27.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Mauaji ya wanawake yaibuka Arusha

Na WAANDISHI WETU

-ARUSHA/SIMIYU

WIMBI la mauaji ya raia limeendelea kushika kasi nchini huku Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akilazimika kutoa wiki moja kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha linafanya uchunguzi wa kina na kuwakamata watuhumiwa waliohusika na matukio ya ukatili wa ubakaji na mauaji ya wanawake eneo la Mto wa Mbu wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha.

Akizungumza na wananchi wa   Mto wa Mbu  jana, Waziri Lugola alimuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kushirikiana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo na kusimamiwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, kuhakikisha uchunguzi wa intelijensia unafanyika juu ya watu wanaohusika na vitendo hivyo vya ukatili.  

Lugola  alisema  haiwezekani wananchi wa eneo hilo wawe wanaishi kwa wasiwasi, wanateswa, kuuawa na kudhalilishwa wakati Serikali ya Rais Dk. John Magufuli ipo, polisi wapo  na wananchi wapo.

Alisisitiza  kwa hatua hiyo lazima mauaji hayo yafikie ukomo.

“Ndugu wananchi Serikali ya Dk. Magufuli haiwezi kuchezewa hata kidogo, lazima tudhibiti hii taharuki na tusipofanya hivyo, hii hali itaendelea kushika kasi jambo ambalo Serikali haiwezi kukaa kimya.

 “Kina mama wataisha kutokana na vitendo hivyo vya ukatili na lazima tuwe na uchungu sasa.

“Jeshi la Polisi lijipange vizuri kwa kufanya kazi ya weledi… kwa   wiki moja hakikisheni mnafanya kazi nzuri ipasavyo  kuwatia mbaroni hao watuhumiwa na kufunguliwa mashtaka haraka iwezekanavyo,” alisema Lugola.

Pamoja na hali hiyo, aliwatoa wasiwasi kina mama wa mji huo na kuwataka kutoa  taarifa za siri kuhusiana na wahusika hao kwa sababu hawatoki mbali bali katika mazingira hayo hayo wanayoishi. 

“Mmependekeza mpige kura za kimya kimya kwa kuwa uwanjani mkiandika majina ya watuhumiwa, mkihofia mkipeleka taarifa Kituo cha Polisi kwa njia ya siri mnahofia mtakuja kujulikana.

“Sijakataa njia mliopendekeza lakini polisi watafanya kazi hii ya  intelejinsia hapa kwa umakini na watawakamata watuhumiwa,” alisema Lugola.

Aliwataka wananchi hao kutoa ushirikiano wa kina kwa polisi  wakati wanafanya kazi zao.

Pia aliwapa angalizo polisi hao wasije wakakurupuka wakati wanafanya uchunguzi huo, wasiwaonee wananchi, wahakikishe wanakua makini wasije wakawasumbua  wananchi ambao wanafanya shughuli zao za  biashara.  

  Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Kigongoni, Kata ya Mto wa Mbu, Devotha Steven, aliiomba serikali iongeze nguvu katika kuwalinda wanawake wa Mto wa Mbu.

Alisema hiyo ni kwa sababu  vitendo vya ukatili vimekuwa vya kusikitisha na pia wanakosa amani popote wanapofanya shughuli zao za kutafuta riziki.

“Mheshimiwa Waziri, ninazungumza kwa machungu, kwa nini tunateseka na Serikali ipo, tunaamini mtasambaratisha haya mauaji, nasema kwa uchungu yatima wanaongezeka.

“Tunaomba tupige kura na wananchi waitwe kutoka Tarafa ya Manyara na Makuyuni ili wahusika wapatikane na tunaomba ulinzi utolewe kwa wale wananchi wanaotoa siri walindwe,” alisema Devotha.

 Mbunge wa   Monduli, Julius Kalanga (CCM), alimwomba Waziri Lugola   wawakamate wahalifu hao ambao wanafanya vitendo vya ukatili  ili ukatili huo uweze kukomeshwa. 

Waziri Lugola yuko mkoani Arusha kwa ziara ya  kazi   akifuatilia utendaji kazi wa taasisi  zilizopo ndani ya wizara yake. 

IGP Sirro kutua Simiyu leo

Wakati huohuo, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro, leo anatarajiwa kutua   katika Kata ya Lamadi wilayani Busega kutokana na kuibuka   mauaji ya watoto katika mazingira ya kutatanisha.

Hadi sasa zaidi ya watoto watatu wameuawa na watu wasiojulikana huku wananchi wakilazimika kupiga kura dhidi ya watu wanaohisi kuhusika na vifo hivyo.

Vilevile,  hadi sasa watu 12 wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo.

Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, ilieleza kwamba   IGP Sirro atakapowasili atakwenda hadi Lamadi ambako atafanya vikao na viongozi wa serikali pamoja na wananchi.

“Habari za jioni, kesho (leo) IGP Simon Sirro atakuja mkoani Simiyu   kutembelea eneo la mauaji katika mji wa Lamadi.

“Waandishi wa habari mnaombwa kufikia ofisi ya RC kwa ajili ya kuelekea Lamadi,” ilieleza taarifa hiyo ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa wanahabari.

Matukio ya kupotea   watoto wadogo katika mazingira ya kutatanisha kabla ya kukutwa wameuawa yanayotokea mkoani Njombe,   yanaonekana kuingia katika Kata ya Lamadi, Wilaya ya Busega mkoani Simiyu.

Matukio hayo yamesababisha  hofu kubwa kwa wakazi wa kata hiyo juu ya watoto wao ambako  wanafunzi watatu   wasichana wameuawa kinyama kwa nyakati tofauti.

Moja ya tukio ambalo limeongeza hofu kwa wananchi wa kata hiyo ni kuuawa kwa Joyce Joseph (8) mwanafunzi wa darasa la pili Shule ya Msingi Lukungu, mkazi wa Kijiji cha Lukungu.

Tukio hilo lilitokea Februari 8 mwaka huu na  mwili wa mwanafunzi huyo ulikutwa  umetupwa katika kichaka   kijijini hapo, baada ya kupotea kwa siku mbili.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Iseni ‘B’, Julias Baraza   siku moja kabla ya tukio hilo, mwanafunzi huyo aliondoka nyumbani kwao asubuhi kwenda shule lakini hakurejea nyumbani mpaka alipokutwa ameuawa na mwili wake kutupwa kichakani.

Matukio yaliyopita 

Tukio la kwanza lilitokea Oktoba 10, mwaka jana wakati mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Mwabasabi, Susana Shija (9)   wa Kijiji cha Lamadi, alipokutwa amekufa na mwili wake kutupwa kwenye jumba chakavu huku baadhi ya viungo vyake vikiwa vimeondolewa.

Mwili wa mwanafunzi huyo ulikutwa ukiwa hauna baadhi ya viungo vyake zikiwamo sehemu zake za siri, mikono yake yote miwili, miguu yote miwili na kuondolewa   nywele zake zote za kichwani.

Mama mzazi wa marehemu, Dina Halili, akizungumza  na waandishi wa habari kwenye eneo la tukio, alisema  mtoto wake alitoweka nyumbani katika mazingira ya kutatanisha wiki mbili zilizopita na akatoa taarifa Kituo cha Polisi Lamadi.

Katika tukio la pili, mtoto wa kike, Milembe    Maduhu (12), mwanafunzi wa darasa la saba,  naye alikutwa akiwa ameuawa ndani ya jengo linaloendelea kujengwa maeneo ya Lamadi   Desemba 13, 2018.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Deusdedit Nsimeki,  mwanafunzi huyo alikuwa akisoma shule moja wilayani Bunda (hakuitaja jina) na alipotea siku kadhaa akiwa anauza vitumbua mjini Lamadi, kabla ya mwili wake kupatikana katika jumba hilo.

Hofu kwa wananchi

Baadhi ya wananchi wakizungumza na Mtanzania mjini  Lamadi walisema   wameanza kuwakataza watoto wao kwenda kutembea au  kwenda kanisani peke yao huku wakilazimika kuwasindikiza kwenda shule.

Diwani wa Kata hiyo, Laurent Bija alisema   bado hajaweza kugundua wahusika wa matukio hayo, licha ya wananchi kuwataja baadhi ya watu ambao wana  shaka nao.

“Hofu ni kubwa   kwa wananchi wangu, hata mimi mwenyewe, maana nimelazimika kuwakataza watoto wangu wa kike wawili   kwenda kanisani au kutembea…lakini shuleni nawasindikiza asubuhi,” alisema Bija.

Mbali na diwani huyo baadhi ya wananchi walilalamikia jeshi la polisi wilayani humo kwa kuwakamata baadhi ya watu ambao walisema ni wahusika lakini wameachiwa.

Mmoja wa wananchi ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema  baada ya kufika matukio mawili, kuna baadhi ya watu walitajwa na wananchi kisha kukamatwa na polisi kwa   lakini walishangaa kuona siku chache watuhumiwa hao wameachiwa.

Hata hivyo, diwani  alisema   jeshi la polisi liliwaachia watuhumiwa hao baada ya kukosa ushahidi wa kuwapeleka mahakamani, licha ya kutajwa na wananchi kuwa inawezekana ndiyo wanahusika.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka  ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa     na wajumbe wa kamati hiyo   walikuwa na kikao  na wananchi   kujadili matukio hayo.

Februari 13, mwaka huu wananchi wa Kata ya Lamadi, Wilaya ya Busega  walipiga kura ya siri ya kuwataja watuhumiwa wa mauaji ya watoto wilayani humo.

Hatua hiyo inatokana na maazimio ya wananchi hao na katika kikao chao na na RC  Mtaka baada ya wananchi hao kusema hawana imani na polisi kutokana na kuwakamata wanaodhaniwa kuwa watuhumiwa na  kuwaachia.  

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,186FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles