Na Jeremia Ernest, Mtanzania Digital
MWANAMITINDO nguli nchini, Martn Kadinda, ameshinda tuzo ya ‘Internetion Fashion Desgner 2022‘ katika tamasha la Ghana Merit Award lililofanyika June10, nchini Ghana.
Hii ni tuzo ya tano ya Kimataifa kwa Mbunifu huyo ambapo mwaka 2018 alipata pia tuzo ya mbunifu bora wa nguo za kiume kutoka nchini Nigeria na tolea bora la Kiafrika mwaka 2019 katika jukwaa la Durban Fashion Fair Afrika Kusini.
Akizungumza na Mtanzania Digital baada ya kupokea tuzo hiyo, Kadinda amesema anafurahi kuona ulimwengu unafatilia kazi zake na kuahidi kuendelea kufanya vizuri.
“Nina furaha kwa sababu malengo yangu ya kuonyesha uwezo wangu duniani yanazidi kufanikiwa siku hadi siku, ni washukuru wandaaji wa tuzo hizi niwaombe waendelee kuandaa kwa sababu inatupatia motisha ya kufanya kazi nzuri kila kukicha,” amesema Kadinda.
Ameongeza kuwa ataendelea kufanya kazi yake kwa bidii na kuwataka wabunifu wengine kutokata tamaa ya kufanya kazi nzuri kwa sababu matunda anayo vuna leo ni matokeo ya kazi aliyoifanya miaka 10 iliyopita.
Nae Mwakilishi wa tamasha hilo, Michael Lincoln, aliyemkabidhi tuzo hiyo amesema Tanzania ni moja ya nchi inayofanya vizuri katika tasnia ya mitindo barani Afrika.
“Tanzania ni nchi ambayo wabunifu wake wanafanya kazi nzuri ndiyo sababu utaona tuzo zaidi ya mbili zimekuja Tanzania na zote ni kutoka katika vipengele vikubwa,” amesema Loncoln.