25.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Masheikh waapa kuiadhibu CCM kesho

2NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM.

KAMATI ya Masheikh na Maimamu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wamewataka waamini wa dini ya Kiislamu na Watanzania kwa ujumla kuhakikisha wanampigia kura na kumchagua mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, ili kuweza kuleta mabadiliko ya kweli nchini.

Kauli hiyo ilitolewa jana wakati masheikh hao wakiwajibu wenzao wa Mwanza ambao Oktoba 17 katika kuadhimisha sherehe za mwaka mpya wa Kiislamu walikaririwa wakimtaja Lowassa kuwa ni mdini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Sheikh Said Rico ambaye alikuwa ameongozana na Sheikh Rajab Katimba pamoja na masheikh wengine, alisema Waislamu wanapaswa kuwapuuza masheikh hao kwa kumshambulia mgombea huyo kuwa ni mdini katika kipindi hiki cha uchaguzi  badala ya kutaja matatizo na mafanikio ya Waislamu.

Alisema masheikh hao wameonyesha chuki binafsi kwa Lowassa kwa kuwa amekuwa akichangia harakati za kuuinua Uislamu ikiwa ni pamoja na kuchangia michango mbalimbali misikitini ikiwemo ujenzi wake.

“Waislamu tuna matatizo mengi, masheikh badala ya kuzungumzia hayo wanayaacha na kuanza kumshambulia Lowassa kwa kivuli cha udini…Kesi ya Sheikh Ponda imekuwa ikiahirishwa kila mara sasa hukumu imepangwa kufanywa Novemba 18, tunapenda kuifahamisha Serikali kuwa sisi Waislamu tutatoa hukumu yetu Jumapili Oktoba 25 wakati tutakapokuwa mbele ya sanduku la kura hatuna haja ya maandamano wala kufanya fujo kwa kuhakikisha tunaleta mabadiliko kwa kumchagua Lowassa,” alisema Sheikh Rico.

Alisema msukumo wa kumtaka Lowassa umetokana na fikra mgando na za kibaguzi ambazo zimekuwa zikiendekezwa na chama dola na kuwafanya Waislamu kuwaona hawana jipya tena na kuamua kutaka mabadiliko ya kweli.

“Waislamu twendeni tukampigie kura Lowassa bila woga na sisi tunataka mabadiliko kwakuwa hata Mtume alibadilika kutoka Makka na kwenda Madina,” alisema Sheikh Rico.

Alisema kwa sasa Watanzania hawapaswi kung’ang’ania chama ambacho kinawafanya wanakula mlo mmoja kama kiboko ilihali wana haki ya kula milo mitatu.

Kwa upande wa Katibu wa kamati hiyo, Sheikh Rajabu Katimba, alisema Waislamu ni jamii ya Watanzania wanaopenda amani lakini viongozi wanapaswa kufahamu kuwa amani haiwezi kuwapo bila haki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles