24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Mauaji watoto Njombe yakutanisha waganga Iringa

RAYMOND MINJA- IRINGA

KUFUATIA mauaji ya watoto mkoani Njombe, Shirikisho la Waganga wa Tiba Asili Tanzania (Shivyatiata) Mkoa wa Iringa, limekutana na kuweka mikakati ikiwemo  kuhakikikisha hakuna mganga atakayefanya kazi za uganga ndani Iringa bila kibali kutoka serikalini.

Akizungumza katika kikao cha waganga wa tiba asili na jeshi la polisi, Mwenyekiti wa shirikisho hilo Abdi Simba, alisema kazi kubwa kwa waganga hao ni kuhakikisha wanashirikiana katika kutokomeza ramli chonganishi.

Alisema shirikisho hilo Mkoa wa Iringa litahakikisha hakuna mganga mgeni atakayeruhusiwa kufanya kazi kupitia leseni kutoka mikoa mingine.

Alisema Waganga wa tiba asili ambao wamekuwa wakitoa huduma ya tiba pasipo kujisajili, wanatakiwa kujisajili Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala ili waweze kutambulika kisheria.

Simba alisema waganga wa Tiba Asilia wanapaswa kuwa waaminifu na waadilifu kwa wateja wao, ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Aidha alitoa wito kwa Serikali kupiga marufuku matangazo ya waganga wa kienyeji kwa kuwa ni kinyume na sheria na ndio chanzo kikubwa cha kuwa na waganga matapeli.

Baadhi ya waganga wa jadi wakizungumza katika kikao hicho walisema kuna umuhimu wa waganga kushirkiana katika kutoa taarifa kwa jeshi la polisi endapo watabaini waganga feki na wapiga ramli chonganishi.

Walisema kuna baadhi ya waganga wamekuwa matapeli  na kuwadanganya watu mbalimbali kwa kupiga ramli chonganishi ambazo zimekuwa chanzo kikubwa cha mauaji ya watoto.

Mmoja wa waganga maarufu mkoani Iringa, Gallus Msekwa, alisema ifike wakati waganga wasitegemee kazi moja bali wajishughulishe na kazi nyingine zikiwemo kilimo na ufugaji kuliko kutegemea kazi ya uganga.

Msekwa ambaye ni mwenyekiti wa nidhamu wa waganga wa tiba asilia mkoa wa Iringa, alisema kuna umuhimu wa waganga wote kupatiwa elimu kwa sababu wengi wao hawana elimu na ndio chanzo cha kupiga ramli.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Iringa, Edith Swebe, akizungumza kwa niaba ya kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Iringa, alisema tasnia ya tiba asilia nchini imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika kutoa matibabu ya magonjwa mbalimbnali.

“Tumekuwa tukishuhudia mauaji, ubakaji ukiongezeka sisi wenzenu tuna dawati la jinsia na watoto ambao sasa tunazo data zinaibuka kila siku na tunajiuliza hivi vitu vinatoka wapi na chanzo chake ni nini? Hivyo kama vipo basi tujue na kushirikiana katika kutokomeza hii tabia” alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles