24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Matukio ya watoto kuibiwa, wanafunzi kutoroshwa yamgusa DC

 Na Ahmed Makongo-Bunda

MKUU wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili amesema  kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu yametokea matukio mbalimbali ya ukatili wilayani hapa, yakiwemo ya wizi wa watoto na utoroshaji wa wanafunzi na kuwapeleka kusikojulikana.

Bupilipili aliyasema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa uwakilishaji na utekelezaji wa miradi ya Serikali katika wilaya hiyo kwa kipindi cha miaka mitano chini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya tano.

Alisema kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, matukio mawili ya wizi wa watoto wawili yaliripotiwa na kwamba katika kipindi hicho pia wanafunzi 29 walipatiwa mimba na kukatisha masomo yao.

“Kwa kipindi hicho watoto wawili waliibwa na pia wanafunzi 29 walipatiwa mimba, hii ni hatari sana inabidi tujitathmini sana Bunda,” alisema Bupilipili. 

Aidha, alisema katika kipindi hicho wanafunzi 19 wa kike walitoroshwa na kupelekwa kusikojulikana na pia watoto 19 walibakwa.

“Wanafunzi 19 walitoroshwa na kupelekwa kusikojulikana… hivi ni wapi huko kusikojulikana?” alihoji Bupilipili.

Alisema matukio mengine ni ya ukatili kwa makundi ya wanawake na watoto kwa kuwashambulia kwa kipigo na kudhuru mwili, na kwamba katika kipindi hicho yameripotiwa matukio 139.

“Kuna matukio mengi ya ukatili wa watoto na wanawake, kwa kuwashambulia na kuwadhuru mwili. Watu wanadundwa kwelikweli wanawafanyia ukatili huo,” alisema Bupilipili.

Aliongeza kuwa matukio ya kuzuia wanafunzi kuendelea na masomo katika kipindi hicho zimepokewa taarifa tano, ambapo pia kuna taarifa za wanaume kutelekeza familia zao na kuongeza kuwa matukio mengine yanasababishwa na mimba za utotoni.

Aidha alisema kuwa familia nyingine na baadhi ya wanajamii wamekuwa wakificha ushahidi wa matukio hayo na kutotoa ushahidi kwa vyombo husika pindi wanapohitajika.

Alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wote pamoja na viongozi mbalimbali, wakiwemo wa madhehebu ya dini kukemea vitendo hivyo.

Mkutano huo wa uwakilishaji wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano umeshirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo wilayani hapa.

Katika mkutano huo, Bupilipili aliwasilisha miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika wilaya hiyo yenye jumla ya halmashauri mbili ambazo ni halmashauri ya wilaya na halmashauri ya mji wa Bunda.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles