27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Matumizi holela ya dawa yanavyosababisha homa ya ini

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


SIKU moja baada ya gazeti hili, kuripoti matumizi holela ya dawa yanavyoathiri ini na figo, Meneja Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani, Elimu kwa Umma wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Maguha Stephano, ameeleza jinsi dawa hizo zinavyoweza kusababisha homa ya ini.

Akizungumza na Mtanzania jana, Dk. Stephano alisema: “Matumizi ya dawa yanapaswa kufanyika kwa umakini na uangalifu kwa sababu zipo baadhi ya dawa ambazo zikitumiwa isivyopaswa huathiri ini moja kwa moja.

“Kimsingi, mtu anapomeza dawa kupitia kinywa huenda moja kwa moja tumboni, huko kuna ‘process’ ambayo hufanyika ili mwili upokee kile kinachohitajika kwa ajili ya kutibu.

“Baada ya mwili kupokea kile kinachohitajika, kile kisichohitajika (uchafu) hutolewa nje ya mwili kupitia ini, matumizi yakiwa holela mtu anaweza kujikuta ametumia kiwango kingi cha dawa na hivyo kuliweka ini lake katika hatari zaidi kuathirika.”

Dk. Stephano alisema matumizi holela ya dawa huweza baadae kumsababisha muhusika kuishia pia kupata ugonjwa wa homa ya ini.

“Ni ugonjwa hatari kuliko Ukimwi, sababu nyingine inayochangia mtu kupata homa ya ini ni kutokana na maambukizi ya virusi vya Hepatitis hasa A, B na C.

“Matumizi kupita kiasi ya pombe nayo huchangia pamoja na wakati mwingine inaweza kusababishwa na seli za mwili kupambana zenyewe kitaalamu tunaita ‘auto immune’,” alisema Dk. Stephano.

Daktari huyo alisema tangu Septemba 12, mwaka huu taasisi hiyo imeanza kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa huo na kwamba huduma hiyo ni endelevu.

“Kirusi cha Hepatitis A huenea kwa njia ya chakula au maji machafu (chenye/yenye vimelea vya kirusi hiki) ni kama vile ugonjwa wa kipindupindu unavyoenea, kirusi cha Hepatitis B na C vyenyewe huenea kwa njia ya majimaji ya mwili kwa mfano kwa kujamiiana na mtu mwenye maambukizi, kuchangia vitu vyenye ncha kali au maambukizi yanayoweza kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kipindi cha ujauzito,” alisema.

Alisema dawa za kienyeji ambazo hazijathibitishwa na mamlaka husika nazo ni hatari kwa ini.

Juzi, akizungumza na MTANZANIA, Rais wa Chama cha Wanafunzi Wafamasia Tanzania (TAPSA), Issaya Mbwilo alisema jamii bado haina uelewa wa kutosha juu ya matumizi sahihi ya dawa.

“Kimsingi kila mtu ana dozi yake na kila dozi ina uwezo wake wa kutibu, lakini unakuta mtu anachukua dozi iliyoachwa na mtu mwingine anaitumia akiamini atapona ugonjwa unaomsumbua jambo ambalo ni kosa,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo sasa chama hicho kimeanzisha kampeni maalumu ya kuelimisha jamii kupitia shule za msingi, sekondari na vyuo kuhusu matumizi sahihi ya dawa.v

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles