26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Matumizi ya gesi asilia sio kwa ajili ya kundi maalum la watu-Dk. Kalemani

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amesema mpango wa kutumia gesi asilia haulengi kundi maalumu la watu wachache bali ni kwa ajili ya Watanzania wote.

Dk. Kalemani ameyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati akikagua mradi wa usindikaji wa gesi asilia (Compressed Natural Gas-CNG) itakayotumika kwenye mabasi yaendeyo kasi maarufu kama mwendokasi (Dar es Salaam Bus Rapid Transit – DART) katika kituo kinachoendelea kujengwa cha magari yaendayo haraka cha DART kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam ambacho awali kilikuwa ni kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani.

“Ni wasihi watanzania waanze kubadilisha mfumo wa magari yao kutoka kwenye mfumo wa mafuta kuja kwenye gesi kwani hii itaokoa pia uharibifu wa mazingira, mpango huu wa kutumia gesi hauko maalumu kwa ajili ya kundi flani la watu hapana bali ni kwa ajili ya Watanzania wote, hivyo niwasihi watanzania kutumia mfumo huu,” alisema Dk. Kalemani.

Aidha, amelitaka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kukamilisha ufungaji wa mitambo ya kusindika Gesi Asilia (Compressed Natural Gas – CNG) kwa matumizi ya magari ndani ya miezi sita.

Waziri Dk. Kalemani ameiagiza TPDC kutoa huduma hiyo si tu kwa magari 300 yaendayo kasi, bali pia kwa watumiaji binafsi ili kuongeza kipato kwa serikali, kuipunguzia DART gharama za uendeshaji na hivyo kuleta unafuu wa gharama za nauli ya mabasi kwa wananchi.

“Sitakuja kuzindua matumizi ya gesi asilia kwa magari 300 tu, hivyo ongezeni wigo wa watumiaji wa gesi asilia kwa magari mengine yakiwemo ya watu binafsi,” amesema Dk. Kalemani.

Kwa mujibu wa Dk. Kalemani, matumizi ya gesi asilia kwenye magari ya watu binafsi yataleta unafuu mkubwa wa gharama ikilingalishwa na matumizi ya petroli na dizeli kwa zaidi ya asilimia 45.

Vilevile, amewashauri wananchi kufunga mfumo utakaowawezesha kutumia gesi asilia kwenye magari yao ambao utawapa unafuu mkubwa katika matumizi ya magari yao.

Dk. Kalemani amesema, kwa sasa kuna magari takriban 800 yanayotumia gesi, hivyo amewashauri wananchi wenye magari na vyombo vingine vya moto waongeze mfumo utakaowawezesha kutumia gesi asilia, na kwamba, huduma hiyo ya kufunga mfumo kwa ajili ya kutumia gesi asilia inapatikana katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT).

Waziri Kalemani amesema, serikali imetenga jumla ya Sh bilioni 10 kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk. James Mataragio, alisema mradi huo umepangwa kuanza kutumiwa na mabasi 300 yaendayo kasi na ulipangwa kukamilika ndani ya miezi sita.

Alisema, kwa kuanzia, vituo vingine vinne vya usindikaji wa Gesi asilia vitajengwa katika maeneo ya Chuo Kikuu – Mlimani City, eneo la Feri, Muhimbili na Kibaha na ujenzi wa vituo hivyo unakwenda sambamba na ujenzi wa kituo cha magari yaendayo kasi cha DART kilichopo Ubungo.

Dk. Mataragio amebainisha kuwa, TPDC imepanga kujenga vituo vitano vya CNG ambapo kati ya hivyo, viwili vitakuwa vituo vikuu (CNG mother stations) na vitatu vitakuwa vituo vidogo (CNG daughter Stations) ambapo Kituo Kikuu kimoja kitajengwa eneo la Ubungo linalomilikiwa na DART maalum kwa mabasi ya mradi wa BRT uliozoeleka kama mwendokasi ambapo kitakuwa na uwezo wa kujaza gesi katika mabasi zaidi ya 300 kwa siku.

Aidha,  ameeleza kuwa, kituo Kikuu cha pili kitajengwa pembezoni mwa barabara ya Sam Nujoma katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es salaam ambapo kituo hiki kwa kuanzia kitakuwa na uwezo wa kujaza gesi katika magari zaidi ya 200 kwa siku na pia kitatumika kuhudumia vituo vidogo (CNG daughter stations) vitakavyojengwa katika maeneo mbalimbali.

Akizungumzia ujenzi wa vituo vidogo, Dk. Mataragio amesema, vituo hivyo vitajengwa eneo la Soko kuu la samaki Feri, Hospitali ya Muhimbili, pamoja na Galagaza-Kibaha katika eneo la ukanda wa viwanda.

Amesema, Kituo cha Muhimbili pamoja na Soko Kuu la samaki Feri vitakuwa na uwezo wa kuhudumia magari zaidi ya 200 kwa siku.

Dk. Mataragio, amemuahidi Waziri Kalemani kuwa, atahakikisha wanatekeleza maagizo yote aliyowapatia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles