27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MASHA: SIJUTII KUHAMA CCM

masha

Na AZIZA MASOUD- DAR ES SALAAM

ALIYEWAHI kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne, Lawrence Masha, amesema hajutii kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu uamuzi huo alichukua akijua anachokifanya ni sahihi.

Masha aliyehamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati wa kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, alitoa kauli hiyo jana akiwa na kundi la vijana waliokamatwa wakati wa uchaguzi huo walipokutana na Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Edward Lowassa.

Alisema aliamua kuhama CCM baada ya kuona waanzilishi wake akiwemo Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru, kujitoa.

“Mimi hapa hawa ni wazee wangu wameanza mbali, siku zote nasema katika kampeni zote tulizopitia, nikawa najiuliza  Kingunge amehama CCM mimi nabaki kufanya nini, amehama hajasema anahamia Chadema lakini kaona kile si chama cha kuendelea pamoja alikuwa ni sehemu ya waanzilishi wa chama.

“Wakati tulipokamatwa nyinyi ndio mlioniponza nisingefungwa kama msingepiga kelele Oysterbay lakini sijutii, nawaambia usiruhusu mtu binafsi akubadilishe mawazo, wewe kumbuka  sababu iliyokufanya uingie huku na chanzo cha wewe kuwepo hapa,” alisema.

Masha alisema vijana hawatakiwi kukata tamaa kwa sababu mapambano yanayoendelea ni magumu yanahitaji uvumilivu.

“Msikate tamaa tupo pamoja, yanaweza yakawa mapambano ya muda mrefu, mapambano magumu wala tusijali, watajaribu kutufilisi wengine watawaumiza ndugu zetu, tusikate tamaa sisi sote Watanzania tujenge nchi tuliyojengewa na baba zetu si hawa waliokuja kuchukua,” alisema.

Pia alisema alipokuwa waziri aliapa kuilinda Katiba ya nchi na si kumlinda mtu.

“Nilipata bahati kuwa waziri, niliapa kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kiapo ambacho siwezi kukisahau, sijawahi kuapa kukilinda chama wala sijawahi kuapa kumlinda mtu binafsi, nimeapa kuilinda Katiba ya Tanzania.

“Kila siku nikiwaangalia watoto wangu, nasema nitafanya kile ambacho naweza kukifanya mimi kuhakikisha watoto wangu wanakaa katika nchi ambayo I a m very proud of it (nchi ambayo nitakuwa najivunia) wametuibia kura, it’s fine (sawa) na sisi kwa uzalendo tuliokuwa nao badala yake tukanyamaza kuliko kuruhusu nchi iende katika machafuko,” alisema.

Masha alisema watawala wanatakiwa kutambua upinzani waliamua kukubali matokeo na si kwamba wamewanyang’anya ushindi.

“Tumekubali si kwamba wamechukua lakini nawaombeni sana, moyo ambao mmeuonyesha kipindi kile muendelee nao ili kuweza kuliendeleza Taifa,” alisema.

Akizungumzia maisha yake katika Gereza la Segerea alipowahi kulala baada ya kutuhumiwa kufanya vurugu katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Masha, alisema kutokana na umri alionao alikuwa akihudumiwa tofauti na wengine.

“Treatment (huduma) yangu ilikuwa tofauti na nyinyi, nakumbuka walinilazimisha kuchuchumaa nikakataa wakanikubalia, mliona wakati naingizwa ndani kitanda kikawekwa kipya, godoro jipya, shuka mpya,” alisema.

Masha alisema vijana wanapaswa kutambua kuwa katika mapambano yoyote wapo watakaoumia, wengine hawatafika lakini msingi wa mambo yote ni kufanya kazi kwa Watanzania walio wengi.

“Wapo ambao hawaamini kwa wale wanaopenda kusoma, tafuta barua imewahi kuandikwa na mzee mmoja ya Martin Luther King, inaeleza kuwa unatambua kabisa kwamba kitu unachokifanya kinaweza kukuweka ndani.

“Lakini unakifanya kwa sababu unajua kabisa ni sawa, lakini unakifanya ili ukifikishe unapotaka kwenda, kwa nyinyi si rahisi watu wote watatambua mnachotaka kukifanya, mimi nimekaa ndani kuna uwezekano tena mkubwa nikakamatwa nikakaa ndani tena kabla ya mwaka 2020,” alisema.

Kwa upande wake, Lowassa, aliyekuwa pia mgombea urais wa Chadema aliyeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alisema Watanzania ni waoga jambo lililochangia wengi wao kushindwa kulinda kura katika uchaguzi wa mwaka jana.

Lowassa alitoa kauli hiyo jana alipokutana na vijana hao waliokamatwa na kufunguliwa kesi katika mikoa mbalimbali wakati wa uchaguzi huo.

“Tulishinda na tutashinda uchaguzi ujao lakini nataka niwaambie vitu viwili, Watanzania ni waoga sana, sisi ni waoga sana ukimwona polisi anakuja kuangalia kura unakimbia, sasa unamkimbia polisi kwanini usilinde kura yako,” alisema.

Lowassa alisema pamoja na kukumbana na misukosuko, vijana hawatakiwi kukata tamaa kwa sababu bado wana kazi kubwa ya kufanya.

“Nimewaita kuwaambia asanteni na poleni sana, nimefurahi kila mmoja anaeleza alivyofurahia maisha ya mahabusu, nawapongeza sana kwa moyo huo, nawashukuru sana.

“Najua mmejifunza mambo mengi lakini mnapaswa muyahifadhi hayo ni mafanikio, mnapaswa mjue mnayatumiaje hayo tuliyozungumza msikate tamaa, tuna kazi ya kufanya kwa hayo mliyoyaongea tunachukulia kama changamoto,” alisema.

Naye Mzee Kingunge alisema anaamini mapambano ni kitu kinachodumu katika dunia ya binadamu na kwamba maelezo waliyoyatoa vijana hao ni wazi kuwa kundi hilo limejitolea kupambana.

“Hili darasa nimejifunza kwamba wapo vijana wameamua kupambana, katika dunia ya binadamu kitu ambacho kinadumu ni mapambano, mazingira yote mnayoyaona katika nchi yetu, za wenzetu kote ni matokeo ya mapambano ya binadamu.

“Binadamu ni mpambanaji haya yote ni mapambano ya binadamu, kama kuna watu wanawaza watapata mema katika dunia hii kwa kupewa tu na Mungu ama na shetani ama na miujiza fulani watu hao wamepotea, kila kitu kinatolewa kwa mapambano sasa na nyinyi mnapambana, sisi tulianza tukiwa sekondari,” alisema.

Kingunge alisema mapambano ya kusaka Uhuru kutoka katika mikono ya wakoloni waliyaanza wakiwa sekondari na walifanikiwa kwa sababu waliamua  kujitolea na kujitoa mhanga.

“Sisi tulijitoa mhanga, wengi walimaliza shule wakaacha kufanya kazi na kujiunga na Tanu kwenda kufanya kazi, haikuwa rahisi watu wengi walitusaliti tuligombana na wazazi wetu, sasa na nyinyi mnapambana katika mazingira haya,” alisema.

Pia alisema mapambano yanahitaji watu wenye moyo wa ujasiri na kwamba hakuna mafanikio bila mapambano.

Alisema mapambano ya vijana wa sasa yanaweza yakaonekana magumu tofauti na waliyokuwa enzi za ukoloni kwa sababu ya kubadilika kwa mazingira.

“Utawala wa kikoloni pamoja na kuwa wanyonyaji, Waingereza hawakuwa wanapenda siasa lakini walikuwa na utamaduni wao, wale walikuwa wastaarabu, tatizo la tawala zetu si wastaarabu, hawaheshimu sheria wala Katiba zao, mtatendewa vibaya na muwe tayari kukabiliana nayo, ”alisema.

Kingunge alisema Chadema inakubalika pamoja na Lowassa, lakini hawawezi kushinda uchaguzi kama hawatapiga kelele kuhakikisha yanafanyika mabadiliko katika vitu viwili kabla ya mwaka 2020.

“Tunapaswa kuhakikisha tunapata Tume Huru ya Uchaguzi pamoja na sheria inayoruhusu matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani, Katiba inapaswa iseme  tusipofanya hivyo tutakuwa na matatizo makubwa na tusahau habari za upinzani kushinda,” alisema.

Kingunge alisema wapinzani wanapaswa kuhakikisha wanapata Katiba mpya ama kusimamia baadhi ya vipengele katika Katiba kuhakikisha vinabadilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles