Elizabeth Kilindi,Njombe
MASHAHIDI wawili, daktari aliyemtibu pamoja na mwanafunzi mwenzake wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Njombe walivyoshuhudia aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Madeke,Hosea Manga anayedaiwa kuadhibiwa na mwalimu wake wa somo la hisabati na kusababishiwa ulemavu wa uti wa mgongo.
Kesi hiyo namba 141 ya mwaka 2019 ya Jamuhuri dhidi ya Focus Mbilinyi, ikiongozwa na Hakimu Mkazi, Ivan Msaki huku Mwendesha Mashtaka, Elizabeti Mallya wakati upande wa watetezi ukiwakilishwa na mawakili Octavian Mbugari na Innocent Kibadu.
Kesi hii iliendeshwa kwa takribani saa tano imeanza kwa kusikiliza ushahidi kutoka kwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Madeke, Given Nyangwinye ambaye ni shahidi namba tatu aliyekuwa anasoma shule na darasa moja na mlalamikaji Hosea Manga aliyekumbwa na masaibu ya kuvunjika uti wa mgongo.
Akieleza mahakama, Given alidai Machi 21, mwaka huu, mwalimu Focus Mbilinyi alitoa kazi ya somo la hesabu yenye maswali 10,baadae kutoa adhabu kwa waliokosa, huku yeye na wanafunzi wenzake akiwemo Hosea wakipokea adhabu hiyo.
Alidai yeye alikosa hesabu 6 na akatandikwa viboko vitano, huku akishuhudia mwenzake hosea aliyekosa hesabu zote akipewa adhabu ya viboko akiwa amening’inizwa kichwa chini miguu juu.
Kwa upande wa shahidi namba nne, Dk. Silvery Mwesige kutoka Taasisi ya Mifupa (MOI) Idara ya Upasuaji wa Ubongo na Mishipa aliieleza mahakama alianza kumuhudumia Hosea kuanzia mwanzoni mwa Aprili,2017 ambapo baada ya vipimo majibu yalionesha alikuwa na mgandamizo sehemu ya mwisho ya uti wa mgongo hali iliyofanya damu isiweze kufika katika eneo hilo.
Baadaye ukaibuka mvutano wa kisheria kwa mawakili watetezi ambao awali walipinga na kuhoji uhalali wa taarifa ya matibabu kutoka MOI, iliyowasilishwa Dk.Mwesige kwa madai shahidi hakushiriki katika baadhi ya vipimo vya Hosea , pingamizi lililomalizwa na hakimu Msaki, baada ya kutoa uamuzi mdogo na ufafanuzi wa kisheria kubainisha uhalali wa taarifa na vielelezo viliyowasilishwa na Dk.Mwesige.
Dk. Mwesigwe alipoulizwa na upande wa utetezi aliiambia mahakama kuwa hawezi kuthibitisha adhabu ya viboko alivyopewa Hosea inaweza kuwa ndiyo imesababisha tatizo alilonalo hivi sasa lakini amekiri kuwa adhabu ya viboko inaweza kuleta tatizo la kiafya kama la mtoto Hosea kutegemeana na nguvu na nyenzo anayotumia mtoa adhabu.
Shauri hili limeahirishwa na litaendelea kusikilizwa tena disemba 2 mwaka huu.
Mwaka 2017, kesi namba 83 ilifunguliwa na baadae kufutwa kutokana na daktari aliyemtibu Hosea Manga alitoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi licha ya kuitwa mara nane.