NA FRANCIS GODWIN
Mashine za kielektroniki (EFD), zimezua kizaa zaa mkoani Iringa baada ya baadhi ya vinyozi na mama lishe wenye migahawa maeneo ya Miyomboni ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuwafungia biashara zao kwa kutokuwa na mashine hizo za kutolea risiti.
Zoezi hilo limefanyika wiki mbili zilizopita katika msako wa biashara zisizo na mashine hiyo ambapo baadhi ya wafanyabiashara waliofungiwa wamelalamikia hatua hiyo kutokana na kipato kidogo wanachopata kupitia biashara hizo.
Mfanyabiashara wa chakula eneo la Miyomboni, Michael Simon amesema TRA ilifunga mgahawa wake kwa zaidi ya wiki mbili kutokana na kuuza chakula bila ya kutoa risiti za EFD ila kwa sasa amelazimika kununua mashine hiyo.
Amesema biashara anayofanya haina tofauti na ile ya mama lishe isipokuwa eneo limewaponza kutokana na bei ya pango katika maeneo hayo.
Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Ramson Tulianje amesema vinyozi na wafanyabiashara ambao wanapaswa kuwa na mashine ni wale ambao kwa siku wanauza kati ya Sh 40,000 na kuendelea bila kujali anafanya shughuli gani.
“Eneo hilo la Miyomboni bei ya kupanga vyumba ni Sh 400,000 kwa mwezi, hivyo kwa kodi hiyo anatambuliwa kama mfanyabiashara mkubwa hawezi kuuza sawa na mfanyabiashara aliyepo nje ya mji,” amesema.