25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Matiko aeleza mikakati ya 2020

DAMIAN MASYENENE – SHINYANGA

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Serengeti, Esther Matiko, amesisitiza kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, wataipigia debe sera ya Serikali ya majimbo ambayo itawapa mamlaka wananchi wa maeneo husika kuchagua miradi na uwekezaji wanaoutaka.

Matiko ambaye pia ni Mbunge wa Tarime Mjini mkoani Mara, alionyesha kutoridhishwa na baadhi ya miradi inayoendelea iliyojikita zaidi kwenye maendeleo ya vitu, badala ya watu.

Aliyasema hayo juzi wakati wa mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari na viongozi wa chama hicho mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga tangu achaguliwe mapema Desemba, mwaka jana.

“Katika sera mbadala, tunaamini na tutasisitiza Serikali za majimbo pale tutakapopata madaraka, tutafanya uamuzi kupitia mabunge madogo ya majimbo yanayowapa wananchi uwezo wa kuamua nini wafanye kulingana na rasilimali zao.

“Kinachoendelea sasa ni uwekezaji katika maendeleo ya vitu badala ya watu, wananchi wanalazimishwa kuikubali kwa nguvu wakati si vipaumbele vyao,” alisema.

Alisema Chadema Kanda ya Serengeti kitautumia mwaka uliopita kutafakari na kujielekeza kuangalia mwelekeo wao katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kujikita katika nyanja muhimu zinazowagusa wananchi ili wakamate dola, kushinda majimbo yote 24 na kata zaidi ya 200.

Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 24, mwaka jana, alisema kilichofanyika ni dhuluma.

“Badala ya Serikali kujipima na kupata mwelekeo, ilitumia mabavu kuwaaminisha wananchi kuwa inakubalika.

“Chadema tumemuomba Rais Dk. John Magufuli kutengua matokeo na uchaguzi huo ujumuishwe na ule mkuu wa mwaka 2020.

“Kama watendaji wa Serikali na viongozi wanaamini wanayoyafanya ni mazuri, walipaswa kujitathmini kupitia huo uchaguzi, hawakupaswa kuuvuruga na kuogopa, wangeacha wapate picha halisi kutoka kwa wananchi.

“Wananchi wanapaswa kupata haki ya kuchagua viongozi wanaowataka, Chadema kwenye mkutano mkuu tuliazimia na tukamuomba rais aufute uchaguzi huo, awawajibishe wote waliohusika kuuvuruga, auunganishe na uchaguzi mkuu wananchi wapate haki waliyodhulumiwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles