24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

Maumivu ya Ugaidi Kenya

*14 wafariki dunia, 700 waokolewa, Rais Uhuru Kenyatta atoa onyo kwa magaidi, washirika wao

Nairobi, Kenya

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amesema operesheni ya saa 16 ya kukabiliana na washukiwa wa ugaidi waliovamia Hoteli ya Dusit2 mjini Nairobi imekamilika na washambuliaji wote kuangamizwa.

Mbali ya hilo alisema watu waliouawa wamefikia 14 na waliookolewa kutoka eneo hilo maarufu kwa raia wa kigeni wakiwa zaidi ya 700.

Hata hivyo, Shirika la Msalaba Mwekundu, ambalo lilishiriki kikamilifu katika operesheni hiyo ikiwamo uokoaji limeripoti waliokufa katika mkasa huo kuwa ni 24.

Aidha kundi la al-Shabab, ambalo tangu mwanzo lilidai kuendesha shambulio hilo limetoa taarifa ya kuwa watu 47 waliuawa.

Kwa mujibu wa maofisa kulikuwa na magaidi watano waliouawa na vyombo vya usalama huku mmoja akijitoa mhanga. 

Juzi Jumanne, magaidi hao waliokuwa wamejihami kwa silaha walivamia jengo la hoteli hiyo ya kifahari yenye jumla ya vyumba 101, ambayo inapakana na Ubalozi wa Australia katika eneo la Westlands jijini Nairobi.

Kamera ya usalama ya CCTV ilionesha washukiwa wanne waliojihami kwa silaha wakiingia viunga vya jengo la hoteli hiyo, ambalo lina ofisi, hoteli pamoja na benki na kuanza kushambulia watu kwa kuwapiga risasi.

Kuna ripoti kuwa washambuliaji hao waliwahi kuonekana eneo la tukio siku za hivi karibuni, katika kile kinachoonekana kusoma mazingira.

Vikosi vya usalama vilifanya msako katika jengo hilo ambapo waliwakuta wafanyakazi waliojaa woga wakiwa wamejificha chini ya meza na hata bafuni, ambapo

kufikia alfajiri ya jana mamia ya watu walikua wameokolewa kutoka jumba hilo.

Karibu watu 30 wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali kadhaa za Nairobi.

Washambuliaji hao wanasemekana walikimbilia ghorofa ya saba ya jengo hilo ambako watu walikuwa wamejificha.

Milio ya risasi ilikuwa inasikika jana asubuhi, katika ghorofa hiyo ya saba ya hoteli, ikiwa ishara kuwa kulikuwa na makabiliano baina ya vyombo vya usalama na magaidi kwa siku ya pili.

Rais Kenyatta, Raila

Rais Uhuru Kenyatta amepongeza vikosi vya usalama kwa kazi nzuri ya kuwakabili magaidi hao.

“Magaidi wote wameuawa. Kwa wakati huu, tumethibitisha kuwa watu 14 wasio na hatia wameangamia kwa mkono wa wauaji hawa na wengine wakijeruhiwa,” alisema Rais Kenyatta.

Akihutubia taifa moja kwa moja kupitia televisheni, Rais Kenyatta amesema serikali yake itaendelea kuboresha usalama katika siku zijazo dhidi ya magaidi.

“Tumechukua tahadhari na tuko macho, nawahakikishia Wakenya na wageni kwamba mko salama nchini Kenya,” alisema Kenyatta na kuongeza.

“Sasa naweza kuthibitisha kuwa operesheni ya usalama katika jengo la Dusit imekamilika. Tutahakikisha kila mmoja aliyehusika na shambulio hili kwa njia moja au nyingine iwe ni kupanga, kufadhili au kutekeleza atakabiliwa vikali,” alisema huku akiapa kuwa serikali yake haitachelea kuwakabili vikali watu hao.

“Hili ni taifa linaloongozwa kupitia sheria. Taifa ambalo linajivunia amani upendo na umoja. Lakini ni lazima ieleweke kuwa hatuwezi kuwaachia huru wale wanaotudhuru sisi na watoto wetu,” alisema.

Kwa upande wake Kiongozi wa Upinzani nchini hapa Raila Odinga alitoa ujumbe wa salamu za rambi rambi kwa familia zilizopotewa na wapendwa wao katika shambulio hilo aliloliita la woga, ambalo kamwe halitawatisha Wakenya.

Naye Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya, Fred Matiangi amepongeza vyombo vya usalama akisema vimeokoa idadi kubwa ya Wakenya na raia wa kigeni.

“Kwa sasa tuko katika harakati za kukamilisha operesheni hii. Vyombo vya usalama vinaendelea kulipekua jengo na kutafuta ushahidi,” alisema Matiang.

Mmarekani aliyenusurika Septemba 11 miongoni mwa waliouawa

Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa kampuni ya Teknolojia, I-DEV International ya Marekani, Jason Spindler, ambaye alinusurika shambulio lingine la kigaidi la Septemba 11, 2001 nchini Marekani ni miongoni mwa waliokufa katika shambulio la Dusit.

Mama wa Jason, Sarah Sandler alikiambia kituo cha habari cha NBC News cha Marekani kuwa mwanae alikuwa akijaribu kutumia utaalamu wake wa teknolojia ya habari kuleta mabadilio chanya katika dunia ya tatu ya masoko yanayochipukia kiuchumi.

Kaka wa Spindler, Jonathan pia alithibitisha kifo hjicho kupityia Facebook.

Wizara ya Mambo ya Nje Marekani ilithibitisha kuwa raia wake aliuawa katika shambulio hilo.

CEO huyo wa I-DEV International, kwa mujibu ya wenzake alikuwa akipata chakula cha mchana katika Hoteli ya Dusit wakati shambulio lilipotokea.

Ofisi za I-DEV ziko katika jingo linguine eneo hilo hilo katika ghorofa ya sita.

Mbali ya Mmarekani, raia wa Uingereza pia ni miongoni mwa waliothibitishwa kuuawa.

Watoto wa vigogo wanusurika

Miongoni mwa watu wengi waliookolewa ni pamoja na binti wa Seneta wa zamani wa Kakamega, Bonny Khalwale na watoto wa kiume wa Kiongozi wa Chama cha ANC, Musalia Mudavadi na Mwakilishi wa Wanawake Vihiga, Beatrice Adagala.

AU, China, Marekani zalaani vikali

Wakati huo huo, mataifa mbalimbali yamelaani shambulio hilo wakilitaja kuwa la kipumbavu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alilitaja kuwa uvamizi mbaya wa kigaidi.

Kwa upande wake, Umoja wa Afrika (AU) umevisifu vyombo vya ulinzi na usalama vya Kenya kwa kuchukua hatua za uokozi wa raia na kupambana na wahalifu mapema iwezekanavyo.

Pia imesema tukio hilo linaonesha umuhimu wa kupitia upya mipango ya kuongeza nguvu kupambana na vikundi vya kigaidi barani Afrika.

“AU inathibitisha utayari wa kuendelea kufanya kazi kwa pamoja na nchi wanachama katika kupambana na visa vya ugaidi ikiwamo nchini Somalia kupitia vikosi vyake vya AMISOM.”

Balozi wa Marekani anayemaliza muda wake nchini Kenya, Robert Godec aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa Marekani inashutumu vikali shambulio hilo.

Amesema maafisa wote wa ubalozi huo wa Marekani wako salama na Marekani iko tayari kusaidia iwapo usaidizi wake utahitajika.

Naye Balozi wa Uingereza nchini Kenya, Nic Hailey, kwa upande wake aliahidi kutoa wataalamu kushirikiana na maofisa wa Kenya kuchunguza shambulio hilo.

Alizungumza na Rais Kenyatta kumhakikishia mshikamano baina ya Uingereza na Kenya kutokana na tukio hilo.

Jana asubuhi ubalozi huo wa Uingereza ulibakia kufungwa na uliwataka raia wake kuhakikisha simu zao za mikononi hazioneshi mahali walipo.

Ubalozi wa China pia ulitoa ujumbe wa kushikamana na Wakenya katka mapambano dhidi ya ugaidi.

Simulizi ya kilichojiri ndani ya hoteli

Nancy, ambaye jina lake kamili limehifadhiwa, ili kulinda utambulisho wake, alikuwa ndani ya majengo ya 14 Riverside Drive ambayo yana hoteli ya nyota ya Dusit D2 na ofisi kadhaa wakati mlipuko ulipotikisa ofisi yake dakika chache baada ya saa tisa kamili alasiri juzi.

Awali alikuwa na matumaini saa moja baadaye, angeondoka kuelekea nyumbani. Lakini hilo halikutokea.

Ni baada ya walinzi kuyaona magari matatu yakielekea katika jengo hilo.

Mmoja wa walinzi alijaribu kuyazuia magari hayo kwa vile eneo la ndani la kuegeshea magari lilikuwa limejaa, lakini magari hayo yaligoma kusimama.

Badala yake moja ya magari hayo lenye namba za usajiri KCN 340E, liliwatishia kuwagonga walinzi hao kabla ya kwenda kusimama kando ya kizuizi.

Watu watatu wenye silaha wakafungua milango ya gari na kutoka nje, wakiwaamuru walinzi kufungua kizuizi hicho.

Walinzi badala yake kwa woga wakakimbia na kuwaacha washambuliaji wakiwa huru kufanya lolote. Wakiwa mita chache tu kutoka shabaha yao, washambuliaji hao walifungua kizuizi na kuingiza gari ndani.

Ndani ya ofisi, Nancy aliendelea na shughuli zake bila kutambua kinachoendelea nje.

Katika eneo la kuegeshea magari, watu wengine wawili, dereva na abiria walishuka kutoka garini na kuungana na watatu wengine kuelekea Hoteli ya DusitD2 hotel.

Wakati wakikaribia eneo la wageni la hotelui, moja ya magari yaliyokuwa yameegshwa nje yakaripuka kwa kishindo kikubwa. Kisha kisanga cha kunusuru roho kikaanza hapo.

Washambuliaji walirusha grenade kuelekea Secret Garden, ambao ni mgahawa wenye matumizi mbalimbali.

Waliingia katika hoteli kupitia mlango wake wa jikoni na kuachia risasi wakati wakielekea eneo la kulia chakula. Polisi baadaye walisema mtu aliyejiotoa mhanga alionekana kutega bomu ndani ya mgahawa huo.

Nancy baada ya kishindo cha kwanza, akiwa amejaa woga, alikimbilia katika kona salama na kujificha na hivyo kuanza harakati za kusubiri kwa muda mrefu kitakachojiri kiwe cha heri au shari.

Awali kabla hawajaingia ndani ya mgahawa, wakiwa nje watu hao wenye silaha na kufunika nyuso zao baada ya kuingia kwa nguvu eneo la hoteli waliwarushia risasi walinzi na raia na kuingia katika mgahawa na kuwapiga risasi watu waliowakuta.

Jengo hilo, moja ya yale ya kifahari zaidi jijini Nairobi likawa ukanda wa vita na Nancy alijikuta katikati ya moto.

Kufikia saa 3.30 usiku wa juzi, Nancy alikuwa bado amejichimbia katika maficho yake, lakini alibakia kuwasiliana na vyombo vya habari kupitia ujumbe mfupi wa maneno.

Baada ya saa za milipuko na risasi, kimya kikatawala katika majengo hayo.

Nje, maofisa wa usalama na makomando walivamia jengo.

Nancy aliambiwa atulie maana hali ilionekana itadhibitiwa muda si mrefu, wakati akitumiwa ujumbe huo, alishikwa na kihoro wakati mlipuko uliposikika tena, aliandika Uuuwii! Hii inatisha. “Asante Mungu nilikumbuka kukaa mbali na madirisha,” aliandika.

Mlipuko huo ulikuwa umetikisa jengo na kupasua vioo vya madirisha. Siku hiyo ndefu ilionekana kuwa mbaya sana kwa Nancy.

Maofisa wa polisi kutoka kituo cha Polisi Gigiri walikuwa wa kwanza kufika eneo huku kiongozi wake,i Richard Muguai akiomba msaada wa askari zaidi kutoka vituo vingine na vikosi maalumu.

Kufikia saa 2.30 usiku, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Joseph Boinnet alisema gorofa sita kati ya saba zilikuwa zimedhibitiwa na hivyo kutarajia kurudisha hali kama kawaida wakati watakapowafurusha wahalifu kutoka gorofa iliyobakia.

Katika wakati huo huo, Nancy, ambaye aliokolewa baadaye baada ya kumalizika operesheni, alituma ujumbe kuwa anashuku sababu ya kuchelewa kuokolewa ni kwa vile washambuliaji walijificha karibu na walipojificha.

Nyumba aliyoishi gaidi yagunduliwa

Wapelelezi wameweza kuigundua jengo huko Mucatha, Kaunti ya Kiambu, ambako mmoja wa magaidi aliishi kwa miezi minne akilipa kodi ya Sh 40,000 za Kenya (Sh 800,000 za Tanzania) kwa mwezi.

Katika uvamizi waliofanya jana, polisi waligundua shimo ndani ya nyumba, ambamo mshambuliaji alihifadhi silaha kadhaa.

Majirani walimwelezea mtu huyo kuwa mwenye tabia ya kirafiki ingawa alionekana kuishi katika makazi hayo kwa nadra.

Mmoja wa majirani alipiga simu polisi baada ya kulitambua gari lililokuwa limetelekezwa karibu na geti la DusitD2, ambalo lilitumiwa na washambuliaji watano walioendesha shambulio hilo.

Al-Shabaab wapoteza nguvu

Eneo la 14 Riverside Drive linafahamika kwa utulivu, ufahari na amani hadi magaidi walipowasili saa tisa alasiri, wakivurumisha mabomu ya kutupa kwa mkono na kuteketeza magari matatu wakati wakiwa katika harakati za kupenya kuvuka vizingiti kuingia eneo hilo.

Ndani ya dakika chache, majengo ya DusitD2, ambayo yanahusisha ofisi, hoteli na migahawa yakachafuliwa na watu wenye taswira za kutisha na haikuchukua muda watu kadhaa wakajikuta wakiwa sakafuni wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa lakini washambuliaji wakiwa bado hawajafahamika.

Iwapo Al-Shabaab, ambalo linadhibiti sehemu kubwa ya maeneo ya vijijini hususani kusini mwa Somalia likitumia sheria kali za Kiislamu, Sharia, linahusika na shambulio la juzi, huo ni ujumbe kwamba bado kuna safari ndefu katika kuutokomeza ugaidi.

Shambulio dhidi ya hoteli ya DusitD2 limetokea katika siku ya maadhimisho ya tatu ya shambulio baya la El Adde nchini Somalia, ambalo lilishuhudia wanamgambo hao wakivamia kambi ya Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Afrika nchini Somalia (Amisom) Januari 15, 2016, na kuua askari zaidi ya 100 wengi wao wakiwa Wakenya, kwa mujibu wa takwimu zisizo rasmi.

Na inakuja wakati Marekani imeimarisha mashambulizi dhidi ya kundi hilo baada ya Ikulu ya Rais Donald Trump kuiruhusu Wizara ya Ulinzi kuimarisha operesheni za kupambana na kundi hilo.

Kama hiyo haitoshi, kuna ongezeko la mashambulizi yanayofanywa na ndege za kivita pamoja na kupelekwa kwa askari wa kwanza wa Marekani nchini Somalia tangu mwaka 1993, kuishauri na kuwasaidia askari wa serikali ya Somalia.

Zaidi ya hayo, Kamandi ya Marekani Afrika (Africom) imeendesha zaidi ya mashambulizi 46 ya anga nchini Somalia mwaka 2018.

Lakini wakati yote hayo yakionesha kupunguza uwezo wa kundi hilo kuandaa mashambulizi, Al-Shabaab linafahamika kuendesha mashambulizi katika maeneo nyeti wakati wowote. Hata hivyo, liko katika shinikizo kubwa, kwa mujibu wa vyanzo vya usalama.

Tangu shambulio la El Adde, kundi hilo limekuwa likijaribu kuendesha mashambulizi mjini Nairobi bila mafanikio.

Februari mwaka jana, polisi waliripotiwa kutengua shambulio kubwa mjini Nairobi baada ya kukamata washukiwa kadhaa wenye silaha huko Merti, Isiolo wakiwa njiani kuelekea Nairobi.

Washukiwa hao walikuwa wamekodi chumba mkabala na Kituo Kikuu cha Polisi Nairobi na watu wawili wanaoshukiwa kuwa sehemu ya kambi ya Al-Shabaab nchini humo pia walikamatwa. Haikuwa wazi majengo gani waliyalenga.

Juni 2017, vikosi vya usalama katika mji wa Bula Hawa nchini Somalia ulio karibu na mpaka wa Kenya na vilikamata washukiwa sita miongoni mwao wawili wakiwa Wakenya. Walikuwa gari wakielekea Kenya wakiwa na malighafi za kutengenezea mabomu.

Hilo likafuatiwa na shambulio kubwa dhidi ya roli katika mji wa Mogadishu Oktoba 2017, ambalo liliua watu zaidi ya 500. Shambulio hilo lilithibitisha kuwa vita ya mwongo mmoja dhidi ya wanamgambo huo bado iko mbali na hitimisho.

Shambulio dhidi ya DusitD2 ni moja ya mashambulizi makubwa ya Al-Shabaab katikati ya Nairobi tangu lile dhidi ya maduka ya kisasa ya Westgate, ambalo liliua watu 67 mwaka 2013 na shambulio dhidi ya Chuo Kuikuu cha Garissa lililoua watu zaidi ya 200 mwaka 2015.

Kabla ya hapo, kundi hilo kla kigaidi lililenga maeneo ya vijijini, kubwa zaidi likiwa la Juni 2014 huko Mpeketoni ambako watu zaidi ya 60 waliuawa.

Tangu hapo Shabaab imekuwa ikiendesha mashambulizi ya ‘lipua na kimbia’yakiwalenga askari na raia huko Lamu na karibu na miji ya mipakani. Pia wamekuwa wakishambulia magari ya abiria na kuua watu wasio wakazi wa eneo hilo.

Lakini makachero wameweza kusambaratisha sehemu kubwa ya kambi za mafunzo nchini humo kupitia mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ugaidi.

Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) lilienda Somalia Oktoba 2011 kile ilichokiita Operesheni Linda Nchi baada ya kundi hilo kulenga maeneo ya Kenya na raia.

Tatizo lilianza kwa kuteka wafanyakazi wawili wa misaada raia wa Hispania katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab, ikiwa ni siku chache baada ya kumteka mwanamke raia wa Ufaransa huko Lamu.

Miaka saba baada ya kuingia kwa askari wa KDF nchini Somalia wakishirikiana na jeshi la AU, Al-Shabaab limesukumiwa maeneo ya vijijini lakini kwa kushtukiza huendesha mashambulizi mabaya mijini.

Lakini pia operesheni za AU zimekuwa zikikabiliwa na changamoto nyingi kwa sababu nchi za magharibi haziko tayari kuingia moja kwa moja na kuwaacha askari wa Afrika pekee kupambana na kundi hilo ambalo linaungwa mkono na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda.

Pamoja na kukabiliwa na ukata jeshi la AU bado linabakia kubwa zaidi duniani la kulinda amani likiwa na askari 22,000 kutoka nchi sita ikiwamo Kenya, ambayo imekuwa mwathirika zaidi wa al-Shabaab iliyo kwenye harakati za kuiondoa serikali ya Somalia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles