26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

MAUWASA: Wananchi tunzeni miundombinu ya maji

Na Samwel Mwanga, Maswa

MWENYEKITI Wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Maswa, (MAUWASA), Paulina Ntagaye ametoa wito kwa wananchi kutunza miradi na miundombinu ya maji ili iweze kuwahudumia na hivyo kuondokana na tatizo la ukosefu wa maji.

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maji na usafi wa Mazingira mjini Maswa (Mauwasa)watembelea miradi ya Maji mjini Maswa mkoani Simiyu.

Pia amewaomba wananchi hao waweze kutuma maombi kuunganishiwa maji majumbani kupitia Mamlaka hiyo iliyoko wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.

Mwenyekiti, Ntagaye ameeleza hayo leo Ijumaa Machi 11, katika ziara  ya wajumbe wa bodi hiyo kutembelea miradi miwili ya maji inayotekelezwa na MAUWASA katika mji wa Maswa.

Akiongoza wajumbe hao katika ziara hiyo Mwenyekiti huyo wametembelea mradi wa uboreshaji huduma ya Maji Maswa mjini kwa ustawi wa taifa kwa maendeleo katika kupambana na maambukizi ya UVIKO-19 pamoja na ujenzi wa tenki lenye ukubwa wa lita Milioni moja linalojengwa kwenye kilima cha Nyalikungu mjini Maswa.

Mwenyekiti huyo ameeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa maji unaotokana na fedha za UVIKO-19  pamoja na ujenzi wa tenki hilo la kuhifadhi maji na kusema endapo miradi hiyo itakamilika itawawezesha wananchi kupata maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

“Niwaombe wananchi watunze  na kulinda hii miundombinu ya maji pia walete maombi kwenye ofisi za Mauwasa ili waweze kuunganishiwa maji kwenye majumba yao,”amesema.

Amesema kupitia fedha za UVIKO-19 Mamlaka hiyo imeweza kusambaza maji kwenye maeneo ambayo kulikuwa hakuna mtandao huku akitolea mfano Mitaa ya Jashimba na Mwanghuhi ambayo wananchi wa maeneo hayo awali walikuwa wakipata shida ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Pia ametumia fursa hiyo kuipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu kwa kuweza kuwapatia fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji kwa lengo la kumtua mama ndoo kichwani.

Naye Mwakilishi wa Wizara ya Maji katika bodi ya Mauwasa, Rosemary Rubigisa amesema kuwa serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo ya maji hivyo ni vizuri wakapatiwa elimu juu ya kuilinda na kuitunza ili iweze kuwanufaisha wao na vizazi vijavyo.

“Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maji kwa hapa Maswa tu Mauwasa imepewa fedha za UVIKO-19 zaidi ya Sh milioni 500 na fedha kwa ajili ya ujenzi wa tenki zaidi ya Sh milioni 400 hizi ni fedha nyingi hivyo ni vizuri miradi hii ikikamilika ilindwe na itunzwe maana ujenzi wake ni gharama sana tofauti na baadhi ya wananchi wanavyofikiria wanapoona maji yamewafikia majumbani,” amesema Rosemary.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Mhandisi Nandi Mathias amesema kuwa wamekuwa na utaratibu wa kufanya ziara kama hizo za kutembelea miradi wanayotekeleza ili wajumbe kupata hali halisi na kutoa ushauri wao kwa ajili ya uboreshaji ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Mhandisi Nandi amesema kuwa hadi kukamilika kwa mradi wa maji wa fedha za UVIKO-19 utagharimu kiasi cha Sh milioni 509.88 na hadi sasa wamepokea kiasi cha Sh milioni 246.46.

Katika ujenzi wa tenki amesema kiasi cha Sh milioni 497.37 zitatumika na hadi sasa wamepokea kiasi cha Sh 369.04.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles