27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MATATIZO KIBITI YATISHIA UWEKEZAJI MKOANI PWANI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama moja kati ya matrekta aina URSUS yanayounganishwa kwenye karakana ya TAMCO mjini Kibaha, ni mradi wa ushirikiano na kampuni ya Poland.

Na Mwandishi Wetu,

MATATIZO ya mauaji yanayofanywa na watu wasiojulikana na kwa sababu zisizoelezwa na wahusika pamoja na Serikali, zimeanza kuathiri uwekezaji mkubwa uliokuwa umeshamiri katika Mkoa wa Pwani.

Rais John Magufuli ameweka wazi kwa wakazi wa Mkoa wa Pawani kuwa matatizo hayo ya ulinzi yana nafasi kubwa ya kupunguza uwekezaji ambao ulionekana kushamiri mkoani humo, kwani si rahisi watu kuwekeza mahali ambapo pana mauaji na kukosa usalama.

Maeneo ya  wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji kumezuka hali ya sintofahamu kutokana  kufanyika mauaji ya kinyama yasiyoelezeka na hivyo kufanya juhudi za Serikali kuendelea na ajenda ya uwekezaji wa viwanda na lengo la kufanya uchumi wa viwanda kuwa gumu  wilayani Kibiti ambapo ni kitovu cha mauaji hayo.

Akizungumzia kwa mara ya kwanza kuhusu matatizo hayo, Rais Dk. Magufuli wakati wa ziara yake ya siku tatu mkoani Pwani, alisema akiwa Mji wa Kibaha Makao Makao ya Mkoa huo kuwa wasishangae kama  viwanda vinaweza visijengwe kwenye maeneo  hafifu kutokana na rabsha hizo na wao wajilaumu wenyewe kwani amani ndio ngao  kubwa ya uwekezaji popote pale duniani.

Aliwataka wenyeji watafakari hali iliyopo na kutoa taarifa kwa Serikali juu ya watu wanaoendesha mauaji hayo ili dola iweze kutekeleza vilivyo majukumu yake ya ulinzi na usalama kwa kuwaondoa wale wote waovu.

“Mwito ninautoa kwa watu kuwafichua watendaji maovu hayo yasiyo na maana, kwani yanafanyika kwa kificho na hivyo ni wazi wahalifu wako kwenye jamii husika na hivyo ni jukumu la watu kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama ili washughilikiwe vilivyo,” alisema.

Akisoma taarifa ya mkoa, Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Evaristi Ndikilo, alisema hali ya ujenzi wa viwanada mkoani humo ni ya kuridhisha kwani kuna viwanda 371 ambapo 89 ni vya kati na vingine ni vidogovidogo.

Alisema  wilaya za Mkuranga, Rufiji na Kibiti ziko nyuma kwenye suala la uchumi wa viwanda kutokana na kukosekana umeme wa uhakika na miundombinu duni ya barabara.

Rais alisema fedha za kupunguza madhila ya miundombinu zimeshatumwa katika wilaya hizo  kutokana na Mfuko wa barabara, lakini alionya kuwa  wananchi wa huko wanahitaji kufanya zaidi katika masuala ya ulinzi na usalama.

“Ushiriki wa wananchi kutoa taarifa ni muhimu ili wale wote wakorofi wakamatwe na kutengwa na raia wema,” alisema Rais.

Alisema ni vigumu sana kwa wawekezaji kuwekeza sehemu yenye tatizo la usalama kwani hawako tayari kuweka mali zao kwenye rehani ya wakorofi na wapinga maendeleo.

Wakati rais akiongea hayo, zaidi ya watu 39 wameshauawa wilayani Kibiti na Mkuranga na wahalifu wasiojulikana na hivyo kuleta taharuki kwa watu waishio huko na kufanya shughuli za uchumi kuwa ngumu kwani watu wamejawa hofu na sintofahamu nyingi.

“Suluhisho liko mikononi mwenu wananchi kuchagua kukumbatia uhalifu au kuachana nao kwa kuwafichua wahalifu,” alisema Rais.

Wauaji wakaidi

Cha ajabu siku tatu baada ya matamshi ya rais, watu watatu wakauawa katika maeneo hayo hayo, ni dalili za wazi kukaidi  amani aliyotegemea Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania.

Mauaji hayo yamekuwa kizungumkuti kwani hakuna aliyejitokeza mbele na kusema kwanini yanafanyika ili mamlaka iweze kutafakari la kufanya ingawa dalili za awali zilikuwa ni kuua viongozi wa chama tawala halafu zikageuka na kutishia dola kwa kuua polisi wanane kwa mpigo.

Ujenzi wa Stiegler Gorge

Serikali imesema  ili kushughulikia uhaba wa umeme na mwendelezo wa kuvuna rasilimali zake kuwa ule ujenzi Katika Maporomoko ya Stiegler wilayani Rufiji, utafanyika hapo ili mpango mzima wa uchumi wa viwanda uwe na uhakika wa umeme rahisi.

Mradi huo wa miaka mingi  kuanzia miaka ya 1980, umeonekana kukumbwa mara nyingi na matatizo ya fedha na pingamizi kutoka taasisi za kimataifa, zikidai kufanya uharibifu mkubwa wa mazingira na hivyo kuleta maendeleo hasi katika uchumi.

Serikali imeamua kushughulikia tatizo hilo kwa ujenzi wa awamu wa bwawa la umeme na kutokana na  Rais Magufuli kusema kuwa wataalamu toka Ethiopia  ndio watafanya tathmini ya mwisho kabla ya ujenzi katika maeneo manane yaliyoainishwa kuwa yanafaa kuzalisha umeme wa maji katika Bonde la Rufiji.

Tafiti yakinifu za awali zinaonesha kuwa bwawa la mita 130 linaweza kujengwa Stiegler Gorge katika awamu nne ambazo zitakuwa zinafuatana kwa megawati 300, halafu  MW600, 300 na mwishowe MW 900.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles