33.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 19, 2021

Matumizi yasiyo sahihi ya barakoa tishio

KUNA kila dalili zinazoonyesha kuwa matumizi yasiyo sahihi ya uvaaji wa barakoa yanaweza kuwa tishio kuliko kutovaa kabisa.

Tangu uzuke ugonjwa wa virusi vya corona, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilishauri uvaaji wa barakoa kama mojawapo ya njia ya kuzuia kuenea kwa virusi hivyo, hasa katika maeneo yaliyoathirika.

Pamoja na kwamba WHO lilionya matumizi ya barakoa yanaweza kutengeneza hali ya kupuuza njia nyingine muhimu kama kusafisha mikono kwa kutumia maji tiririka au vitakasa mikono, hilo ndilo linaloonekana kuakisi matumizi ya wengi hasa katika viunga vya Dar es Salaam.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya watu hawazingatii matumizi sahihi ya uvaaji wa barakoa ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.

MTANZANIA Jumapili limeshuhudia baadhi ya watu wakivaa barakoa pasipo kuanza kusafisha mikono yao, wengine kujitishwa kichwani, chini ya kidevu, kuweka mifukoni na wengine wakijifunga mikononi.

Ukikatisha katika mitaa mbalimbali Dar es Salaam utakutana pia na baadhi ya watu ambao wameweka barakoa kichwani, wengine chini ya kidevu na wanapotaka kuvaa tena hawazingatii iwapo mikono yao ni misafi au inagusa midomo, pua na macho.

Wapo pia kina dada na kina mama ambao baada ya kutumia barakoa kwa muda, huamua kuzikunja na kuweka kwenye mikoba yao na kuendelea na shughuli nyingine  na pale watakapozihitaji tena huzichukua pasipo kusafisha mikono yao na kuzivaa tena.

Wapo pia kina kaka na kina baba ambao wameonekana wakiwa wamekunja na kuweka barakoa zao katika mifuko yao ya shati au suruali na pale wanapohitaji kuvaa au kuingia kwenye daladala utaona mara wanachomoa na kuvaa.

 Watu wanaopita mtaani watakubaliana na uchunguzi wa gazeti hili pia, kwamba lipo kundi ambalo linaonekana pia kuvaa barakoa chafu.

Barakoa hizo ni pamoja na zile zinazonunuliwa kwenye maduka ya dawa ambazo hushauriwa kitaalamu kuvaliwa na kubadilishwa kila baada ya saa nne hadi sita ili kujikinga vyema na magonjwa au matatizo ya upumuaji,  vikiwamo virusi vya corona.

Hata zile za vitambaa ambazo hushauriwa kufuliwa na kupigwa pasi, nazo baadhi wanaonekana kutozingatia utaratibu huo.

“Mimi hii barakoa nimenunua dukani sh 2,000 tangu Makonda (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda) alipotangaza tuvae, nina sijui mwezi, kwani kuna shida?” alisema Mohammed Athumani mkazi wa Tandale alipozungumza na gazeti hili baada ya kubaini amevaa ambayo si safi.

Alipoulizwa iwapo anafahamu matumizi sahihi ya barakoa, alijibu; “ Tumeishaambiwa tuvae, kwahiyo mimi nikiamka kwenda kwenye shughuli zangu naangaza iko wapi nagongelea ili nisiwekewe usiku na watu kama nyinyi, kwani kuna shida?”

Katika uchunguzi wake huo, gazeti hili limeshuhudia pia baadhi ya watu wakijaribisha barakoa moja baada ya nyingine zile zinazoshonwa kwa kitambaa na kuuzwa na watu mbalimbali barabarani.

Mteja anapojaribisha na kupata ile ambayo anaona inamtosha sawasawa huchukua hapo hapo na kuivaa bila kujali kama kuna mtu mwingine alijaribisha badala ya kuifua kwanza. 

Huko nyuma, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, aliwahi kueleza kuhusu matumizi sahihi ya barakoa kutokana na kuwapo mitazamo na mijadala tofauti tofauti kuhusu matumizi sahihi ya barakoa za vitambaa. 

Kwa mijibu wa Dk. Ndugulile barakoa za N95 zinapaswa kutumika na watoa huduma wa afya wanaohudumia wagonjwa wa Covid-19, kwamba hazipaswi kuvaliwa mitaani, majumbani wala maofisini.

 “Barakoa za upasuaji (surgical masks), hizi zinapaswa kuvaliwa na watumishi wa afya ambao hawana direct contact na wagonjwa, pia zinaweza kuvaliwa na jamii kwenye maeneo ya mikusanyiko kwa muda wa saa 4 hadi 6, pia hazipaswi kuvaliwa kutwa nzima na kurudia matumizi (re-use),” alisema Dk. Ndugulile. 

Alisema kumekuwa na sintofahamu kuhusu namna ya uvaaji wa barakoa za upasuaji ambazo zinatakiwa kuvaliwa kwa usahihi kama njia ya kujinga na maambukizi.

“Upande wenye rangi (blue, kijani, zambarau nk) unapaswa kuwa nje, upande wenye chuma unapaswa kuwa juu,” alisema Dk. Ndugulile.

Akizungumzia kuhusu barakoa za kitambaa, alisema nazo zinaweza kutumika ili kupunguza uwezekano wa maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine majumbani na sehemu za mikusanyiko, huku akitaka kuzingatiwa kwa kutumia vitambaa vya pamba.

 “Kutumia layers zaidi ya mbili katika utengenezaji wa barakoa hizo, kuwa na barakoa angalau mbili ili kuruhusu kufanyiwa usafi wa mara kwa mara, barakoa zifuliwe kwa maji na sabuni na kupigwa pasi,” alisema Dk. Ndugulile.

Alisema matumizi ya barakoa sio mbadala wa kunawa mikono au kuzingatia umbali kati ya mtu na mtu, bali ni nyongeza ya hatua hizo.

 “Tuhakikishe barakoa zilizotumika hazitupwi ovyo, badala yale zichomwe moto ili kuepuka kuokotwa na kutumiwa na watu wengine, vile vile watu hawapaswi kuazimana barakoa iliyokwisha kutumika, kila mtu awe na yake na kila mtu aendelee kuzingatia maelekezo yanayotolewa mara kwa mara na Wizara ya Afya kuhusu hatua mbalimbali za kujikinga na ugonjwa huu,” alisema Dk. Ndugulile.

Katika mwongozo wake kwa jamii jinsi ya kujikinga na virusi vya corona, Shirika la Afya Duniani (WHO) linasisitiza matumizi ya barakoa yanayozingatia utaratibu wa uvaaji wake, utoaji wake na jinsi ya kuziondoa kwenye matumizi kwa kuzingatia njia sahihi za usafi.

Lakini pia ili kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo WHO inashauri kutojigusa mdomo na pua.

Pia inashauri watu kukaa mbali na mikusanyiko mikubwa na kuwapo umbali wa angalau mita moja kati ya mtu na mtu, hasa wenye dalili za corona kama kukohoa au kupiga chafya. 

Zaidi WHO inashauri kuzingatia usafi mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kunawa mikono  kwa sabuni na maji au kutumia vitakasa mikono (sanitizer). 

Inashauriwa pia iwapo unakohoa au kupiga chafya, jizibe kwa kutumia kiwiko cha mkono au tishu ambayo ukimaliza matumizi yake unashauriwa kuitupa.

WHO pia inashauri mtu mwenye dalili za ugonjwa huo kuhudumiwa kwa kutengwa.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
156,882FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles