26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Matumizi holela ya dawa yanavyosababisha ugonjwa sugu wa figo

share-kidney-failure

Na Veronica Romwald – Dar es Salaam

UTAFITI uliofanywa kati ya Agosti, 2014 hadi Februari 2015 katika Hospitali ya Bugando na Sekou Toure mkoani Mwanza kwa kuwapima watoto 513, ulibaini asilimia 16.2 walikuwa tayari wana matatizo ya figo.

Watoto waliokutwa na maradhi hayo waligundulika pia kuwa na ugonjwa wa malaria, seli mundu (sickle cell anaemia), maambukizi ya bakteria
kwenye koo na ngozi.

Aidha, wengi walikuwa wameanzishiwa matibabu ya kutumia mitishamba kabla hata ya kufikishwa hospitalini kufanyiwa vipimo zaidi.

Utafiti mwingine uliofanyika mkoani Kilimanjaro kati ya Januari na Juni 2014, uliohusisha watu 481 kutoka katika kaya 146, asilimia 7 walionekana kuwa na matatizo ya figo.

Utafiti huu ulionyesha uhusiano wa karibu kati ya uwepo wa tatizo la figo na ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu na matumizi ya mitishamba.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hivi karibuni.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa wizara hiyo, Catherine Sungura, anasema hadi kufikia Machi, mwaka huu jumla ya wagonjwa 190 walipata huduma ya kupandikizwa figo nchini India.

“Serikali imekuwa ikigharamia matibabu kwa asilimia 100, ni ghali mno wengi wanaweza kuwa na matatizo ya figo bila kujitambua hasa wale wenye magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu,” anasema.

Daktari

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto na Figo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Jacqueline Shoo, anasema ingawa ugonjwa wa shinikizo la damu na ule wa kisukari husababisha mtu kupata ugonjwa sugu wa figo lakini
matumizi holela ya dawa za kutuliza maumivu hasa diclofenac nazo husababisha maradhi hayo.

“Jamii yetu inapenda mno kutumia kitu kinaitwa self medication…yaani mtu akijisikia maumivu badala ya kwenda hospitalini kupima kujua tatizo ni nini huenda kununua dawa za maumivu mfano diclofenac na
kuzimeza pasipo ushauri wa daktari,” anasema Dk. Shoo.

Dk. Shoo anasema dawa hizo zinapotumika bila ushauri wa daktari ni hatari kwani zinaweza kusababisha hitilafu kwenye utendaji kazi wa figo na mwishowe mtu kupata tatizo hilo.

“Pamoja na dawa za kutuliza maumivu, dawa ya kutibu ugonjwa wa UTI iitwayo gentamacin nayo huchochea mtu kupata maradhi hayo ingawa zikitumika kwa usahihi hufaa kwa matibabu ya maumivu.

“Dawa za matibabu ya maambukizi ya njia ya mkojo yaani UTI zikitumika kiholela hasa hizi gentamicin husabisha figo kushindwa kufanya kazi, wapo watu wakijisikia maumivu wakati wa haja ndogo basi wanakimbilia
moja kwa moja duka la dawa, si sahihi kumeza kwa kujiamulia lazima umuone daktari,” anasisitiza.

Dk. Shoo anafafanua kwamba matumizi ya dawa za kienyeji au mitishamba ambazo hazijathibitiswa ubora wa viwango vyake nazo huchangia uwezekano wa mtu kupata maradhi hayo hasa kwa watoto.

Hali ikoje

Inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia nane hadi 16 ya watu duniani wanaugua ugonjwa sugu wa figo na tatizo hilo linazikumba zaidi nchi zilizoko katika ukanda wa Jangwa la Sahara ambako asilimia 13 ya watu katika nchi hizo wana matatizo ya figo.

Daktari huyo anasema ni vema jamii ikabadili tabia na kujiepusha na matumizi holela ya dawa mbalimbali na kufuata ushauri wa wataalamu.

Dk. Shoo anasema katika hospitali hiyo wamekuwa wakipokea wagonjwa kati ya 10 hadi 20 kwa mwezi ambao wamefikia daraja la tano na wanahitaji kupandikizwa figo au kuanza matibabu ya uchujaji damu.

“Tunapokea wagonjwa zaidi ya 100 wanaohitaji huduma ya kuchujwa damu kila siku na wengi wakiwa katika mchakato wa kupandikizwa figo kwa udhamini wa serikali,” anasema.

Watoto

Dk. Shoo anasema tatizo hilo pia huwapata watoto ambapo Muhimbili hupokea watoto 10 wanaougua magonjwa mbalimbali ya figo ambao
hupatiwa matibabu ya kliniki kila Jumanne.

“Wengi wao wakiwa na ugonjwa wa nephrotic syndrome ambao ni kama wa aina ile isiyokubali dawa za kawaida basi huweza kusababisha figo kufeli katika siku za usoni za utoto hao.

“Hivyo, katika kliniki hiyo watoto hupata uangalizi wa karibu wa afya zao pamoja na kupatiwa matibabu ya kuzuia figo zao kufeli kwa haraka.

“Kwa ujumla wagonjwa wengi huja wakati hali ya ugonjwa ikiwa katika hatua ya tano ambayo ni ya mwisho, mara nyingi katika hatua hii huwa
ni changamoto kunusuru maisha yao kutokana na madhara ambayo yanakuwa tayari yameshawapata kwa muda mrefu,” anasema.

Anasema kutokana na uhaba wa wataalamu wa figo katika hospitali nyingi hapa nchini, kuna changamoto kubwa ya kubaini tatizo la figo
likiwa katika hatua za mwanzoni.

“Pia inachangiwa na uhaba wa vifaa katika vituo mbalimbali vya afya ambavyo wagonjwa wetu hupatiwa matibabu ya awali wanapoanza kuona afya
zao haziko vizuri,” anasema.

Dalili

Daktari huyo anasema miongoni mwa dalili ambazo mtu anaweza kuziona ni kuvimba mwili kunakoanzia usoni, kupungua au kukosa kabisa haja ndogo, kukojoa mkojo wenye damu au rangi ya kahawia.

Anasema dalili nyingine ni shinikizo la damu, kuchoka mwili na kupungukiwa na damu.

“Dalili hizi hujitokeza baada ya figo kupata athari kubwa, hivyo inawezekana kabisa mtu kuwa na tatizo la figo bila kuwa na dalili lakini mara unapoona una dalili nilizozitaja hapo juu ni vizuri ukaenda hospitali ili upimwe na wataalamu na kupata matibabu au ushauri,” anasema.

Dalili za usugu

Anasema baadhi ya dalili zinazoashiria ugonjwa sugu wa figo ni kama vile kukosa haja ndogo, kuwashwa mwili, kutapika, kukosa hamu ya kula, kuvimba mwili na nyinginezo hasa ugonjwa unapofikia hatua ya tano.

“Changamoto iliyopo ni kuwa katika hatua za awali ya ugonjwa huu dalili huweza kudhaniwa ni za magonjwa yaliyozoeleka zaidi mfano malaria, typhoid na mengine ambapo dalili kama uchovu wa mwili, kutapika, kukosa hamu ya kula ni dalili za magonjwa hayo.

“Hivyo wagonjwa hutibiwa magonjwa hayo kwa muda mrefu kumbe tatizo ni figo,” anasema.

Shinikizo la damu

Daktari huyo anasema ugonjwa wa shinikizo la damu huwa hauna dalili za moja kwa moja hivyo ni lazima mtu apimwe ‘blood pressure’ ndipo agundulike kama anao.

“Sasa unapokuta vitu hivi havifanyiki mara kwa mara katika vituo vyetu vya afya hasa vile vya awali, hatimaye mtu anaweza kuja kugundua baadaye kwamba ana shinikizo la damu bila matibabu na
hivyo likasababisha kufeli kwa figo.

“Ni vyema watu wajenge utamaduni wa kwenda kupima afya zao mara kwa mara ili kujua kinachowasumbua badala ya kumeza dawa wao wenyewe,” anashauri.

Kuhusu hali ambayo husababisha figo ishindwe kufanya kazi  zake kabisa au kufanya kazi chini ya kiwango, anasema; “Hitilalafu hiyo husababisha mkusanyiko wa taka sumu ndani ya mwili ambazo huleta madhara mbalimbali na kusababisha dalili za ugonjwa wa figo na hata kusababisha umauti.

“Figo zilizoshindwa kufanya kazi vizuri kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu ambapo baada ya matibabu hurejea katika ufanisi wake wa kazi hujulikana kama acute kidney injury,” anasema.

Daktari huyo anasema tatizo hilo hutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kupatwa na malaria kali, maambukizi ya njia ya mkojo, kupoteza maji mengi mwilini, mfano kutokana na ugonjwa wa kuhara, kupoteza damu nyingi kwa mfano wakati wa kujifungua na sababu nyinginezo.

“Ugonjwa sugu wa figo huathiri hadi asilimia 20 ya watu wazima na zaidi ya asilimia 30 ya watoto wadogo ulimwenguni na kusababisha vifo
hadi asilimia 20 kwa wagonjwa waliopatwa na tatizo hilo,” anasema.

Anasema usugu hutokea pale ugonjwa wa figo unapokuwapo kwa kipindi cha zaidi ya miezi mitatu bila kutibiwa.

“Hili ni tatizo kubwa linaloathiri sehemu kubwa ya wagonjwa wa figo na kusababisha madhara makubwa kwa afya ya binadamu.

“Ugonjwa sugu wa figo umegawanyika katika madaraja matano. Daraja la tano ndilo ambalo wagonjwa wameathirika kwa sehemu kubwa sana na kuhitaji kupandikizwa figo nyingine au kusafisha damu kwa mashine ili kuondoa sumu mwilini na kunusuru maisha yao,” anasema Dk. Shoo.

Anasema katika madaraja ya awali yaani la kwanza hadi la nne, wagonjwa hutibiwa kwa dawa za kitaalamu na kushauriwa kuhusiana na lishe.

“Lakini matibabu ya daraja la tano ni ya utaalamu mkubwa unaogharimu fedha nyingi kote duniani na hivyo mkazo mkubwa katika matibabu ni kutoa elimu ya kinga ili kuzuia kupata ugonjwa wa figo pamoja na kutibu mapema madaraja ya awali ili kuzuia kufikia daraja la tano kwa haraka,” anasema.

Anasema magonjwa makuu yanayosababisha ugonjwa sugu wa figo ni kisukari, ugonjwa wa shinikizo la damu na magonjwa ya ndani ya
figo, saratani mbalimbali, maambukizi ya virusi vya Ukimwi na matumizi holela ya dawa za maumivu.

WAGONJWA

Nyaganya Donald (29) ni mmoja wa wagonjwa wanaotibiwa maradhi ya figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), anasema aligundulika kuwa na maradhi hayo Oktoba 23, mwaka jana.

“Wataalamu wanasema figo zinaposhindwa kufanya kazi sawasawa husababisha sumu zinazozalishwa mwilini kushindwa
kutoka nje kwa njia ya majimaji hasa kwa kutoa haja ndogo,” anasema Donald.

Anasema tangu alipogundulika kuwa na tatizo hilo amekuwa akihudhuria kliniki kwa wiki mara tatu kufanyiwa huduma ya kuchuja damu ‘dialysis’.

Donald anasema ingawa matibabu hayo yanamsaidia mgonjwa kuishi lakini yanagharimu fedha nyingi.

“Natakiwa kuhudhuria kliniki mara tatu kwa wiki, yaani Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kwa ajili ya kufanyiwa ‘dialysis. Matibabu ni ghali, kwa kila siku huwa natoa Sh 300,000. Hivyo kwa siku zote hizo ni Sh 900,000 kwa wagonjwa wenye bima za afya,”
anasema.

Anasema alijulishwa kuwa matibabu hayo husaidia kwa upande mmoja lakini yanayofaa zaidi ni yale ya kupandikiziwa figo.

“Daktari amenishauri niende nikapandikizwe figo kwani ndio njia nzuri zaidi ya kutibu maradhi haya.

“Nitapewa rufaa ya kwenda India kwa sababu matibabu hayo hayapo nchini kwa sasa, tayari nimepata mtu wa kunichangia figo ambaye ni mdogo wangu,” anasema.

Alivyoanza kuugua

Akisimulia jinsi ilivyokuwa hadi akapatwa na maradhi hayo, Donald anasema hafahamu kikamilifu tatizo lilitokana na nini ila anadhani lilichangiwa pia na matumizi yasiyo sahihi ya dawa za kutibu maradhi ya typhoid.

“Wakati fulani nilikuwa nasumbuliwa na typhoid nikaenda hospitalini wakaniandikia dawa, nilipotumia nilikaa kwa muda kidogo nikaanza kuumwa tena, nilipoenda kupima nikaambiwa bado nilikuwa na typhoid nikapewa tena dawa zilezile,” anasema.

Anasema alizichukua dawa hizo na kwenda kuzitumia, hata hivyo alikaa tena kwa muda mfupi na kuanza kuumwa tena dalili zikiwa kama za awali.

“Nilipoona bado naumwa na dalili ni zilezile safari hii sikurudi hospitalini kupima, nikajisemea mwenyewe kwa kuwa dalili ni zilezile maana yake ni kwamba bado typhoid inanisumbua. Kwa hiyo nilikwenda katika duka la dawa nikanunua tena dawa ile ile.

“Nikaenda nazo nyumbani na kuanza kuzitumia, maskini kumbe sikujua kuwa nilikuwa nazidisha dozi. Nilimeza dozi mbili ndani ya mwezi mmoja, nikazidi kuumwa, niliporudi hospitali walinieleza kuwa nilimeza
dawa zile kimakosa kwani nilipaswa kumeza dozi moja baada ya miezi miwili,” anasema.

Donald anasema tangu wakati huo aliendelea kuugua hadi alipopimwa na kugundua kuwa figo zake zimeathirika na kuanzishiwa matibabu hayo
ya dialysis.

“Namshukuru mdogo wangu aliyejitolea kunipa figo yake moja, ameshafanyiwa kipimo cha awali ambapo huwa wanaangalia makundi yetu ya damu, walikuta yameendana na sasa wanaendelea kumfanyia vipimo vingine kabla hatujaenda India,” anasema.

Anasema mbali na changamoto hiyo ya gharama anasema nyingine ni upotevu wa muda katika kufuatilia matibabu hayo.

“Mimi ni mtumishi wa serikali katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, imebidi niombe likizo na uhamisho kabisa ili nihamie Dar es Salaam kwa ajili ya kujitibia.

“Japo najitibia kwa kutumia bima lakini muda wangu mwingi unapotea, wakati mwingine nakuja kliniki saa tatu naondoka saa nane kwa sababu wagonjwa ni wengi na kila mmoja anahitaji huduma,” anasema.

Rufaa ya kwenda India changamoto

Anasema mchakato wa kupata rufaa kwenda India nao ni mrefu hali ambayo imekuwa ikiwakatisha tamaa wagonjwa wengi.

“Kwa mfano mimi nimechukua miezi sita sasa tangu nilipoanza kufuatilia rufaa ya kwenda India na bado sijafanikiwa, silaumu mtu naona hali hiyo
inatokea pengine ni kutokana na uhaba wa madaktari.

Mgonjwa mwingine

Alfred Sabuni (32) naye ni mmoja wa wagonjwa wanaotibiwa Muhimbili baada ya kupatwa na ugonjwa wa figo.

Sabuni anasema aligundulika kuugua maradhi hayo mwaka 2012.

“Nakumbuka nilipokuwa nasoma katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) nilikuwa napatwa na homa za mara kwa mara, nilikuwa natapika
mno, nikaenda hospitalini wakanipima hawakuona tatizo lolote linalonisumbua.

“Lakini walinipa dawa za malaria na typhoid wakiamini kwamba huenda nilikuwa nasumbuliwa na magonjwa hayo,” anasema Sabuni.

Anasema hata hivyo pamoja na kutumia dawa hizo bado aliendelea kupatwa na homa za mara kwa mara.

Anasema baadae alirudi Dar es Salaam lakini bado alipata homa na kutapika kuliendelea.

“Nikiwa Dar es Salaam nilikwenda Hospitali ya Tumaini nikakutana na daktari, aliponiona tu aliniambia nitakuwa nasumbuliwa na figo na akanishauri nifanye kipimo cha ultra sound,” anasema.

Anasema baada ya kufanyiwa kipimo hicho daktari alibaini kuwa figo zake zilikuwa zimesinyaa na kuwa ndogo ndogo, hivyo akamshauri kufika Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Kupata mchangiaji tabu

“Kupata mtu wa kukupatia figo ni changamoto, kuna vipimo vipatavyo 14 na vyote ikiwamo hicho cha ‘group’ la damu, mke wangu yupo tayari kunisaidia kupata figo moja na ameshaanza vipimo,” anasema Sabuni.

Anasema elimu ndogo kwa jamii kuhusu ugonjwa huo huwafanya baadhi ya watu kuwanyanyapaa wagonjwa wa figo.

“Unajua wengi hufika Muhimbili wakitokea katika mikoa mbalimbali nchini, tukiwa hapa kliniki tumekuwa kama ndugu sasa.

“Siku moja nilikwenda kumsalimia rafiki yangu ambaye naye ni mgonjwa tulikutana Muhimbili, alitokea Kigoma na hakuwa na ndugu wengine hapa Dar es Salaam zaidi ya huyo aliyekuwa amempokea.

“Siku hiyo alikuwa akimtolea maneno mabaya akimfukuza kwamba amechoka kumlea atafute pa-kwenda kuishi ili aendelee kujitibu, nilisikitika
mno lakini sikuweza kumsaidia kwa kuwa hali yangu si nzuri,” anasema.

Upandikizaji Muhimbili

Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru, anasema wamekusudia kuanzisha huduma ya upandikizaji figo hapa nchini ifikapo
Januari, mwakani.

“Hatua hiyo itasaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda nje kupata huduma hii. Tumepanga kupanua huduma za kusafisha figo
kwa kuongeza idadi ya mashine zetu kutoka 23 za sasa hadi kufikia 42,” anasema Profesa Museru.

Anasema tayari wataalamu 20 wakiwamo madaktari bingwa, wataalamu wa usingizi, wauguzi na wataalamu wa maabara wapo nchini India kujifunza
namna upandikizaji figo unavyofanyika.

“Kuna zaidi ya watu 100 wanaofika kupata huduma ya kuchuja damu kila siku, asilimia 80 wanahitaji kupandikizwa figo lakini kuwapeleka nje
ya nchi wote hawa ni gharama kubwa.

“Tunatarajia wataalamu wetu watarejea Desemba mwaka huu na huduma hiyo itaanza kutolewa Januari mwakani, pia tuna mpango wa kuchuja damu kwa watu wenye maambukizi ya Ukimwi na homa ya ini hapa Muhimbili,” anasema.

Figo ni nini
Figo ni kiungo kimojawapo kati ya viungo muhimu  katika mwili wa binadamu, hufanya kazi maalumu ya kuchuja taka sumu mbalimbali zilizotengenezwa ndani ya mwili, kazi yake kuu ni kusawazisha viwango
vya maji  mwilini na shinikizo la damu.

Pia husaidia katika utengenezaji wa vimeng’enyo muhimu vinavyochangia katika utengenezaji wa seli nyekundu za damu, husaidia ujengaji wa mifupa na kazi nyinginezo.

Kwa kawaida binadamu huwa na figo mbili, moja ikiwa katika upande wa kushoto na nyingine upande wa kulia sehemu za ubavuni.

Figo hupokea damu toka sehemu mbalimbali za mwili ambapo husafishwa kwa kuchujwa taka sumu ambazo hutolewa mwilini kwa njia ya haja ndogo
(mkojo).

Mkojo  hutengenezwa kutokana na maji na madini mbalimbali yakiwamo sodiamu, potasiamu, fosiforus, tundikali mbalimbali, urea, kreatinini
na nyinginezo ambazo zote kwa pamoja zinakuwa zimechunjwa na figo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles