25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Matajiri nane Afrika waporomoka kama Mo

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

RIPOTI mpya ya Jarida maarufu linalofuatilia watu wenye utajiri mkubwa duniani la Forbes, mbali na kuonyesha ukwasi wa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji maarufu kama Mo umeporomoka kwa Dola za Marekani milioni 300 katika kipindi cha mwaka mmoja, imeonyesha pia matajiri wengine nane wa Afrika nao wamekumbana na hali kama hiyo.

Ripoti hiyo ya mwaka 2020, iliyotolewa juzi imeonyesha kuwa miongoni mwa matajiri waliokumbana na hali hiyo ni tajiri namba moja Afrika, ambaye ni raia wa Nigeria, Aliko Dangote.

Tofauti na ilivyoripotiwa na gazeti dada la hili la MTANZANIA Jumamosi ambalo lilionyesha kimakosa kwamba utajiri wa Dangote umeongezeka, hata hivyo kwa mujibu wa Forbes imebainika kuwa utajiri wake umeshuka hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 10.1 kutoka dola bilioni 10.3 mwaka uliopita.

Taarifa ya Forbes inaeleza kuwa Dangote anakabiliwa na hali hiyo katika wakati ambao pia kuna kushuka kidogo kwa bei ya hisa katika biashara yake ya Sementi ambayo ndiyo  kubwa.

Kwa upande wa Mo, licha ya ukwasi wake kuporomoka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka jana hadi dola bilioni 1.6, kijana huyo anayetambulika kama bilionea mdogo barani Afrika, hata hivyo ripoti hiyo imeonyesha amepanda kutoka nafasi ya 17 aliyokuwa akiishikilia mwaka 2019 hadi kufikia nafasi ya 16 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Forbes, Pamoja na Mo matajiri nane wameshuhudia wakipanda au kushuka kwa angalau Dola za Marekani milioni 700. 

Aidha anayetajwa kuanguka zaidi katika orodha ya mabilionea 20 wa Afrika ni bilionea wa Zimbabwe, Strive Masiyiwa ambaye msingi wa fedha zake ni kwenye mawasiliano.

Utajiri wa Masiyiwa umeshuka hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 1.1 kutoka dola bilioni 2.3  mwaka mmoja uliopita, na hivyo kumfanya kuwa bilionea aliyeanguka zaidi.

Masiyiwa ana miliki hisa nyingi katika kampuni mbili ambazo zinafanya biashara katika soko la hisa la Zimbabwe.

Lakini uamuzi wa mwezi Juni wan chi yake kupiga marufuku fedha zote za kigeni  na kutumia dola ya Zimbabwe tu iliongeza mfumuko wa bei na kusababisha dola iliyoamriwa kutumika kushuka zaidi.

Matokeo yake hali hiyo ikasababisha hisa za Masiyiwa katika kampuni hizo za mawasilino za ‘Econet Wireless Zimbabwe  na kampuni ya Cassava Smartech kuporomoka.

WALIOPANDA

Mbali na hao walioporomoka, Forbes imemtaja aliyepanda zaidi kwa mwaka huu ni bilionea kutoka Misri, Nassef Sawiris, ambaye  kwa mara ya kwanza ameshika nafasi ya pili huku utajiri wake ukikadiriwa kufikia dola bilioni 8  kutoka dola bilioni 6.3 mwaka jana. 

Pamoja na kwamba Sawiris biashara zake kubwa ni kwenye kampuni za ujenzi na kemikali biashara nyingine ya viatu anavyozalisha kwa nembo ya Adidas akiwa na hisa asilimia 5.7nayo imeonekana kumpandisha katika nafasi hiyo.

Bilionea wa pili anayetajwa kupanda zaidi ni raia wa Nigeria, Abdulsamad Rabiu ambaye sasa utajiri wake umefikia dola bilioni 3.1 kutoka dola bilioni  1.6 mwaka jana.

Kupanda huko wa Rabiu kunaelezwa kunatokana na kujikita kwenye biashara ya sementi ambako mwaka jana alielezwa kuingiza mtaji wa Dola za Marekani milioni 600.

Katika nchi 54 za Afrika, ni nchi nane tu ndizo zenye mabilionea ambazo ni: Misri na Afrika Kusini ambazo kila moja ina mabilionea watano, inafuatia Nigeria yenye wanne na Morocco wawili  wakati Algeria, Angola, Tanzania na Zimbabwe zikiwa na bilionea mmoja mmoja.

Miaka tisa iliyopita nchi nne tu za Afrika ndizo zilizokuwa na mabilionea.

Katika ripoti ya mwaka huu ukimwacha Dangote ambaye ameshika nafasi ya kwanza na Sawiris nafasi ya pili nafasi ya tatu imeshikwa na watu wawili Mike Adenuga na Nicky Oppenheimer ambao wote wana miliki dola bilioni 7.7.

Bilionea Johann Rupert ameshika nafasi ya tano ($ bilioni 6.5), Issad Rebrab nafasi ya sita ($ bilioni 4.4), Mohamed Mansour nafasi ya saba ($ bilioni3.3), Abdulsamad Rabiu nafasi ya nane ($ bilioni 3.1), Naguib Sawiris nafasi ya tisa ($ bilioni 3). 

Kwa upande wa wanawake walioingia katika orodha ya matajiri 20 barani Afrika, ni pamoja na binti wa Rais wa zamani wa Angola, Jose Dos Santos, Isabel ambaye ameshika nafasi ya 13 akiwa na ukwasi wa dola bilioni 2.2 na Folorunsho Alakija kutoka Nigeria ambaye ameshika nafasi ya 20 akiwa na dola bilioni moja. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles