29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

MATOKEO VIASHIRIA VYA UKIMWI HADHARANI

Na Veronica Kazimoto-Bukoba

IMEELEZWA kuwa asilimia 97 ya Watanzania wanaoishi katika kaya zilizochaguliwa kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi katika mikoa 11 ambayo imeshafikiwa hadi sasa,  wameshiriki kikamilifu katika utafiti huo unaoendelea kufanyika nchini.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dk. Albina Chuwa, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa utafiti huo kwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Wambura Sabora, alipofanya ziara mkoani humo kuangalia jinsi zoezi la utafiti huo linavyoendelea.

“Ninayo furaha kukutaarifu kwamba,  mpaka sasa utafiti huu umeshafanyika katika mikoa 11 ya Tanzania Bara pamoja  na visiwa vyote vya Zanzibar yaani Pemba na Unguja.

“Jambo la kufurahisha zaidi ni mwitikio wa wananchi ambao ni asilimia 97 ya wanaoishi katika kaya zilizochaguliwa kwa ajili ya utafiti kukubali kushiriki,” alisema Dk. Chuwa.

Mikoa ambayo imekamilisha utafiti huo ni pamoja na Singida, Dodoma, Manyara, Iringa, Njombe na Ruvuma. Mikoa mingine ni Mbeya, Songwe, Katavi, Tabora na Kigoma.

Kwa upande wake Sabora alisema, zoezi la utafiti huo mkoani humo linaendelea vizuri na mpaka sasa hakuna tatizo lolote lililoripotiwa ofisini kwake.

“Nami nichukue fursa hii kukueleza kwamba zoezi hili linaendelea vizuri hapa mkoani Kagera na mpaka sasa hakuna shida yoyote iliyojitokeza.

“Aidha, maeneo ya Kerwa, Missenyi na Wilaya ya Bukoba tayari yamekamilisha utafiti huu”, alisema Sabora.

Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Chonyonyo Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera aliyehojiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa kuhusu jinsi alivyoshiriki kwenye utafiti huo, alisema amefurahishwa na utafiti huo.

“Nimefurahishwa na utafiti huu kwa kuwa sikutarajia kupima vipimo vya magonjwa ya homa ya ini, kaswende pamoja na UKIMWI kwa wakati mmoja nikiwa nyumbani kwangu,” alisema mkazi huyo

Utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania unaendeshwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya kwa Tanzania Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS), Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC).

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,579FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles