26 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Matokeo mabaya darasa la  saba yawaliza madiwani

Diwani wa Kata ya Musanja katika Halmashauri ya Musoma Vijijini, Elias Ndaro, akichangia hoja kuhusu matokeo mabaya ya mtihani wa darasa la saba katika halmashauri hiyo ambayo ilishika nafasi ya mwisho kwa Mkoa wa Mara katika matokeo ya mwaka huu.

Na SHOMARI BINDA-MUSOMA

HALI mbaya ya ufaulu wa mitihani ya  taifa ya darasa la saba mwaka huu katika Halmashauri ya Musoma Vijijini mkoani Mara, imewashtua madiwani ambao wametaka kuwapo baraza litakalokuwa na ajenda moja ya kujadili ufaulu mbovu.

Katika matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Halmashauri ya Musoma Vijijini ilishika nafasi ya mwisho kwa Mkoa wa Mara, jambo ambalo limewasikitisha madiwani hao.

Katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika kijijini Chumwi, madiwani hao walisema hawawezi kuendelea kukaa kimya na matokeo mabaya ya mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne kwa kuwa watu wa mwisho.

Diwani wa Kata ya Musanja, Elias Ndaro, alisema huu ni mwaka wa pili mfulululizo Halmashauri ya Musoma Vijijini inakamata nafasi ya mwisho kwenye matokeo ya mitihani na kuwafanya vijana wengi kubaki mitaani bila kuendelea na elimu hali ambayo ni hatari na inapaswa kutafutiwa ufumbuzi.

Alisema jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika ikiwa ni pamoja na kutoa motisha kwa walimu lakini bado hali ya ufaulu imekuwa mbaya hivyo kudai ni muhimu pia kukutana na walimu na kuona kikwazo na changamoto iko wapi.

“Matokeo kwenye halmashauri yetu ni mabaya na kupitia baraza hili tutoke na azimio la kufanya baraza maalumu la kujadili suala hili  kuweza kuwasaidia watoto wetu waweze kufaulu kwenye mitihani yao na kuendelea na elimu.

“Kila diwani aguswe na jambo hili na tufanye uhamasishaji wa uchangiaji wa miundombinu ya elimu kwenye kata zetu lakini tukiendelea kukaa kimya na jambo hili la elimu tutaendelea kuwa wa mwisho kwenye kila jambo,” alisema Ndaro.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma Vijijini, Ibrahim Buluya, alisema kuna kila sababu ya kukutana kwenye baraza maalumu kujadili jambo la elimu kwa kuwa ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo.

Alisema watafanya mawasiliano na mkurugenzi wa halmashauri kukutana mapema na kujadili matokeo mabaya na kupata ufumbuzi wake  kuweza kuepuka matokeo mabaya katika siku zijazo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles