31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MATUKIO YA KUKUMBUKWA KATIKA MICHEZO 2016

dogo-lee

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO

ZIMEBAKI siku 12 kuweza kusherehekea mwaka mpya wa 2017 na kuuaga mwaka 2016, ndani ya siku 365 za mwaka 2016 kuna mambo mbalimbali yalijitokeza, yakiwa ya furaha na mengine yenye kutia simanzi.

Leo hii Mtanzani SPOTIKIKI limekuandalia matukia mbalimbali ambayo yalitokea katika michezo, huku mengine yakiwa ya furaha na mengine simanzi.

Kifo cha Muhammad Ali

Alikuwa nyota wa ngumi duniani ambaye alizaliwa Januari 17, mwaka 1942 nchini Marekani, aliweka historia kubwa katika mchezo huo kutokana na kutwaa mataji mengi.

Bondia huyo ambaye alikuwa na urefu wa futi 6 na inchi 3, sawa na Cm 191, alifanikiwa kupigana jumla ya mapambano 61, huku akifanikiwa kushinda mapambano 56, huku 37 akishinda kwa KO na 5 akipoteza kwa kuchezea kichapo.

Bondia huyo alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi kwa muda mrefu tangu alipostaafu mchezo huo, lakini ilipofika Mei mwaka huu hali yake ilizidi kubadilika siku hadi siku na hatimaye alipoteza maisha Juni 3, nchini Marekani. Kifo cha bondia huyo kiliwagusa wengi, hasa wale ambao walikuwa wanafuatilia ngumi duniani.

Usajili wa Paul Pogba

Ilikuwa Agosti 8 mwaka huu ambapo ulimwengu wa soka ulisimama na kupokea taarifa za usajili wa kiungo wa Juventus, Paul Pogba, ambaye alirudi katika klabu yake ya zamani ya Man United.

Hii ilikuwa historia mpya katika soka kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 kusajiliwa kwa kitita kikubwa cha fedha duniani, ambapo alichukua pauni milioni 100.

Ilikuwa historia ya pekee katika soka duniani, ikiwa kabla ya mchezaji huyo kuweka rekodi hiyo mpya iliyokuwa inashikiliwa na Gareth Bale, ambaye alijiunga na Real Madrid akitokea Tottenham kwa kitita cha pauni milioni 85.

Bifu la Toure na Guardiola

Yaya Toure ni nyota wa klabu ya Man City ambaye anacheza nafasi ya kiungo ndani ya klabu hiyo, nyota huyo amekuwa akitoa mchango mkubwa tangu kujiunga kwake akitokea klabu ya Barcelona mwaka 2008.

Kuondoka kwa mchezaji huyo ndani ya Barcelona kulitokana na kuwa na mgogoro na kocha wake wakati huo, Pep Guardiola, hivyo kocha huyo aliamua kumuuza kwa Man City na kusababisha wawili hao kuwa na bifu.

Bifu la wawili hao liliendelea mara baada ya kocha huyo kusaini mkataba wa kuitumikia Man City, ambapo mkataba huo ulikamilika Februari, mwaka huu.

Lakini kocha huyo alikuja kujiunga na klabu hiyo wakati wa majira ya joto, hapo ndipo bifu la wawili hao lilianza tena, hata hivyo, wakati wa tetesi za usajili wa kocha huyo Toure alipanga kutaka kuondoka kwa kuwa hakutaka kufanya kazi na kocha huyo.

Baada ya Guardiola kuwasili ndani ya klabu huyo alionesha wazi kuwa hana maelewano mazuri na kiungo huyo, ambapo mara kwa mara aliwekwa benchi ndani ya kikosi chake.

Kwa sasa wawili hao wanaanza kuelewana mara baada ya mchezaji huyo kuomba radhi kutokana na tofauti zao, lakini bado Guardiola hajampa nafasi ya kudumu mchezaji huyo.

Murray kuongoza kwa ubora

Huyu ni nyota wa mchezo wa tenisi kutoka nchini Scotland, amefanya makubwa msimu wa mwaka 2016 tofauti na miaka ya hivi karibuni.

Kujituma kwake katika michuano mbalimbali kama vile Wimbledom kulimfanya mchezaji huyo aweze kushika nafasi ya kwanza kwa ubora duniani katika michuano hiyo.

Nafasi hiyo alikuwa anaiwania kwa kipindi kirefu zaidi ya miaka 20, lakini amekuja kufanikiwa mwaka huu huku akimgaragaza mpinzani wake, Novak Djokovic.

Ajali ya Chapecoense

Ilikuwa Novemba 28 mwaka huu, ambapo taarifa mbaya katika ulimwengu wa soka ilitanda kwamba ndege ambayo ilibeba jumla ya watu 82 ilianguka nchini Colombia na kupoteza maisha ya watu 76.

Katika ajali hiyo kulikuwa na wachezaji wa klabu ya Chapecoense ya nchini Brazil, ambao walikuwa wanakwenda nchini Colombia kwa ajili ya kucheza mchezo wa fainali ya kwanza ya michuano ya Copa Sudamericana dhidi ya wapinzani wake, Atletico Nacional.

Ajali hiyo ilipoteza maisha ya wachezaji 19 wa klabu hiyo ya Chapecoense pamoja na viongozi wa klabu hiyo, huku wachezaji watatu wakinusurika na kifo.

Lilikuwa ni tukio ambalo liliwagusa wengi katika michezo na maisha ya kawaida na kutokana na klabu ya Atletico Nacional kuguswa na vifo vya wachezaji hao, waliamua kuliomba shirikisho la soka Amerika ya Kusini kuwapa ubingwa huo wapinzani wao kama sehemu ya heshima ya mwisho.

Hiyo ni ajali ambayo imetikisa kwa mwaka 2016 kwa upande wa michezo, hivyo itakumbukwa sana kwa kipindi hiki, hasa pale timu itakapopigana kutafuta nafasi ya kuendelea kukaa sawa kwenye soka.

Oscar Pistorius

NI mwanariadha mlemavu kutoka nchini Afrika Kusini, alikutwa na hatia mwaka 2013 baada ya kumuua mchumba wake Reeva Steenkamp kwa kumpiga risasi mara nne eneo la kifuani.

Kesi ya mwanariadha huyo ilikuwa inasogezwa mbele kila mara kwa ajili ya kuwapa maofisa nafasi ya kufanya uchunguzi juu ya tukio la mauaji ambalo lilifanyika siku ya sikukuu ya wapendanao mwaka 2013.

Hata hivyo, nyota huyo wa mbio alikanusha kwamba ameua kwa kukusudia, huku sheria ikimtaka aende jela miaka 15 na wakati huo familia ya marehemu Reeva ikidai kuwa adhabu hiyo ya miaka 15 ni michache sana.

Julai mwaka huu hukumu ya mwanariadha huyo ilitolewa jijini Pretoria, Afrika Kusini chini ya jaji Thokozile Masipa, ambapo Pistorius alihukumiwa kwenda jela miaka sita, tofauti na vile ambavyo wengi walidhani.

Hukumu hiyo ilileta wakati mgumu na maswali mengi, huku familia ya Reeva ikiamini kuwa mwanariadha huyo amependelewa kwa kiasi kikubwa.

Hata hiyo, mwezi mmoja kabla ya hukumu hiyo, wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake, timu ya wanasheria wake ambao walikuwa wanamtetea mteja wao walimshauri kuvua miguu yake ya bandia na kutembea kwenye chumba cha mahakama bila miguu hiyo.

Hatua hiyo ya kuvua miguu ya bandia iliyomfanya ashindwe kusimama vizuri ilikuwa na lengo la kumshawishi jaji ili auone udhaifu wake na kuamua ama amhukumu kutumikia jela kwa muda mfupi, tukio hilo lilileta gumzo kubwa.

Pistorius ameweka historia kubwa katika mchezo wa riadha kwa upande wa walemavu, ambapo aliwahi kufika nusu fainali katika michuano ya Olimpiki kwa kukimbia umbali wa mita 200 mwaka 2012 jijini London, nchini Uingereza.

Rigobert Song kuzushiwa kifo

Alikuwa nyota wa soka wa timu ya taifa ya Cameroon pamoja na klabu ya Liverpool, alifanya makubwa katika soka, huku akiwa timu ya taifa ambapo alianza kucheza soka huku akiwa na umri wa miaka 17 ndani ya kikosi cha Taifa.

Kipindi anaanza kuitumikia timu ya taifa alionekana ni mchezaji pekee mwenye umri mdogo ndani ya kikosi hicho, huku akicheza nafasi ya ulinzi wa kati kabla ya kuanza kupata nafasi nyingine za kucheza kama vile West Ham.

Tukio lake ambalo lilitikisa dunia mwaka huu ilikuwa kuanzia Oktoba tatu ambapo kulienea taarifa kwamba mchezaji huyo hali yake ni mbaya na amekimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu nchini Cameroon, kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi.

Siku mbili baadaye taarifa zilienea kwamba mchezaji huyo amepoteza maisha wakati anasafirishwa kwenda nchini Ufaransa kwa ajili ya matibabu kutokana na hali yake kuwa mbaya.

Taarifa kwenye mitandao mbalimbali zilienea, ikiwamo katika klabu yake ya zamani ya West Ham, ambao waliposti taarifa hiyo kwamba mchezaji wao wa zamani amefariki, lakini hakukuwa na ukweli wowote, ila mchezaji huyo alikuwa amepoteza fahamu.

Hadi sasa bado anaendelea vizuri na yupo hospitali kwa ajili ya matibabu, hata hivyo, mwanzoni mwa Desemba mchezaji huyo alionekana kupata nafuu zaidi na kuweza kuongea na mashabiki wake kupitia mitandao ya kijamii.

Hili ni tukio ambalo liliwagusa wapenzi wa soka nchini Cameroon, barani Afrika na duniani kote kwa ujumla.

Hodgson kujiuzulu England

Alikuwa kocha wa timu ya taifa ya England kwa miaka minne hadi kufikia Julai mwaka huu tangu 2012 alipojiunga na timu hiyo na kupewa imani kwamba anaweza kuipeleka mbali, hasa katika michuano ya Euro, lakini hakuweza kufanya hivyo kutokana na kukutana na ushindani mkubwa dhidi ya wapinzani wake.

Katika michuano ya Euro mwaka huu ambayo ilifanyika nchini Ufaransa, ilikuwa ni nafasi yake ya mwisho kuifundisha mara baada ya kutolewa mapema dhidi ya wapinzani wao, Iceland, kitendo ambacho kilikuwa ni aibu kwa timu kubwa kama hiyo kufungwa na kisiwa cha Iceland.

Kabla ya kutolewa katika michuano hiyo kulikuwa na tetesi kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kocha huyo kufukuzwa kama atashindwa kufanya vizuri, hivyo baada ya kutolewa na Iceland aliona atangaze mapema mwenyewe kuwa anajiuzulu nafasi hiyo hata kabla ya chama cha soka kutangaza kumfukuza kocha huyo.

Kujiuzulu kwa kocha huyo kulitikisa katika vichwa vya habari mbalimbali barani Ulaya, lakini baada ya siku chache nafasi ya kocha huyo ikachukuliwa na Big Sam tangu Julai 22, lakini hata yeye hakuweza kudumu, aliitumikia timu hiyo kwa siku 67 hadi Septemba 27 ambapo walivunja mkataba wa miaka miwili.

Hayo ni baadhi ya matukio machache ambayo yaligusa vichwa vya habari kwa mwaka 2016.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles