Mauaji ya ushirikina yakosesha usingizi viongozi

Chiku Galawa
RC Chiku Galawa

 

Na Ibrahim Yassin, Tunduma

MAUAJI  yanayohusishwa na imani za ushirikina mkoani Songwe yameongezeka kwa kasi hali iliyosababisha Kamati ya Ulinzi na Usalama   kukutana kujadili itakavyokabiliana na hali hiyo.

Hilo lilibainishwa na wakazi wa Songwe kwa nyakati tofauti na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo.

Baadhi ya wananchi hao,Ajuaye Dimai na Elly Makenge kwa nyakati tofauti, walisema vimekuwapo vitendo vya  mauaji ya kinyama vya watu wananyofolewa baadhi ya viungo vya sehemu za miili yao, mauaji yanayodaiwa kufanywa kwa imani za kupata utajiri.

“Watu wanaofanya mauaji haya wamekuwa wakisaka utajiri kwa nguvu, wakitumia ushirikina kwa kuhitaji viungo vya binadamu yakiwamo macho, ulimi, vidole, moyo na vinginevyo, ambavyo wanavipeleka kwa waganga wa kienyeji.
“Kuna baadhi ya waganga wa kienyeji wanawarubuni wafanyabiashara kupeleka   viungo   wawatengenezee dawa kwa lengo la kupata utajiri.  Serikali isipochukua hatua hali itakuwa mbaya,”alisema Makenge.

Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Mathias Nyange, alisema ni kweli mauaji ya aina hiyo yamekuwa yakiendelea.

Alisema zikipita  saa sita hajapokea taarifa za mauaji ya aina hiyo siku hiyo hulala usingizi mzuri.

Nyange alisema kila siku zimekuwapo  taarifa za mauaji katika kila wilaya za mkoa huo.

Alisema  katika uchunguzi wa  polisi imebainika kuwapo   baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanaoendesha vitendo hivyo kwa imani ya kupata mafanikio.

Hata hivyo, Kamanda Nyange, alisema polisi wanajipanga kuendesha semina elekezi kwa wananchi kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za vijiji  kuwapa uelewa wananchi waachane na imani hiyo.

“Juzi tu maeneo ya Mbozi tumeokota mwili wa mtu ukiwa umeuawa na kutolewa macho,”alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani humo, Luteni (mstaafu), Chiku Galawa, alisema hata yeye alipofika mkoani humo alipata taarifa za   mauaji hayo yanayohusishwa na imani za ushirikina.

Galawa   alisema kwa sasa hakuna kulala na watahakikisha wanatembelea vijiji vyote mkoani humo kutoa elimu hiyo   jamii ijue wazi kuwa mafanikio hayaji kwa kuua bali ni juhudi za kufanya kazi kwa kujituma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here