JOHANES RESPICHIUS Na MARGRETH MWANGABAKU (TUDARCo)
DAR ES SALAAM
MAUZO ya hisa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) yameshuka kutoka Sh bilioni 12.5 hadi Sh bilioni 4, ikichangiwa na kupungua kwa hisa zilizouzwa na kununuliwa kutoka milioni 46 hadi laki 6.
Akizungumza na waandishi wa habari,, alisema kushuka huko kulisababishwa na baadhi ya wawekezaji kuamua kuwekeza kwenye hati fungani ambazo mauzo yake yalipanda kutoka Sh bilioni 1.4 hadi bilioni 8.18.
“Mauzo haya yametokana na kuuzwa kwa hati fungani 10 za Serikali na za kampuni binafsi zenye thamani ya Sh bilioni 9.4 kwa jumla ya gharama ya Sh bilioni 8.18.
“Kampuni zilizoongoza katika mauzo ya hisa ni TBL kwa asilimia 94.77 ikifuatiwa na TCC asilimia 2.89 na Benki ya CRDB asilimia 1.53,” alisema Mary.
Alisema kuwa ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa sokoni ulipanda kwa Sh bilioni 300 kutoka Sh trilioni 17.9 hadi trilioni 18.3, kutokana na kupanda kwa bei za hisa za NMG asilimia 11.86, EABL asilimia 2.51, KCB asilimia 2.35 na ACA asilimia 2.16.
Aidha Mary alisema ukubwa wa mtaji wa kampuni za ndani uliongezeka kwa Sh milioni 480 kutoka Sh trilioni 7.7 hadi trilioni 7.71 baada ya kupanda kwa bei ya hisa za DSE kwa asilimia 1.69 kutoka Sh 1,180 hadi 1,200.
Kwa upande wa viashiria, alisema kiashiria cha kampuni zilizopo sokoni kilipungua kwa pointi 35 kutoka 2,066.3 hadi 2,101.51 ikichangiwa na kushuka kwa bei za hisa za kampuni mbalimbali.
Alisema kiashiria cha kampuni za ndani, yaani TSI kilibaki kwenye wastani wa pointi 3,670, pia sekta ya viwanda iliendelea kuwa kwenye wastani wa pointi 4793.
Mary alisema huduma za kibenki na kifedha ilipanda kwa pointi 0.61 kutoka 2632.35 hadi 2632.96 huku sekta ya huduma za kibiashara ikibaki kama awali kwenye wastani wa pointi 2475.