21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, August 16, 2022

Matamshi bosi wa wafanyakazi dhidi ya Ruto yalivyopingwa

ISIJI DOMINIC

NCHINI Kenya wikiendi haiwezi kupita bila wanasiasa kutumia majukwaa iwe ni ya mazishi, sehemu za kuabudu au shughuli za kitaifa kupiga siasa zinazohusu uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2022, licha ya Rais Uhuru Kenyatta kuwaonya.

Aidha maridhiano kati ya Rais Uhuru na kinara wa upinzani, Raila Odinga, hutawala zaidi huku baadhi ya wanasiasa wa Jubilee wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto waliopachikwa jina la ‘Tangatanga’ wakimtaka Odinga kuheshimu ‘handshake’ na kuacha kuingilia mambo yanayohusu chama chao.

Kundi lingine ndani ya Jubilee linalotambulika kama ‘Kieleweke’ wakishirikiana na wanachama wa ODM wanaounga mkono ‘handshake’ wanasisitiza agenda nne kuu za Rais Uhuru ikiwemo mapambano dhidi ya ufisadi lazima yaendelezwe.

Ruto ndiye anayeonekana kuwania urais uchaguzi mkuu ujao kutokana na maelezo ya washirika wake, na mpinzani wake japo naye hajaweka wazi nia yake ya kuwania urais kwa mara nyingine tena ni Raila.

Mvutano baina ya wafuasi wa pande hizi mbili yanamuweka Rais Uhuru katika wakati mgumu kutekeleza ahadi zake kwa wananchi lakini (Rais Uhuru), amesisitiza hatayumbishwa kutimiza azma yake ya kuiacha Kenya inayoheshimika na haina chembechembe ya ufisadi.

Katika kukoleza mbio za kuwania urais mwaka 2022, Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli, akiwa katika kaunti ya Lamu mwishoni mwa wiki iliyopita, alimwambia Ruto asahau ndoto za kuwa rais akisisitiza jina lake halitakwepo kwenye karatasi za kupiga kura.

Ni kauli iliyochukuliwa kwa uzito mkubwa na tafsiri ya kila aina na wabunge wanaomuunga mkono Naibu Rais. Kiongozi wa walio wengi bungeni, Aden Duale, alimuonya bosi huyo wa wafanyakazi kuwa muangalifu na matamshi yake ambayo yanaweza kuvuruga amani.

“Lazima atuambie alikuwa anamaanisha nini kwamba Naibu Rais hatakuwa debeni. Kama viongozi kutoka maeneo mbalimbali nchini tunatakiwa kuwa waangalifu na matamshi yetu kwa sababu tunaweza kuligawa taifa kwa misingi ya kikabila wakati ajenda yetu ni kuwaunganisha Wakenya wote,”alisema Duale.

Naye Mbunge wa Lamu Mashariki, Stanley Muthama, alimtaka Atwoli kushughulikia masilahi ya wafanyakazi na kuacha kumuandama Ruto huku akiongeza watu wa Lamu hawatamkaribisha kama nia yake ni kutukana viongozi.

“Hakuna cha maana Atwoli alichokiongea alipokuja katika kaunti yetu. Badala ya kuongea kilichomleta pale akaamua kutukana watu lakini tunamwambia kwamba hatutamuacha, tutamshughulikia,”alisema Muthama.

Kwa upande wake, Mbuge wa Lunga Lunga, Khatib Mwashetani, alimshutumu Atwoli kwa kueneza uongo dhidi ya Ruto kuhusu masuala ya ufisadi.

“Kama unaona mtu ni fisadi na unao ushahidi, basi ipeleke ofisi za Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma. Kama Atwoli ana nia ya kujiunga na siasa, aweke nia yake wazi ili tumshughulikie,”alisema Mwashetani.

Hata hivyo, matamshi ya Atwoli yameungwa mkono na Mbunge wa Alego Usonga, Samuel Atandi, akisema Katibu Mkuu huyo wa COTU ni kiongozi mzoefu ambaye anachokisema yana uzito.

“Yuko sahihi, namuunga mkono. Kwangu mimi yeye ni tunu ya taifa na akiongea lazima asikizwe kwa umakini,” alishauri Atandi akimtaka Naibu Rais kutopuuza alichokisema Atwoli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,814FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles