23.9 C
Dar es Salaam
Friday, September 30, 2022

MARUKUFU KUTOA TALAKA KWA SIMU

Na SALUM VUAI,ZANZIBAR


WAZIRI wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Moudline Castico, amekemea tabia ya baadhi ya wanaume kuwataliki wake zao kupitia ujumbe wa simu.

Akizungumza na wanachama wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) katika Tawi la Kiembesamaki Unguja, Waziri Castico alisema kitendo cha kutaliki mke kwa ujumbe wa simu (SMS) ni dharau na udhalilishaji.

Waziri huyo alieleza masikitiko yake kwamba baadhi ya wanaume wanaofanya hivyo ni wale waliowezeshwa na wake zao wanaojituma, ambapo hali za waume hao zilikuwa duni wakati wakioana.

Alisema wapo wanaume wanaosaidiwa kujenga nyumba na hata kununuliwa magari na wake zao, lakini hatimaye wanawatoa thamani na kuwanyanyasa baada ya kupata wanawake wanaowaona ni wazuri zaidi.

Alieleza kuwa jambo baya zaidi ni kuacha kuwashughulikia watoto kwa kuwanyima huduma na matunzo hali inayowasukuma kuzurura mitaani na kuingia katika ajira mbaya na kusababisha wafanyiwe vitendo vya udhalilishaji.

“Dini zote zinaitambua ndoa kuwa ni kitu cha heshima na ina maadili yanayopaswa kufuatwa na watu wanaoamua kushirikiana kimaisha.

“Hata hivyo, iwapo kunatokezea sababu ya wanandoa kutengana, lazima waachane kwa wema, heshima na mafahamiano ili ihsani waliyokuwa nayo wakati wakiwa pamoja iendelee na hasa wanapokuwa wamejaaliwa kupata watoto.

“Kuacha kuna taratibu zake, akina baba mnapowapenda wake zenu muwe na busara, mnapoanza pamoja lazima muende pamoja kama unavyombembeleza siku ya kwanza.

“Sio kashakuchumia mali zako, ushakuwa na uwezo, kakununulia kigari unampelekea talaka kwenye simu,” alisisitiza waziri Castico.

Katika hotuba hiyo pia Castico aliwanasihi wanawake kuwa waaminifu kwenye ndoa zao hata pale waume zao wanapokengeuka, badala ya kutaka kulipa kisasi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mahmoud Thabit Kombo alisema wanawake wanapaswa kuengwaengwa kama mboni ya jicho badala ya kuwanyanyasa kwani daraja yao kwa Mwenyezi Mungu ni kubwa.

“Bila ya msaada, nguvu na imani ya mwanamke, wanaume wasigeweza kupata mafanikio wanayojivunia katika maisha yao, hivyo lazima waoneshe shukurani kwao kwa kuwatunza na kuwapa heshima wanayostahiki.

“Wanawake ni mama zetu sote tunaujua uzito wa kubeba mimba na uchungu wa uzazi ambapo wakati wa harakati za kujifungua, mama anakuwa baina ya uhai na kifo, tutafute pepo kwa kuwa tunza mama zetu,” alisema.

Thabita mbaye pia ni Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, aliwaahidi wanachama wa UWT pamoja na wanawake wengine wa Kiembesamaki kuwa wataendelea kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayowakabili hatua kwa hatua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,298FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles