30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MATUKIO MUHIMU YALIYOACHA HISTORIA YA NAPE NNAUYE KWENYE MICHEZO

Na ZAINAB IDDY


ALHAMISI ya wiki iliyopita, Rais Dk. John Magufuli, alifanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri kwa kumwondoa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na nafasi yake kuchukuliwa na Dk. Harrison Mwakyembe.

Nape ameondolewa kwenye nafasi hiyo akiwa tayari ametimiza mwaka mmoja na miezi miwili ya uongozi wake kwenye wizara hiyo.

Kipindi akiwa katika nafasi hiyo yapo mengi yaliyojitokeza ambayo yanaacha kumbukumbu kwa wadau wa michezo nchini.

SPOTIKIKI inakuletea baadhi ya mambo hayo yatakayoweka kumbukumbu, pamoja na kauli za wadau wa michezo juu ya kuondolewa kwake na kipi wanakitarajia kwa waziri anayevaa viatu vyake.

Bajeti ya michezo 2016/17

Katika mwaka wa fedha 2016/17, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, bajeti yake ilipungua kwa asilimia 21, ukilinganisha na mwaka uliopita wa fedha.

2015/16, wizara hiyo iliidhinisha Sh bilioni 21.957 kwa matumizi ya kawaida, lakini mwaka huu wa fedha ulioanza Julai mwaka jana zilitengwa Sh bilioni 17.326, ikiwa ni punguzo la Sh bilioni 4.631 sawa na asilimia 21 jambo lililoonekana kutokubalika kwa wadau wengi wa sekta hiyo.

BMT yatumbuliwa

Katika harakati za kuboresha sekta ya michezo nchini, Februari 19 mwaka jana, Nape, alitengua uteuzi wa Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Henry Lihaya pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Leonard Thadeo na msaidizi wake, Juliana Yasoda.

Waziri Nape alifikia uamuzi huo wa kumtoa Lihaya kutokana na kukaa kwenye wadhifa huo kwa muda mrefu, bila kuonekana kuwa na mabadiliko ya kimaendeleo katika sekta ya michezo na hivyo nafasi yake kuchukuliwa na Mohammed Kiganja.

Kitendo cha kuondolewa Lihaya, kiliwafurahisha wengi hasa baada ya kuteuliwa Kiganja, ambaye anaonekana kufiti kwa asilimia 100 katika baraza hilo kutokana na utendaji wake wa kazi.

Umitashumta na Umisseta

Juni 13 mwaka jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene, alitangaza kusitisha mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi na Sekondari nchini (Umitashumta na Umisseta), ambayo ilipangwa kufanyika kitaifa jijini Mwanza kuanzia Juni 13 hadi Julai 5, mwaka jana.

Sababu ya kufanya hivyo, ilikuwa kupisha zoezi la kumalizia utengenezaji wa madawati ili kutimiza agizo la Rais Magufuli la kuondoa upungufu wa madawati kwa shule za msingi na sekondari nchini.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Nape alitangaza kuyarejesha mashindano hayo huku akizitaka taasisi zinazohusika na suala hilo kuendelea na mipango ya kimaendeleo, lengo likiwa ni kuibua vipaji vya michezo shuleni.

Mfumo wa ukodishwaji na hisa

Klabu za Simba na Yanga nazo zilijikuta katika mgogoro na Serikali, baada ya kutaka kuingia kwenye mfumo wa uendeshaji na uwekezaji wa klabu zao.

Sakata hilo lilianza baada ya klabu hizo kuamua kutoka kwenye umiliki wa timu wa wanachama kuelekea kwenye umiliki wa hisa na ukodishwaji.

Katika suala hilo, Mwenyekiti wa Yanga, alitaka kuikodisha timu hiyo kwa miaka 10, akiimiliki nembo ya timu ya Yanga, wakati upande wa Simba mfanyabiashara, Mohamed Dewji ‘Mo’, akitaka kuchukua hisa asilimia 51 ya kumiliki klabu hiyo.

Wanachama wa klabu hizo walibariki mabadiliko hayo ya mfumo wa uendeshaji na Yanga ikiwa tayari imeingia mkataba wa miaka 10 wa ukodishwaji na Kampuni ya Yanga Yetu Limited, Septemba mwaka jana, Simba ikiwa katika hatua ya mwisho kumkabidhi klabu hiyo Mo kwa umiliki wa hisa za asilimia 51.

Serikali kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), Mohamed Kiganja, ilitoa uamuzi wa kusimamisha michakato hiyo hadi timu hizo zitakapofanya mabadiliko ya katiba zao kupitia Sheria ya Baraza hilo na Kanuni za Msajili namba 442 Kanuni 11 kifungu kidogo cha (1-9).

Suala hilo lilionekana kuungwa mkono pia na waziri, huku akiwasisitiza Simba na Yanga kuhakikisha wanafuata sheria na kanuni za kungia kwenye mfumo wa kampuni.

Kufungwa Uwanja wa Taifa

Ilizoeleka mara nyingi timu za Simba na Yanga zinapofanya uharibifu katika Uwanja wa Taifa, hupigwa faini pekee, lakini mwaka jana chini ya Waziri Nape hali ilikuwa tofauti baada ya kuzuiwa kuutumia na hivyo kulazimika kuhamia dimba la Uhuru.

Mbali na kuzuiwa kuutumia Uwanja wa Taifa, lakini pia fedha za mapato yao milangoni nazo zilizuiliwa kwa lengo la kufidia gharama za uharibifu uliofanyika na mashabiki wa timu hizo.

Hatua hiyo iliamuliwa baada ya kufanyika kwa uharibifu wa miundombinu ya uwanja huo katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kati ya timu hizo Oktoba mosi mwaka jana na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Baada ya kufanyika kwa ukarabati na timu hizo kuomba radhi, Nape aliamuru waruhusiwe kuutumia lakini wakipewa masharti.

Mkono wa TRA waigusa TFF

Ni zaidi ya miaka 10 iliyopita, Shirikisho la Soka nchini (TFF), limekuwa na deni kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wilaya ya Ilala, lakini katika uongozi wa Nape shirikisho hilo lilionja joto ya jiwe, baada ya kufungiwa akaunti pamoja na ofisi zilizopo eneo la Karume.

TRA iliifungia TFF baada ya kuidai kiasi Sh bilioni1.6 ikiwa ni kodi iliyotokana na makato ya mshahara wa makocha wa kigeni wa timu za taifa katika kipindi cha mwaka 2010-2013, Jan Poulsen, Kim Poulsen na Jacob Michelson.

Pia Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye mchezo wa timu ya Taifa (Taifa Stars) dhidi ya Brazil uliofanyika mwaka 2010, ulichangia deni hilo la kodi kwa asilimia kubwa.

TFF waliweza kupunguza fedha hizo kwa asilimia 50 na kukaa kimya, kabla ya TRA hivi karibuni kuamua kuzifunga ofisi zake na hadi Nape anaondolewa kwenye nafasi ya uwaziri bado hazijafunguliwa.

Kujengwa uwanja mkubwa Dodoma

Miongoni mwa mambo yaliyowafariji wanamichezo wengi nchini ni baada ya Mfalme wa Morocco, Mohammed VI, kuahidi kujenga uwanja wa kisasa wa michezo mkoani Dodoma.

Rais Magufuli alimwomba mfalme huyo alipotembelea Tanzania ambapo aliahidiwa uwanja huo utakaogharimu dola milioni 80 hadi 100, sawa na Sh bilioni 171.216.

Ahadi ambayo Watanzania wanaisubiri kwa hamu kuona utekelezaji  wake na hilo limetokana na mafanikio ya kimataifa yanayopatikana hivi sasa, kupitia wanamichezo wa Tanzania na Waziri Nape kuwasapoti kwa hali na mali.

Tiketi za kielektroniki

Baada ya muda mrefu kuwa na matukio ya ‘upigaji’ fedha katika Uwanja wa Taifa, Nape alifanikiwa kuzuia jambo hilo baada ya kutengenezwa mfumo wa kutumia tiketi za kielektroniki jambo ambalo limeweka historia kubwa katika soka la Tanzania.

Hamasa michezoni

Moja ya vitu vitakavyowakumbusha wadau wengi wa michezo ni hamasa zake alizotoa kwa wanamichezo hasa wanapokuwa na dhamana ya Taifa.

Inakumbukwa Nape ndiye aliyekuwa akihamasisha Watanzania wampigie kura Mbwana Samatta katika kuwania tuzo ya uchezaji bora wa mwaka 2015, lakini pia amekuwa akitoa sapoti kubwa juu ya kuzichangia timu za taifa, Serengeti Boys na ile ya wanawake, Twiga Stars.

Mbali na soka, Nape ametoa pia sapoti kwa washiriki wa Olimpiki mwaka jana na Alphonce Simbu, kuweka rekodi baada ya kushika nafasi ya tano kwenye mbio za marathon za kilomita 42, Agosti 21 mwaka huo huo mjini Rio de Janeiro, Brazil huku akitoa sapoti kwenye vyama vingine ikiwemo kuogelea, netiboli na riadha.

Kauli za wadau

Wakizungumza na SPOTIKIKI wadau mbalimbali wa michezo, wanasema hawataacha kumkumbuka Nape kutokana na mengi mazuri aliyoyafanya katika sekta ya michezo, lakini kubwa kusimamia misingi imara ya utendaji kazi wake, pia wapo tayari kufanya kazi na yeyote aliyepangwa katika wizara hiyo.

Selestine Mwesigwa ni Katibu Mkuu wa TFF, anasema: “Kwanza nimpongeze Mwakyembe kwa kupewa sekta nyingine yenye changamoto nyingi na tunamwahidi kushirikiana naye, huku tukiamini atatufikisha hatua nyingine mbele kutoka pale alipoachia aliyemtangulia kwani Nape alijijengea utaratibu wa kukutana na viongozi husika kila Jumanne kwa lengo la kubadilishana mawazo katika kuhakikisha tunakuwa na maendeleo.”

Naye Katibu wa Chama cha Ngumi za Kulipwa nchini (PST), Antony Ruta, alisema wamepokea vema mabadiliko hayo, ingawa watamkumbuka Nape kutokana na kuweza kufanya kazi kwa kuweka weledi mbele kuliko mapenzi.

“Mwakyembe atatusaidia sana katika masuala ya sheria kwa kuwa ngumi mara nyingi zimekuwa zikikumbwa na migogoro, lakini ukweli atakayekwambia anamsahau Nape atakuwa anakudanganya kwa jinsi alivyofanya kazi katika sekta yake, huku akiwa si mwoga wa kumwajibisha yeyote anayekwenda kinyume, ndio maana katika uongozi wake michezo imekuwa na mafanikio makubwa,” anasema Ruta.

Naye Makamu Katibu Mkuu wa Chama cha Mieleka Tanzania (Awata) Eliakim Melkizedeki, anasema: “Nape alikuwa mwanamichezo na sehemu sahihi aliyokuwepo si mara moja, alionekana viwanjani na katika shughuli mbalimbali za kimichezo, lakini kwa kuwa hatupo naye kwenye nafasi hiyo hatuna budi kufanya kazi na mtu aliyekuwepo, kwani anaweza kutufikisha pale tunapopataka Watanzania,” anasema Melkizedeki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles