Na Clara Matimo, Mtanzania Digital
Masheikh kutoka Mkoani Mwanza wameungana na Sharifu, Sayyid Jaafari bin Sayyid Muhammad ambaye anatoka katika ukoo wa Mtume Muhammad na kusoma dua kwa ajili ya kuliombea taifa amani na baraka.
Maombi hayo yamefanyika hivi karibuni katika maeneo tofautitofauti Wilaya ya Nyamagana na Ilemela zilizopo mkoani Mwanza yakiongozwa na Sharifu kutoka nchini Kenya ambaye aliongozana na watu watano.
Akiwa mkoani Mwanza Sharifu aliwahamasisha waislamu kupendana, kumpenda Mtume Mohammad na kuyapa heshima yake Matukufu ya Kiislamu.
“Jifunzeni na tendeni mambo aliyoyafundisha Mtume wetu ikiwemo kupendana pia kama una tofauti na mwenzio ziondoe na umsamehe, ishini kwa wema na watu wasio waislamu tiini sheria za nchi bila shuruti mkifanya hivyo mtakuwa mnayaishi mafundisho ya Mtume wetu Mohammad,” alisema Sharifu.
Akizungumza na Mtanzania Digital, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, alisema: “Faida kubwa tuliyoipata waislamu kwa ugeni huu wa Sharifu ni kuwaleta waislamu pamoja, hata kama baadhi yao walikuwa na mitazamo tofauti anapokuja anawaunganisha maana wote wanaamini yeye ni ukoo wa Mtume hakuna muislamu yeyote anayeweza kukwepa kuwa naye.
“Nawausia waislamu wenzangu tuendeleze mapenzi ambayo tumeoneshana kwa siku hizi ambazo Sharifu ambaye ni Mjukuu wa Mtume Mohamed alikuwepo mkoani kwetu hata baada ya kuondoka kwake maana umoja wetu ndiyo unaweza kufanya maendeleo baina yetu tukiwa tumefarakana hatuwezi kufanya maendeleo,”alisisitiza Sheikh Kabeke.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, Alhaji Sheikh Mussa Kalwanyi, aliwaasa watanzania na viongozi wa dini kuendelea kuiombea nchi wakati wote ili amani iliyopo iendelee kudumu.
Kila mwaka Ukoo wa Mtume Mohammad ukiongozwa na Sharifu Mkubwa hutembelea Mkoa wa Mwanza lengo likiwa ni kufanya dua, maombi na kukagua vituo vya kiislamu kwa kuwa kuna maulid za ada ambazo ukoo huo unazisimamia zinazofanyika mkoani humo.
Sharifu na wenzie waliingia Mkoani Mwanza Oktoba 31, 2022, waliondoka Novemba 2, 2022.