Kazi kubwa ya kanisa iwe kuhubiri amani kwa waumini wake na wananchi kwa jumla” alisema Makamu wa Rais huku akinukuu neno la Mungu katika Waebrania 12:14, ambalo linasema. “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote” alisema.

Alisema pia serikali inalitegemea kanisa ni katika kujenga maadaili mema ya jamii.

Kutokana na hali hiyo Makamu wa Rais alilitaka kanisa kusaidiana na serikali katika kupiga vita tamaduni mbaya za nje ili kujenga Taifa lenye maadili ya kitanzania kwa kupiga vita rushwa na ufisadi ambavyo ni adui wa maendeleo ya nchi.

Maaskofu waliosimikwa jana ni Askofu Mkuu Msaidizi Bwami Mathias, Askofu Shemu Mwenda (Jimbo la Kati), Askofu Simon Bikatago wa Jimbo la Magharibi, Askofu Jackson Maneno wa Jimbo la Tanganyika na Askofu Eliasaph Mathayo wa Jimbo la Mashariki.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga, aliwataka wanaume kujitokeza kwa wingi kupima afya zao kwa hiyari ili kujua kama wana maambukizi ya VVU ili waweze kuanza dawa mapema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles