Na VICTORIA GODFREY-DAR ES SALAAM
MCHEZA Kickboxing maarufu nchini, Japhat Kaseba amesema kuwa, ana mpango wa kuandaa mashindano ya vijana ya mchezo huo, ambayo itafanyika baada ya tamko la Serikali la kuruhusu mikusanyiko ya watu, ikiwamo michezo.
Machi 17 mwaka huu, Serikali ilipiga marufuku mikusanyiko ya watu, ikiwa ni tahadhari ya kuepuka kusambaa kwa virusi vya corona.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kaseba alisema lengo ni kuchagua timu ya vijana ambayo itaandaliwa kwa shiriki mashidano ya kimataifa.
“Tayari vijana wapo kutoka mikoa mbalimbali ambao watapata fursa ya kushiriki mashindano hayo,”alisema.
Kaseba alisema kuwa, mpango uliopo ni kuendelea kuhamasisha vijana wengi waweze kujitokeza kujifunza mchezo huo, kutoka katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Alisema kuwa, matarajio yao kuona Tanzania inakuwa na nyota wengi ambao wataitangaza vyema Tanzania.
“Ninatamani sana kuona vijana wanafuata nyayo zangu na kupata warithi wengi zaidi,”alisema Kaseba.