31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MASHABIKI SASA KUINGIA UWANJANI KWA MASHARTI

 ZAINAB IDDY – DAR ES SALAAM 

LIGI Kuu Tanzania Bara ikitangazwa kuendelea Juni 13, mwaka huu, mashabiki watakaohitaji kuingia uwanjani watatakiwa kufuata masharti kuzishuhudia timu zao. 

Kwa sasa ligi hiyo itachezwa katika Kituo kimoja cha Dar es Salaam kutokana na hofu ya kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona. 

Ligi hiyo ilisimama Machi 17, mwaka huu, baada ya Serikali kusitisha shughuli za mikusanyiko ya watu, ikiwamo michezo kutokana na kuwapo kwa janga hilo. 

Hata hivyo, Rais John Magufuli ameruhusu michezo kuendelea ikiwamo Ligi Kuu Bara kuanzia Juni mosi, mwaka huu. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo, Jinsia, Wazee na Watoto iliyosainiwa na Ummy Mwalimu na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, imeeleza katika mazingira ambayo watazamaji wataruhusiwa kuingia uwanjani ukaaji utangatie umbali wa mita moja na uvaaji wa barakoa kwa muda wote ndani ya uwanja. 

Taarifa hiyo ilisema kuwa uongozi wa uwanja, vyombo vya dola na wasimamizi wengine wa ligi watapaswa kuwaruhusu watazamaji ambao watakuwa tayari kuzingatia na kutii kanuni za afya, lakini pia kuwachukulia hatua kali watakaokaidi ikiwamo na kuwatoa uwanjani au kuwazui kushuhudia mchezo. 

Ilisema utaratibu wa kuwapima joto wachezaji na viongozi wengine kwa kusimamiwa na madaktari wa timu husika unapaswa kusimamiwa kikamilifu. 

Pia ilisema wachezaji hawataruhusiwa kushangilia kwa kukumbatiana wala kugusana mikono ili kuepuka kupata maambukizi ya virusi vya corona. 

Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almas Kasongo, amesema tayari taarifa ya kurejea kwa Ligi Kuu Bara zimetolewa kwa timu zote. 

Kasongo alisisitiza wachezaji kuchukua tahadhari ya kujikinga na corona. 

“Baada ya kamati kukaa vikao vya mara kwa mara vilivyoanzia Jumatatu ya wiki hii, tumekubaliana ligi kurejea Juni 13 na kumalizika mwanzoni mwa Julai,” 

Tumesisitiza kuzingatia kanuni za afya kama ilivyotakiwa na Wizara ya Afya kwa sababu corona bado ipo,” alisema Kasongo. 

Kasongo alisema wanatarajia kutoa ratiba ya ligi hiyo kesho ili kila timu iweze kujua inaanza kucheza na nani, pamoja na maelekezo mengine. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles