Nora Damian
Shamrashamra za Wiki ya Mwananchi zimezidi kupamba moto katika maeneo mbalimbali ya nchi ambako kumeshuhudiwa wanachama wa Klabu ya Yanga wakijitokeza kufanya shughuli za kijamii na kutoa misaada ya kibinadamu.
Leo Jumamosi Agosti 3, Umoja wa Matawi ya Yanga Tabata umejitokeza kufanya usafi katika Zahanati za Tabata A na Segerea sambamba na kutoa vifaa vya usafi katika zahanati hizo na mashuka katika Kituo cha watoto yatima cha Malaika kilichopo Kimanga.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa Umoja wa Matawi ya Yanga Tabata, Adeltus Kazinduki, amesema wameguswa kufanya usafi kuboresha mazingira katika hospitali hizo.
“Wiki ya Mwananchi inamlenga kila raia ambaye yuko katika nchi hii, ndiyo maana kwa umoja wetu tuliamua tuje kufanya usafi hospitalini tuwajali watu wenye mahitaji,” amesema Kazinduki.
Kilele cha Wiki ya Mwananchi kitafikia tamati kesho katika Uwanja wa Taifa ambako Yanga itaivaa Kariobangi Sharks ya Kenya.