26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 3, 2024

Contact us: [email protected]

MATOKEO KIDATO CHA NNE: SHULE SABA ZAIFUTA MACHOZI SERIKALI

 

NA Waandishi Wetu-DAR ES SALAAM

HALI ya shule kongwe za Serikali nchini inazidi kuwa mbaya, baada ya matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba mwaka jana kuonesha kuwa katika shule bora zenye zaidi ya watahiniwa 40 za Serikali ni saba pekee zilizoingia katika 100 bora.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa katika tovuti ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Shule ya kwanza ya Serikali ni Kibaha Sekondari ya Pwani iliyoshika nafasi ya 16 kati ya shule 3, 280 zenye watahiniwa zaidi ya 40 ambazo watahiniwa wake walifanya mtihani huo.

Taarifa hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN),  kwa kupanga shule kuanzia ya kwanza na kuzigawa kwa rangi huku zile zenye ufaulu mzuri kuwa kwenye rangi ya kijani, ufaulu wa kati rangi ya njano na ufaulu mbaya rangi nyekundu.

Taarifa hiyo imeonesha kuwa shule nyingine za Serikali kwenye 100 bora na namba ilizoshika kwenye mabano ni Mzumbe ya Morogoro (27), Kilakala ya Morogoro (28), Shule ya Wasichana Kibosho ya Kilimanjaro (36),Shule ya Wavulana Tabora (41) na Ilboro ya Arusha (42).

Baadhi ya shule kongwe za Serikali ambazo hazijaingia katika kundi hilo ni pamoja na  shule ya wasichana Tabora Girls (113) Msalato ya Dodoma (129) na Azania ya Dar es Salaam (451).

Wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya bajeti ya mwaka 2016/17, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema wizara yake imeandaa mpango wa ukarabati wa shule kongwe za sekondari nchini na kwamba katika awamu ya kwanza, shule 33 zitakarabatiwa.

Alizitaja shule zilizo kwenye mpango wa kukarabatiwa kuwa ni pamoja na Ihungo, Ilboru, Kilakala, Mwenge, Msalato, Mzumbe, Nganza, Pugu, Same, Tabora Boys na Tabora Girls.

Nyingine ni Azania, Jangwani, Kantalamba, Mpwapwa, Tosamaganga, Malangali, Milambo, Nangwa, Kibiti, Minaki, Ifakara, Songea Boys, Ndanda, Kigoma, Kibaha na shule za ufundi za Bwiru Boys, Ifunda, Iyunga, Moshi, Mtwara, Musoma na Tanga.

“Mazingira ya kufundishia na kujifunzia yana mchango mkubwa katika kuinua ubora wa elimu katika ngazi zote,” alisema Profesa Ndalichako.

Moto kuwaka shule za mwisho Dar

Katika hatua nyingine, Ofisa  Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Nsunza, jana aliliambia gazeti hili kwamba  shule sita zilizoshika mkia katika mkoa wake zilikuwa na viashiria vya kufanya vibaya, ambapo walimu pamoja na wakurugenzi wa halmashauri husika walipewa hadhari baada ya matokeo ya mtihani wa kujipima wa kanda.

 “Hizi shule zilionyesha viashiria vibaya kwenye mtihani wa kujipima wa Moko ambapo wakuu waliandikiwa barua na wakurugenzi na kuitwa ambapo walipewa onyo na mikakati ya kuzikomboa shule hizo lakini hata hivyo jitihada hizo zimekwama,” alisema Janeth.

Janeth aliongeza ofisi yake tayari imechukua hatua ya kuwahoji walimu wakuu wa shule zilizofanya vibaya na baadaye watazungumzia hatua zilizochukuliwa.

“Ni mapema mno kuzungumzia hatua tulizochukua kwa wakuu wa shule na walimu katika shule zilizofanya vibaya ila tunaendelea kuwahoji na kadri siku zinavyoenda tutatoa msimamo wetu kama mkoa nini kifanyike na hatua zilizochukuliwa,” alisema Janeth.

Alisema shule hizo zilizofanya vibaya ni kati ya shule za kata zilizojengwa na wananchi ambapo Manispaa ya Kinondoni zipo 49, Ilala 41 na Temeke 38.

Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa juzi, wanafunzi waliopata ufaulu mzuri (daraja la I-III) ambao ndiyo wenye uwezekano mkubwa wa kwenda kidato cha tano ni 96,018 sawa na asilimia 27.60, kati yao waliopata daraja la  kwanza ni 9,458 sawa na asilimia 2.72, wavulana wakiwa 5,723 sawa na asilimia 3.37 na wasichana 3,735 sawa na asilimia 2.1.

Waliopata daraja la pili ni 32,391 sawa na asilimia 9.31 kati yao wavulana ni 19,959 sawa na asilimia 11.75 na wasichana 12,432 sawa na asilim8ia 6.98.

Watahiniwa waliopata daraja la tatu ni 54,169 sawa na asilimia 15.57 wavulana wakiwa 31,054 sawa na asilimia 18.28 na wasichana 23,115 sawa na asilimia 12.98.

Matokeo yanaonyesha pia kuwa, watahiniwa walipata daraja la nne ni 148,744 sawa na asilimia 42.75 wavulana wakiwa 68,130 sawa na asilimia 40.1 na wasichana 80,614 sawa na asilimia 45.28.

Waliofeli mtihani huo ni watahiniwa 103,164 sawa na asilimia 29.65 wavulana wakiwa 45,024 sawa na asilimia 26.5 na wasichana wakiwa 58,140 sawa na asilimia 32.66.

Katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2015, watahiniwa wa shule waliopata daraja la kwanza walikuwa  5,973 sawa na asilimia 2.77 tu, hivyo ikilinganishwa na mwaka 2016, ufaulu kwenye eneo hili umeshuka.

Kwa daraja la pili mwaka 2015 walikuwa  19,791 (asilimia 9.01), daraja la tatu 27,749 (asilimia 13,56) na daraja la tatu la juu ni watahiniwa 53,513 (asilimia 25,34).

Waliopata daraja la nne ni watahiniwa 71.358 sawa na asilimia 67.91 na waliofeli ni 47,812 sawa na asilimia 32.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles