24.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Matumizi ya nishati jua, kichocheo kipya cha ufanisi kwa biashara za hoteli

ANDREW MSECHU – DAR ES SALAAM.

KUMEKUWA na malalamiko kuhusu kupanda kwa uzalishaji na uendeshaji katika biashara, hatua inayochochea kupanda kwa gharama kwa watumiaji wa mwisho kwenye huduma, zikiwemo za hoteli.

Hata hivyo, baadhi ya hatua zinazochukuliwa zinaonesha kuwa katika suala la gharama za nishati, matumizi ya nishati mbadala ya mwanga jua kumesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza gharama za nishati katika hoteli nyingi.

Katibu Mtendaji Tarea, Mhandisi Mathew Matimbwi anasema matumizi ya nishati ya mwangajua yamekuwa kimbilio kwa wafanyabiashara wengi katika maeneo mengi mijini na hata pembezoni mwa miji.

Maeneo haya ni yake yenye uhakika wa nishati ya umeme lakini wa gridi ya taifa, lakini tayari gharama za matumizi ya nishati hiyo yanawasukuma watumiaji kutafuta nishati mbadala kwa ajili ya kuhuisha gharama za uendeshaji.

Anasema miongoni mwao ni wafanyabiashara na wasimamizi wa biashara za hoteli, ambao wengi wameamua kuepuka matumizi ya umeme ambao ni gharama kubwa kwa kuweka vichemshio vya maji vinavyotumia nishati ya mwanga wa jua (solar heater).

Mhandisi Matimbwi anasema zipo hoteli ambazo tayari zimeshafungwa na zilishaanza matumizi ya mfumo wa uchemshaji amji kwakutumia nishati ya mwanga wa jua kuwa ni Rombo Green View iliyopo Sinza, JB Belmont-Benjamin Mkapa, JB Belmont PSPF Golden Jubilee, Tamali hoteli, Landmark Hoteli (Dar es Salaam) na Kiromo View iliyopo Bagamoyo.

Mhandisi Matimbwi anasema kwa kuwa gharama kubwa za umeme kwenye hoteli zinatokana na uchemshaji maji yanayotumika kwa shughuli mbalimbali, ipo haja ya wamiliki wa hoteli kutumia mfumo wa umemejua kwa kuwa gharama yake ni ya mara moja na isiyosumbua.

“Nishati ya mwanga wa jua hutumika kwenye hoteli kuchemsha maji ambayo yanahitajika sana na wageni, hapa unaweza kupunguza gharama za umeme na wenye hoteli wengi wanaweza kufaidika kupitia hii,” anasema.

Anasema umemejua ni wa uhakika, endelevu na unaondoa changamoto ya kukatika kwa umeme kwa sababu mionzi ya jua inapatikana wakati wote.

Matumizi ya umemejua yanaweza kusaidia katika utunzaji wa mazingira na kuvutia watalii kukaa katika hoteli zinazopatikana karibu na hifadhi za Taifa.

Akizungumzia namna walivyoanza matumizi ya umemejua kuchemshha maji katika hoteli yao, Meneja Rombo Green View, Benjamin Robert anasema walianza matumizi hayo kwa kufunga solar heater muda mrefu kidogo uliopita, kati ya mwaka 2000 hadi 2005.

Anasema walichukua uamuzi huo baada ya kuelezwa namna matumizi ya mashine hizi yanavyoweza kusaidia kupunguza gharama za umeme hasa katika kuchemsha maji ya vyumbani, suala ambalo hawajawahi kulijutia.

“Hoteli yetu ina vyumba vingi katika ghorofa kama tano, ambavyo iwapo tukitumia umeme katika kuchemsha maji tunatumia umeme mwingi sana.

“Tuliamua kuzifunga sola heater ili kupata unafuu katika kuchemsha maji ya moto kwenye vyumba vyetu kwa ajili ya kuogea na shughuli nyingine kwa wateja wetu.

“Tangu wakati huo tumekuwa tukinusuru fedha nyingi ambazo zingetumika kununua umeme ambao kwa sasa gharama yake ni kubwa, kwa hiyo umeme wa kawaida tunaendeela kutumia katika masuala mengine,” anasema.

Anasema walipokuwa wakitumia umeme wa gridi kuchemshia maji matumizi yalikuwa makubwa, gharama za umeme zilikuwa juu, lakini baada ya kubadilisha mfumo huo wanaona unafuu baada yaa kuamua kutumia umemejua.

Anaeleza kuwa matumiziya nishati ya umeme jua kuchemshia maji amesaidia kupunguza gharama za umeme kwa karibu shilingi milioni tatu kwa kwezi, kutoka Sh milioni 15 walizokuw awakitumia awali hadi Sh miliooni 12 kwa sasa.

Kwa upande wake, Meneja Mauzo na Masoko wa Peacock Hotel, Tabitha Kidawawa anasema wameona upo umuhimu wa kutumia sola heater na tayari wameshaanza utaratibu wa kuzifunga katika hoteli yao.

Anasema bado matumizi rasmi hayajaanza lakini wanaona itakuwa sehemu ya kuwezesha hoteli yao kupunguza gharama za uendeshaji kwa kuwa baada ya kuweka mashine hizo wana uhakika zitasaidia kupunguza matumizi ya umeme.

Anasema ni kweli kwamba umeme wa gridi ni muhimu sana, ila kutokana na gharama kubwa wanaona ipo haja ya kutafuta njia mbadala ili njia hizo zisaidie kupungua gharama za uendeshaji.

“Nishati mbadala kupitia solar heater imekuwa njia yao ya kwanza kwa ajili ya kujaribu kuitumia kuchemshia maji ya vyumba vya wateja ili kuepuka matumizi ya heater za umeme au mkaa.

“Kw amujibu wa maelekezo ya wataalamu, ninaona hii ni njia sahihi kwa kuwa solar heater zikishanunuliwa na kufungwa, kinachofuata ni gharama za matengenezo pale zinapoharibika, suala ambalo halitokei mara kwa mara,” anasema.

Anasema kwa sasa hawezi kukisia kwamba wanaweza kuokoa gharama kiasi gani, ila kwa kuwa wameshachukua uamuzi wa kuzitumia, wana uhakika zitakuwa na msaada mkubwa.

Nishati isiyoharibu mazingira

Kwa mujibu wa ripoti ya Informa UK Ltd kuhusu Ufanisi wa Nishati katika Hoteli iliyochapishwa mwaka 2018, inaeleza faida za matumizi ya nishati ya umemejua kuwa ni pamoja na utunzaji wa mazingira hatua ambayo huvutia watalii kwa kuwa hupendelea hoteli zinazothamini matumizi sahihi ya mazingira.

“Tatizo viongozi wa hoteli nyingi duniani hawana uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya nishati na zaidi hutupia lawama gharama kubwa za uwekezaji kwenye mfumo wa nishati mbadala,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Aidha, Rais wa Chama cha Wamiliki wa hoteli (HAT), Nuru Karamagi anasema matumizi ya umemejua kwa sasa yameshika kasi hasa kwa hoteli zilizopo pembezoni mwa miji ambako hakujafikiwa na umeme wa gridi.

“Awali walikuwa wanatumia zaidi umeme unaozalishwa na jenereta ila ujio wa solar kwa kiasi kikubwa umewaamsha wamiliki wengi kwani sasa wamebaini kuwa matumizi ya solar ni ya gharama nafuu kuliko kununua mafuta ya kuendeshea jenereta.

“Lakini zipo hoteli ambazo hutumia umeme wa solar katika baadhi ya maeneo mijini, ila ni hoteli chache kwa sababu wamiliki wengi wa hoteli zilizopo mijini ambazo zimefikiwa na umeme wa gridi, wanahisi ni gharama kubwa kubadilisha mfumo wa umeme katika hoteli yake ili kuweka umeme wa solar,” anasema.

Anasema sasa kuna muamko mkubwa wa matumizi ya nishati jadidifu kama ilivyo kwa umemejua.

Hata hivyo, anasema biashara ya hoteli bado haijatengamaa, ndio maana hoteli nyingi zilizofungwa miaka mitatu iliyopita hazijafunguliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles