Christina Gauluhanga, Dodoma
JAMII imetakiwa kuhakikisha inatumia vyakula na matunda yanayozalishwa kwa kilimo hai ili kuepuka magonjwa yatokanayo na matumizi ya kemikali na viuatilifu.
Hayo yalielezwa jana jijini Dodoma katika mkutano wa kitaifa wa kilimo hai ulioandaliwa na Shirika la Kuendeleza Kilimo Hai (Toam), Shirika la Kimataifa la Chakula Duniani (Fao), Ubalozi wa Ufaransa na wadau wengine.
Akizungumza katika mkutano huo, mtaalamu wa lishe na chakula, Dk. Jacques Berger alisema wakulima kuendelea kutumia kilimo cha kisasa na kuacha cha asili watachangia kwa kiasi kikubwa kuathiri afya ya jamii.
“Kuendelea kutumia kemikali katika kuzalisha mazao ni kuzidi kuongeza idadi ya magonjwa katika jamii ambayo Serikali inazidi kubeba mzigo kwa ajili ya matibabu,” alisema Dk. Berger.
Alisema matumizi ya baadhi ya vyakula na matunda yenye kemikali yanaonyesha kuongeza idadi ya magonjwa ya uvimbe tumboni na kansa.
Dk. Berger alisema upatikanaji wa vyakula vya lishe na visivyo na kemikali utachangia kuleta taifa na jamii yenye afya.
Alisema wakati sasa umefika wa wakulima, Serikali na wadau mbalimbali kutumia fursa walizonazo kusambaza na kuuza vyakula vinavyozalishwa kwa kilimo hai.
“Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo baadhi ya mazao yake yana vimelea vya sumu inayosababishwa na wakulima kuweka mbolea au mbegu zenye kemikali.
“Upo umuhimu wa kuzingatia vyakula lishe ili kuepuka utapiamlo kwa kuwa kilimo na chakula ndio chanzo cha ugonjwa huo,” alisema Dk. Berger.
Alisema pia kuna changamoto ya tafiti ambazo nyingi bado hazijaweka bayana tofauti ya chakula cha kilimo hai na kile kinachotumia kemikali.
Dk. Berger alisema kemikali zina madhara katika udongo, mazingira na kiafya pia, hivyo ni vema jamii ikaepuka na kuendeleza kilimo hai pamoja na kulima mazao mseto.