30 C
Dar es Salaam
Saturday, June 10, 2023

Contact us: [email protected]

MAUWASA kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji Sangamwalugesha

Na Samweli Mwanga, Maswa

Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA) iliyoko katika Mkoa Simiyu imejipanga kuondoa changamoto ya upatikanaji wa Maji Safi na Salama kwa wananchi wa mji wa Sangamwalugesha wilayani humo.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Juni 21, 2021 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Mhandisi Mathias Nandi wakati akizungumza na wananchi wa mji huo katika mkutano wa hadhara juu ya tatizo la maji linalowakabili wananchi hao.

Amesema kwa sasa Mamlaka hiyo imepanga kuongeza mtandao wa maji ya bomba kwa kutandaza mabomba ili waweze kuwahudumia wakazi wote wa mji huo wapatao 8,676 kwa kuwaunganishia maji majumbani. Ameongeza kuwa kwa sasa wanawahudumia wateja 11 tu ndiyo waliounganisha maji tangu waanze kuendesha huduma ya usambazaji wa maji katika mji huo.

“Mtakumbuka ni hivi karibuni Serikali ilitutaka tuwahudumie wananchi wa Sangamwalugesha na ile Jumuiya yenu ya watumiaji maji ya zamani kwa sasa haipo mmehamishiwa Mauwasa hivyo jukumu la utoaji na usambazaji wa maji nilakwetu.”

“Tumekuta ni wananchi 4,822 tu ndiyo wanaopata maji safi na salama kwenye vituo vya kuchotea maji ila sisi tumejipanga kuongeza mtandao wa maji kwa kusambaza mabomba katika mji huu wa Sangamwalugesha ili watu wote 8,676 waweze kupata maji safi na salama kwa kuwaingizia maji majumbani ila hadi sasa ni watu 11 tu ndiyo waliongiza maji,” amesema Mhandisi .

Mhandisi Nandi pia alieleza katika mkutano huo kuwa kwa sasa wameamua kutengeneza chanzo kipya cha maji ili kiweze kukidhi mahitaji ya kuwahudumia wananchi hao kwani chanzo kilichoko kwa sasa hakitoshelezi na lengo la kufanya hivyo ni kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama.

Amesema kuwa  changamoto iliyopo kwa sasa ni ukosefu wa fedha ili waweze kufanya uboreshaji huo na tayari wameshaomba kiasi cha Sh milioni 100 serikali ili waweze kuondoa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa mji huo.

Pia amesema kuwa kwa sasa watahakikisha vituo vyote 13 vya kuchotea maji vilivyopo kwenye mji huo vinafanya kazi ili wananchi waweze kupata huduma ya maji.

Akizungumzia malalamiko ya wananchi juu ya gharama kubwa za kuunganisha maji majumbani kwa maunganisho mapya amesema kuwa sheria ya Mdhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) inawataka kuwaunganishia maji wananchi umbali usiozidi mita 60 kutoka bomba kuu.

Naye Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge ameiagiza Mauwasa kuhakikisha changamoto zilizopo za wananchi kushindwa kuingiza maji majumbani kutokana na kile kilichodaiwa gharama kubwa kushughulikiwa ndani ya mwezi mmoja.

“Niwaagize Mauwasa kero zote zile ambazo mnaweza kuzitatua zipatiwe ufumbuzi ndani ya mwezi mmoja mkazijadili kwenye bodi yenu ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama,”amesema.

Awali baadhi ya wananchi walieleza jinsi wanavyoshindwa kuunganisha maji kutokana na gharama kuwa kubwa ya maunganisho mapya ya maji na hivyo kushindwa kumudu.

Wamesema kuwa hata maji ambayo wamekuwa wakiyapata majumbani yamekuwa yakitoka kwa muda mfupi na kukatika tena hivyo kuwafanya kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwa kuchimba visiwa kandokando ya mito ambayo imezunguka mji huo.

“Hili suala la maji ni tatizo kubwa kwani tunatumia muda mwingi kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi katika nyumba zetu na hata hayo maji yanayotoka majumbani ni muda mfupi tu yanakatika kwa hali hiyo huwezi kuyachota na matokeo yake tunakwenda kwenye visima ambapo ni umbali mrefu,” amesema Mkadasi Maulid.

Aidha, waliiomba Mamlaka hiyo kulipatia ufumbuzi tatizo hilo la
upatikanaji wa maji safi na salama ili kuwaepusha kukumbwa na magonjwa ya MLIPUKO kama vile kutapika na kuharisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,409FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles