25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MASTAA WALIVYOWASHA MOTO TOZO MPYA ZA BASATA

Na CHRISTOPHER MSEKENA


BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata) limeeleza kuwa kampuni itakayompa dili msanii italazimika kulipa tozo kwa baraza hilo, kiasi cha shilingi milioni 5 kwa kutangaza bidhaa zake au shilingi laki 5 kwa kampuni kujitangaza kupitia msanii au sanaa.

Basata wametangaza bei hizo mapema wiki hii, hali iliyoibua mjadala mzito kwenye tasnia ya burudani, ikiwagusa mastaa na wadau muhimu katika sekta hiyo.

Mastaa mbalimbali wamesema uamuzi huo wa Basata una lengo la kuwaumiza kwani hali yao kama wasanii siyo nzuri na kwamba hata mafanikio kidogo waliyonayo ni kwa juhudi zao wenyewe.

Wameeleza kuwa, sanaa ni ajira na kwamba vijana wengi wanatumia vipaji vyao kuendesha maisha, hivyo Basata wanapaswa kujadiliana nao upya ili kupata mawazo mbadala ya kuweka sawa sakata hili.

Msanii mmoja nchini, ambaye alikataa kutajwa jina lake gazetini alisema: “Basata hawapaswi kuwa mwiba kwenye sanaa, wanapaswa kuwa daraja la kutuvusha kutoka katika hali ya chini na kutuweka juu kiuchumi kwa kuseti ajenda zitakazokaribisha kampuni nyingi kuwekeza kwetu wasanii.”

Mbali na huyo, wasanii kadhaa wamezungumzia ishu hiyo na hapa chini ni maoni yao;

STEVE NYERERE

Huyu ni Mwenyekiti wa Uzalendo Kwanza, amekuwa mstari wa mbele katika masuala mbalimbali yanayowahusu wasanii. Steve ameliambia Swaggaz kuwa huu ndiyo muda wa wasanii kuungana na kupinga bei hizo ili Basata na wadau wengine muhimu wakae chini kujadili upya.

“Wasanii wana matatizo mengi, tuna hali mbaya na bado tunatengenezewa muhtasari wa kunyonywa tu. Tusiposimama kuwa wamoja siyo muziki siyo filamu siyo sarakasi wote tuungane tutoe sauti moja tuseme Basata wametukosea, tutarudi kukaa chini, tatizo letu tumegawanyika tuna matabaka ambayo hayana msingi.

“Milioni 5 ni nyingi sana kwa msanii ambaye amejiajiri mwenyewe. Basata watuite, sisi ni watoto wao, tukae pamoja, tuzungumze kwa sababu ukweli ni kwamba tuna majina makubwa ila hatuna hela nyingi kiivyo,” anasema.

WITNES KIBONGE MWEPESI

Yupo katika Kamati ya Matukio na Burudani ya Chama Cha Muziki wa Kizazi Kipya (TUMA), yeye  anasema licha ya wasanii asilimia 75 kutojisajili katika chama,  Basata wanapaswa kuwawezesha ili hizo dili ziwe nyingi.

“Tunaingiza pesa kidogo, hawatusimamii kwa lolote, mifereji tunachimba sisi ili mvua ikinyesha tupate kitu, halafu mwisho wa siku hicho kitu kidogo tunagawana nao wenyewe ambao hawatufanyii kitu chochote,” anasema Witnes.

BILLNAS

Ni rapa makini anayefanya vizuri kwa sasa, yeye anasema Basata ilitakiwa ijadiliane na wasanii kwanza kabla haijatangaza tozo hizo, kwani wasanii na kampuni wanalipa kodi hivyo haina haja ya kampuni kulipa tena Basata fedha hiyo.

“Basata hawajui sisi tunavyofanya kazi, kampuni ikinipa dili mimi basi inalipa kodi TRA, lakini siyo hivyo tu mimi pia nalipa kodi TRA na hilo fungu langu linapigwa panga na lebo inayonisimamia, sasa hapo mi msanii nitapata nini?! bora tusiimbe tu maana hizo kampuni zenyewe zitatukimbia,” anasema Billnenga.

NIKKI WA PILI

“Matangazo yapo ya aina nyingi, kampuni inaweza kumtumia msanii kuweka tangazo lao katika ukurasa wake wa Instragram, wakamlipa kwa posti moja au mbili, sasa ukisema hapo kampuni ilipe Basata milioni 5? Sasa kwani kwa posti moja msanii hulipwa bei gani, kifupi hapo hizo dili zitakufa,” anasema.

BASATA WATOA NENO

Baada ya kukusanya maoni hayo, Swaggaz lilifunga safari hadi Ofisi za Basata zilizopo Ilala jijini Dar es Salaam ambapo lilifanikiwa kuzungumza na Godfrey Mngereza ambaye ni Katibu Mtendaji wa baraza hilo.

Akizungumzia ishu hiyo, Mngereza alisema: “Sheria hii ipo ili wasanii waweze kuthaminika na kuna makampuni makubwa ambayo wanaweza kutoa hela hiyo, hatujapata changamoto yoyote katika hayo makampuni zaidi ya wasanii.

“Kazi ya sanaa ni mali ya msanii na ana uhuru nani aitumie kwa ridhaa yake, hivyo lazima aje ofisini na tuzungumze endapo hilo tangazo ni la kujitolea au lah na kumbuka kampuni lazima itanufaika kwa msanii hata kama msanii atakuwa amejitolea,” anasema Mngereza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles