Asha Bani
Kundi la matapeli linadaiwa kutumia jina la Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi nchini (NEC) Dk. Athumani Kihamia kwa lengo la kutapeli watu ili kujipatia fedha.
Akizungumza na Mtanzania kwa njia ya simu leo Jumamosi Juni 15, Dk. Kihamia amesema kuna watu wamefungua akaunti feki ya mtandao wa kujamii wa facebook na kuwatapeli watu kwa kuwatumia ujumbe wa maneno (Messenger), ambapo ametoa tahadhari kwa wananchi kua makini na utapeli huo unaoendelea.
“Kuna baadhi ya watu wamefungua akaunti kwa jina langu na kulitumia kwa kujipatia fedha kwa njia hiyo ya utapeli huku wakijua ni kosa kisheria, baadhi ya jumbe wanazotuma ni pamoja na kwamba Dk. Kihamia anauwezo wa kuwatafutia kazi katika mbuga ya Hifadhi ya Serengeti,”
“Yaani tayari kuna watu wameliwa fedha na hao matapeli hao kupitia sehemu ya ujumbe unaosema sema hivi “angalia kama kuna mtu amemaliza chuo na hajapata kazi uniambie maana kuna kazi shirika la Marekani la Thomson Zoology kule Serengeti national park na wanahitajika watu wawili wenye diploma au degree kwa ajili ya kazi ya reservations na mshahara milioni moja na laki nane kama kuna mtu aniambie mapema nimpe namba ya huyo mzungu ahsante,” amesema.
Dk. Kihamia amesema aliishawahi kukanusha taarifa hiyo kupitia mitandao ya kijamii lakini anaona hali inazidi kuwa mbaya hivyo amewataka wananchi kupuuza ujumbe huo.