24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Maseneta wanapowaweka katika wakati mgumu magavana

ISIJI DOMINIC

KWA wiki kadhaa sasa, magavana wamejikuta katika wakati mgumu kujibu maswali yanayohusu matumizi ya fedha yaliyotengewa kaunti zao kutoka kwa Kamati ya Bunge la Seneti ya Hesabu za Serikali (PAC).

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeonesha namna baadhi ya magavana wanavyotumia vibaya fedha za umma wakati huo huo wakihitaji Bajeti zao kuongezwa. Jukumu la kuwahoji kwa mujibu wa Katiba lipo chini ya maseneta.

Hali hiyo ya magavana kuwekwa kitimoto ilisababisha Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), Wycliffe Oparanya, kuhamasisha magavana wenzake kutohudhuria vikao vya seneti vinavyohoji matumizi ya fedha ambayo ripoti ya CAG imegundua imegubikwa na dosari nyingi.

PAC ya Seneti imeionya CoG kuacha kuingilia jukumu la maseneta kwa mujibu wa Katiba kuhakikisha matumizi ya fedha katika kila kaunti yanatumika ipasavyo.

Mwenyekiti wa PAC, Moses Kajwang’, alisema CoG ni mgeni katika ukaguzi wa fedha za umma na kwamba gavana yeyote atakayeshindwa kujitokeza mbele ya Seneti atabeba msalaba wake mwenyewe.

“Ninamwambia Oparanya aache kuhamasisha magavana kwa sababu CoG haina mamlaka kukagua fedha za umma na pia nawasisitizia magavana wasipotoshwe na Oparanya kwa sababu sheria itachukua mkondo wake,” alisema Kajwang’.

Kauli ya Kajwang’ iliungwa mkono na Seneta wa Migori, Ochillo Ayacko, ambaye alitaka magavana na maofisa wa kaunti kukaguliwa mali zao (lifestyle audit).

“Ufisadi umeingia kwenye kaunti hivyo kuna umuhimu wa ukaguzi wa mali jambo ambalo litahakikisha matumizi mazuri ya fedha za umma,” alisema Ayacko.

Kinachofanywa na PAC ya Seneti ni jambo muhimu katika kupambana na vita dhidi ya ufisadi na pia inawapa nafasi magavana kuthibitisha kwa Wakenya kwamba wanao uwezo kuelezea hiyo fedha ndogo ambayo kaunti inapata imetumikaje na imemnufaisha vipi mwananchi wa kawaida.

Lakini namna PAC ya Seneti imekuwa ikiwabana magavana imezua maswali mengi huku ikidaiwa ni kutunishana misuli hususani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022. Magavana wamekuwa wakiwaambia maseneta kwamba wao wanawawakilisha wananchi wa kaunti zao kwa kufanya vikao vyao jijini Nairobi wakati ambaye yupo karibu na wananchi kila siku kuhakikisha huduma stahiki zinawafikia ni wao magavana.

Aidha majibizano makali katika vikao vya kukagua matumizi ya fedha za umma kwa mujibu wa ripoti ya CAG inaelezwa ni mojawapo ya mbinu inayotumiwa na maseneta kuwadhalilisha magavana ili uchaguzi mkuu utakapofika wao (maseneta) wawanie nafasi za ugavana.

Wakenya wameshuhudia katika vikao hivyo namna seneta wa kaunti anavyoweza kumbana gavana wake ukizingatia wote wanatoka chama kimoja. Mathalani, Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui, alijikuta katika wakati mgumu alipobanwa na Seneta wa kaunti hiyo, Susan Kihika, licha ya wote kuchaguliwa kwa kura nyingi kupitia Chama cha Jubilee.

Ni dhahiri vita kati ya Kinyanjui na Kihika ni ya kupata umaarufu kisiasa huku wakiikodolea macho nafasi ya ugavana 2022. Chochote anachofanya gavana kimepata upinzani kutoka kwa seneta. Hivi karibuni, Kinyanjui alinunua basi mbili zitumike na shule, makundi ya jamii na wafanyakazi wa kaunti akisisitiza shule za umma zimekuwa zikihangaika kununua mabasi na kushindwa kumudu mahitaji muhimu ya masomo.

Uamuzi huo ulipingwa vikali na Kihika akisema hayo ni matumizi mabaya ya fedha za umma badala ya fedha zilizotumika kutatua mahitaji muhimu ya wananchi wa Nakuru akitolea mfano wa ukarabati wa barabara eneo Bunge la Kuresoi Kusini na Kaskazini au kununua dawa zitakazotumika hospitalini.

Hali kama hiyo pia inashuhudiwa kaunti ya Nandi kati ya Gavana, Stephen Sang na Seneta, Kiprotich Cherargei, licha Naibu Rais William Ruto kuwapatanisha. Wawili hawa wamekuwa wakishambuliana hadharani kuhusu ufisadi na tuhuma nyinginezo zinazohusu uendeshwaji wa kaunti.

Huko Trans Nzoia tofauti zipo kati ya Gavana, Patrick Khaemba na Seneta, Michael Mbito, ambapo seneta huyo anamtaka gavana aeleze miradi iliyokwama ikiwamo hospitali na vituo vya basi huku pia akishutumu staili yake ya uongozi akisema anafanya kazi kwa kujitenga.

Mvutano huu kati ya magavana na maseneta ukilenga zaidi uchaguzi mkuu ujao unarudisha nyuma utekelezaji wa miradi ya maendeleo na zile agenda nne kuu za Rais Uhuru Kenyatta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles