Na Hadija Omary, Lindi
KIONGOZI wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2021, Luten Josephine Mwambashi amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, Hashim Komba kutotumia Wahandisi wa kubabaisha katika miradi ya maendeleo badala yake watumie wahandisi wazoefu ili kuleta tija.
Luten Mwambashi ametoa agizo hilo mapema leo Agosti 25, 2021 baada ya mbio za mwenge wa Uhuru kufika katika Hospital ya wilaya ya Nachingwea kwa lengo la kuzidu mradi wa jengo la wodi ya kisasa ya uzazi.
Amesema ili kuleta tija kwa wananchi katika miradi mikubwa kama hiyo inayotekelezwa na halmashauri ni vyema Wahandisi wanaotumika wakawa ni wataalamu wa kazi hiyo na sio kuokota okota ambapo hupelekea miradi hiyo kutokuwa na tija iliyokusudiwa.
“Serikali yetu inatujali na inaleta miradi kila kukicha sasa kama wahanidi wenyewe tulionao ni hawa ambao niwakubahatisha kila siku tutakuwa tunagombana katika hii miradi kwa maana itakuwa inaenda ndivyo sivyo,” amesema Luteni Mwambashi.
Amesema pamoja na kwamba amekubali kuzindua jengo hilo lakini alichukuwa muda mrefu kukagua nyaraka mbali mbali ili kujiridhisha thamani ya pesa iliyotumika pamoja na kengo lenyewe.
“Nilichogundua ni kwamba wilaya hii inachangamoto ya mainjinia na ndicho kilichotuchelewesha, hakuna injinia anaeweza kusimamia miradi mikubwa kama hii ya maendeleo,” amesema.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mganga mkuu wa wilaya hiyo, Charles Mtabo alieleza kuwa mradi huo hadi kukamilika kwake umegharimu kiasi cha Sh 474,946,758 ambapo kiasi cha Sh milioni 400 zilitolewa na Serikali Kuu na Sh milioni 74.946 ni kutoka Halmashauri ya wilaya.
Mtabo almesema jengo hilo la wodi ya wazazi limegawanyika katika maeneo tofauti tofauti ambayo ni eneo la mama kusubiri kabla ya kujifungua, sehemu ya kujifungulia, chumba cha upasuaji, sehemu ya waliojifungua bila upasuaji, sehemu ya waliojifungua kwa upasuaji na sehemu ya watoto waliozaliwa kabla ya muda (njiti).
Hata hivyo Mtabo alibainisha kuwa ujenzi wa mradi huo umemaliza kabisa changamoto ya uchache wa vyumba uliokuwepo kwenye wodi ya uzazi ya zamani ambapo wodi hiyo ya zamani ilikuwa na vyumba 9 bafu 3 na vyoo vitatu huku wodi mpya ya sasa ina vyumba 30, vyoo na bafu 10 na vyoo 11.
Ametaja manufaa mengine ya mradi huo kuwa ni kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga vinavyosababishwa na matatizo ya uzazi pamoja na kuimarisha usiri kwenye vyumba vya kujifungulia ukilinganisha na vyumba vilivyokuwa vinatumika kwenye wodi ya zamani.
Naye Mariamu Saidi ni mkazi wa Wilaya hiyo ya Nachingwea amesema kuwa anaishukuru serikali kwa kuwajengea wodi mpya katika hospital yao ya wilaya kwani itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa maambukizi ya magonjwa kutokea kwa mgonjwa mmoja hadi Mgonjwa mwingine kutokana na Msongamano uliokuwepo kwenye wodi ya zamani.
“Kutokana na uchache wa vyumba katika wodi yetu ya wazazi ilikuwa inatulazimu akina mama wengi kurundikana kwenye hizo wodi chache jambo ambalo ni hatari kwa afya zetu kama wazazi na hata kwa watoto tunao wazaa ni rahisi kupata maambukizi ya magonjwa,” alisema Mariamu.