29.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Mashine za BVR zagoma tena Makambako

Na Michael Mapollu, Makambako
UBORESHAJI wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa kutumia mfumo mpya wa kielekroniki umeingia dosari baada ya baadhi ya mashine zinazotumika kwa ajili ya kazi hiyo kushindwa kufanya kazi.
Kazi hiyo iliingia dosari jana katika Mji mdogo wa Makambako mkoani Njombe ikiwa ni siku ya kwanza ya kuanza uandikishaji huo.
Tatizo hilo lilibainika baada ya mashine nyingi zilizopangwa kufanikisha kazi hiyo kutofanya kazi katika baadhi ya vituo vilivyotengwa kwa ajili ya uandikishaji, huku wataalamu walioteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wakishindwa kuzitumia sawasawa.
Katika vituo vya kujiandikisha vilivyopo Kata ya Mjimwema, Lyamkena, Mwembetogwa na Mlowo, MTANZANIA lilishuhudia msururu mrefu wa wananchi wakiwa wamepanga foleni kwa ajili ya kujiandikisha, lakini walishindwa kutimiza ndoto yao baada ya mashine kushindwa kufanya kazi.
Pia katika baadhi ya vituo uandikishaji ulichelewa kuanza hadi saa saba mchana, huku wananchi wengine wakikata tamaa na kuamua kurudi majumbani.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na MTANZANIA waliilaumu NEC kwa kuendesha uandikishaji huo bila kuwa na maandalizi yoyote hadi kusababisha usumbufu na kupoteza muda, huku mashine nyingine zikishindwa kufanya kazi vizuri.
“Kama vifaa havifanyi kazi vizuri au wataalamu wenyewe wanaonekana hawajapata mafunzo ya kutosha kuweza kutumia mashine hizo, sasa kulikuwa na sababu gani kuanza zoezi hilo leo? Ni kwanini kusiwe na maandizi ya kutosha kwa ajili ya zoezi hili?” alihoji mwananchi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Mwananchi huyo alidai kuwa kituo alichojiandikisha mashine zilizokuwa zikitumika kupiga picha zilikuwa zikitoa picha nyeusi, huku nyingine zikiwa hazionekani kabisa kiasi cha kumfanya mtu asitambulike sawasawa.
Hata hivyo, katika baadhi ya vituo wananchi hawakujitokeza kwa wingi kujiandikisha ambapo hadi saa nane mchana idadi ya waliojitokeza ilikuwa kati ya 15 na 18.
Kutokana na hali hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania bara, John Mnyika, alilalamikia uandikishaji huo, huku akiitaka NEC kurekebisha hali hiyo.
Mkurugenzi wa NEC, Julius Mallaba, amekiri kutokea kwa changamoto hizo, huku akiipongeza Chadema kwa kufuatilia na kubaini kasoro hizo.
Alisema tume yake isingeweza kubaini kasoro hizo kwa urahisi.
Mapema mwaka jana wakati wa uandikishaji wa majaribio katika baadhi ya kata za Manispaa ya Kinondoni, mashine hizi za BVR zilichemsha kwa kupata joto kwa kile kilichoelezwa kuwa mazingira yake hayaendani na hali ya hewa ya Tanzania.
Pamoja na hali hiyo, vyama vya upinzani, hasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimekuwa vikiitaka NEC kuachana na utaratibu wa kutumia mashine hizo na hata kuonyesha hofu ya kukwama na kazi ya uandikishaji kutokwenda kwa wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles