Na Christian Bwaya,
MTOTO wa jirani yangu yuko likizo. Imebidi arudi nyumbani kwa sababu shule ya bweni anakosoma imefungwa hivi majuzi. Ingawa inatarajiwa angepumzika wakati huu wa likizo, bado mtoto ametengenezewa ratiba nyingine kumwezesha kuendelea na masomo ya ziada ‘twisheni’ kwenye shule ya jirani. Mpango huu maalumu umemwekea mtoto wa jirani yangu mkazo zaidi kwenye maeneo kama mwandiko, hesabu za kuzidisha na kugawanya pamoja na lugha.
Ratiba hii ya likizo ni ngumu kidogo kwa mtoto. Kwanza, mtoto analazimika kuondoka nyumbani asubuhi na kurudi saa nane mchana. Hakuna muda wa kupoteza. Lakini pia, mtoto hurudi na kazi nyingi za nyumbani ambazo ni sharti zikamike kabla ya siku inayofuata. Bahati nzuri, walimu wake wanaolipwa fedha za ziada kwa kazi kubwa wanayofanya wanajituma zaidi kuliko inavyokuwa wakati shule zimefunguliwa. Kujituma huko kunatafsirika kwenye wingi wa kazi ambazo mtoto hurudi nazo kila siku.
Jambo hili linafanyika kwa nia njema. Jirani yangu kwa kweli anafanya haya yote kwa lengo la kumwandalia mtoto maisha mazuri. Kama mzazi msomi, anaelewa na sisi tunakubaliana naye kuwa elimu ni ufunguo wa maisha. Ujinga, kwa upande mwingine, ni adui wa maendeleo.
Maendeleo haya ya ‘kisasa’ yametufanya wazazi tuwe na matarajio makubwa kwa watoto kuliko ilivyokuwa zamani. Tumewatengenezea watoto shinikizo kubwa la kufanikiwa. Ili kukidhi matarajio hayo, tumeamini mtoto lazima asome na kufaulu. Tunapima mafanikio ya mtu kwa kigezo cha ufaulu wa mitihani.
Hakuna tatizo la kuwa na matarajio makubwa. Kufikiri mambo makubwa ni kichocheo cha kujituma na kujibidiisha. Anachokifanya jirani yangu kimsingi ni kumtengenezea mtoto mazingira ya kuelimika ili hatimaye awe na maisha mazuri. Badala ya mtoto kushinda nyumbani akiangalia televisheni, kwenda shule kunamsaidia. Kadhalika pale ambapo mtoto anapokuwa na shida ya kitaaluma, inakuwa rahisi kupata msaada wakati huu wa likizo.
Hata hivyo, matarajio hayo lazima yazingatie hali halisi. Upo uwezekano wa matarajio haya kuleta changamoto zisizotarajiwa. Kwa mfano, kwa sababu ya matarajio makubwa, wazazi hawako tayari kuona mtoto ‘anacheza cheza’ nyumbani. Mtoto mwenye miaka mitatu, kwa mfano, anaanza kutarajiwa ajue kusoma, kuandika na kuhesabu. Walimu nao wanakuwa na kazi ya kuhakikisha wanafikia matarajio hayo ya wazazi. Walimu hawa wa elimu ya awali, mathalani, wanajenga imani kuwa shughuli ya maana waliyonayo kama walimu bora ni kuhakikisha mtoto mdogo ‘anaivishwa kitaaluma.’
Wazazi hawatarajii mtoto acheze, aimbe, akosee, afeli, ajifunze. Muhimu kwao ni mtoto ‘kushika masomo’, ikiwamo kujua Kiingereza. Hiki ndicho kinachomkabili jirani yangu anayempeleka mwanawe wa darasa la kwanza ‘twisheni.’ Haamini kuwa mtoto anaweza kufanya vizuri bila ‘nguvu za ziada.’
Matarajio haya makubwa yana athari kadhaa kwa watoto. Kwanza, watoto wanajikuta wakitumia muda mwingi kwenye masuala ya kitaaluma ambayo wakati mwingine yanazidi umri wao. Eneo la uelewa wa mambo linawekewa msisitizo mkubwa kuliko maeneo mengine ya muhimu kwenye kimakuzi.
Pili, ukubwa wa matarajio haya unatufanya wazazi tusitambue juhudi kubwa zinazofanywa na watoto. Mtoto wa jirani yangu anafanya vizuri lakini kwa maoni ya mzazi, bado. Hali kama hii inaweza kumkatisha tamaa mtoto ambaye kimsingi analazimika kuwa mtu mzima kabla ya wakati wake.
Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.